IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Mahudhurio ya wananchi katika uchaguzi ujao yatatoa pigo kwa adui

20:40 - January 09, 2012
Habari ID: 2254230
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amehutubia mkutano mkubwa wa maelfu ya watu uliojumuisha maulamaa, wanafunzi na matabaka mbalimbali ya wananchi wa mkoa wa Qum waliokwenda kuonana naye na kusema kuwa, tukio muhimu la tarehe 19 Dei katika mji wa Qum lilikuwa mwanzo wa historia ya mabadiliko ya sasa ya dunia.
Ameashiria mchango wa subira na kuwa makini katika mafanikio ya siku zote ya utawala wa Kiislamu wa Iran na kubainisha sababu mbili muhimu za kufeli njama za maadui na kustawi kwa nguvu na uwezo wa taifa la Iran ambazo ni kusimama kidete Mfumo wa Kiislamu hapa nchini katika misingi yake na mahudhurio ya wananchi katika medani mbalimbali. Amesisitiza kuwa, kinyume na dhana na uchambuzi wa kambi ya ubeberu, utawala wa Jamhuri ya Kiislamu hii leo hauko katika mazingira kama yale ya Waislamu wa awali waliozingirwa katika pango la Shiib Abi Twalib, bali uko katika mazingira yanayoshabihiana na yale ya (vita vya) Badr na Khaibar, na kwa rehema zake Mwenyezi Mungu mahudhurio ya wananchi katika uchaguzi ujao wa Bunge ambayo ni dhihirisho la kushirikishwa katika kujiamulia mambo ya nchi yao, yatakuwa makubwa na kutoa pigo kwa adui. Ameongeza kuwa viongozi na wagombea katika uchaguzi huo pia wanawajibika kutayarisha mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi sahihi na wenye ushindani kwa kuheshimu sheria kikamilifu.
Katika mkutano huo ambao umefanyika sambamba na siku ya kukumbuka tukio la harakati ya wananchi wa Qum hapo tarehe 19 Dei mwaka 1356 (9 Januari 1978), Ayatullah Khamenei ameitaja harakati hiyo ya wananchi wa Qum kuwa ilikuwa cheche katika anga ya mbinyo na ukandamizaji mkubwa ya kipindi cha utawala wa kidhalimu wa kifalme hapa nchini. Ameongeza kuwa harakati hiyo ilikuwa mwanzo wa matukio mbalimbali ya baada yake na silsila ya vikao vya arbaini hapa nchini. "Kwa hakika tukio la tarehe 19 Dei huko Qum lilitayarisha uwanja mzuri wa kutokea Mapinduzi ya Kiislamu, kusimama kidete wananchi wa Iran, kuvunjwa haiba bandia ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, kulifanya taifa la Iran kuwa kigezo cha kuigwa na hatimaye kuanzisha mwamko wa Kiislamu na matukio mengine muhimu katika eneo hili", amesisitiza Kiongozi Muadhamu.
Ameitaja "subira na kuwa makini" kuwa ni sababu mbili muhimu za kuendelea mafanikio na ushindi wa mataifa mbalimbali. Amesema kuwa taifa la Iran limeyaonesha mataifa mengine tajiriba na uzoefu mkubwa wa mafanikio yaliyotokana na subira na kuwa makini.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuwa makini kuna maana ya kutopoteza njia, lengo na kutojiendea ovyo, na subira inamaanisha kusimama imara kwa mataifa kizazi baada ya kingine katika njia sahihi, na kazi kubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba yamewawezesha wananchi wa Iran kulinda mambo hayo mawili katika kipindi chote cha zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Ayatullah Khamenei amesema kazi ya kuimarisha subira na umakini na kudumishwa mafanikio na uwezo wa taifa la Iran mbele ya dhulma na tabia ya kupenda kujitanua ya kambi ya kufru na istikbari inahitajia mambo mengine mawili. Amesema kuwa kusimama kidete kwa mfumo mzima wa Kiislamu juu ya misingi na kutopotoka na kuachana na misingi hiyo na vilevile mahudhurio yanayoambatana na maarifa ya wananchi katika medani mbalimbali vimezima njama na vitimbi vyote vya adui.
Ameashiria njama kubwa za kambi ya ubeberu ikiongozwa na Marekani na Wazayuni kwa ajili ya kudhoofisha masuala hayo mawili na akasema kuwa, licha ya njama zote hizo lakini mambo hayo mawili bado yapo na yataendelea kuwapo kwa baraka zake Mwenyezi Mungu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kama mambo hayo yangetengana, basi kungetokea dosari katika mafanikio ya Mfumo wa Kiislamu hapa nchini, kwani lau kama viongozi na maafisa wa utawala watakuwa na azma kubwa lakini wananchi wasijitokeze katika medani, hakuna kazi itakayofanyika; kama ambavyo lau viongozi na maafisa wa utawala watapatwa na hali ya kutetereka, basi hali hiyo ingekuwa na taathira mbaya katika kuelewa na katika kuchukua maamuzi mbele ya jeshi la kufru na upotofu, na utawala wa Kiislamu ungepata pigo na hatimaye wananchi wangeondoka katika medani mbalimbali.
Ayatullah Khamenei ameashiria mwenendo wa kambi ya ubeberu wa kutumia njia na mbinu zote kwa ajili ya kutia dosari na kuteteresha irada na azma ya viongozi na kuwavunja moyo wananchi na akasema kuwa, viongozi wa Kimagharibi wanakariri mara kwa mara kwamba lengo la vikwao vyao dhidi ya Iran ni kuwachosha wananchi na kuwaondoa katika medani na vilevile kuwalazimisha viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu wabadilishe misimamo yao; hata hivyo viongozi hawa wa nchi za Magharibi wanakosea na kamwe hawatafanikiwa katika lengo hilo, kwa sababu viongozi hawa waovu weliokosea mahesabu wanadhani kwamba utawala wa Kiislamu hapa nchini uko katika mazingira yanayoshabihiana na yale ya kipindi Waislamu walipokuwa wamezingira na washirkina wa Makka katika pango la Shiib Abi Twalib, ilhali taifa la Iran hii leo liko katika mazingira kama yale ya kipindi cha vita vya Badr na Khaibar.
Amesema kuwa katika kipindi cha sasa ambapo taifa la Iran limepata mafanikio mengi na linashuhudia dalili za ushindi na mafanikio mapya, kambi ya ubeberu inafanya juhudi za kuvuruga njia yake na kuwaondoa wananchi katika medani kwa kuwatishia kwa vikwazo wananchi na viongozi. "Taifa la Iran limechagua njia hii yenye fahari kwa maarifa na limefanya jitihada kubwa na kutoa wahanga wengi kwa ajili ya njia hii", amesisitiza Ayatullah Khamenei.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa harakati ya kudumu ya taifa la Iran katika njia ya kuelekea kwenye vilele vya mafanikio haiwezi kusimama. Amesema kuwa adui anakusudia kuvuruga irada ya azma ya wananchi na viongozi katika kipindi ambacho uwezo na nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu kwa sasa haiwezi kulinganishwa na kipindi cha miaka 20 au 30 iliyopita, na udhibiti wa kidhahiri wa kambi ya ubeberu katika miaka iliyopita pia unadhoofika na kunyon'gonyea siku baada ya siku.
Ayatullah Ali Khamenei ameongeza kuwa irada na azma ya viongozi kwa ajili ya kusonga mbele katika njia ya Allah, dini na ufanisi wa dunia na Akhera ni imara, na wananchi daima watakuwa pamoja na harakati hiyo kubwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema uchaguzi ni miongoni mwa medani za kudhihirisha mahudhurio ya wananchi. Ameongeza kuwa tangu muda mrefu huko nyuma vituo na ofisi kuu za jeshi la kambi ya kufru na ubeberu hadi majeshi ya kawaida ya kambi hiyo ndani na nje ya nchi vimekuwa vikifanya njama kubwa za kupunguza mahudhurio ya wananchi katika uchaguzi ujao wa Bunge hapa nchini, lakini kwa baraka zake Mola mahudhurio hayo yatakuwa makubwa na kutoa dharba kubwa dhidi ya maadui.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa uchaguzi utaleta nishati na kutia damu mpya katika mwili wa utawala wa Kiislamu hapa nchini. Ameongeza kuwa medani ya uchaguzi ina baadhi ya matatizo licha ya sifa hizo zote muhimu na chanya, na kwa sababu hiyo tunapaswa kuwa macho ili matatizo hayo yasijitokeze.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa uchaguzi wa Rais wa mwaka 1388 (2009) ulikuwa na kumbukumbu nzuri na mbaya na kusisitiza kuwa kumbukumbu nzuri zaidi ya uchaguzi huo ni mahudhurio makubwa na ya kustaajabisha ya wananchi milioni 40 katika zoezi la kupiga kura, na kumbukumbu mbaya zaidi ni ile ya mivutano ya kisiasa ya baadhi ya watu wasiokuwa safi, majahili na baadhi yao ambao walikuwa maadui katika uchaguzi huo.
Amesema katika uchaguzi wowote ule yumkini kukawepo malalamiko ya baadhi ya watu lakini sheria imeainisha njia ya utatuzi katika hali kama hii; hata hivyo katika uchaguzi wa mwaka 2009 baadhi ya watu walikhitari njia ya kuvunja sheria, kusababisha hasara kwa nchi na wananchi na kuwafurahisha maadui na kutekeleza mipango yao lakini waliambulia patupu, kwa sababu wananchi walikuwa katika medani, na wakati wowote taifa linapokuwa katika medani hakuna mtu anayeweza kufanya mambo yanayokwenda kinyume cha sheria.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja matukio ya baada ya uchaguzi wa Rais wa mwaka 2009 kuwa yalikuwa tajiriba na somo na kuongeza kuwa, uchaguzi ni kielelezo cha mahudhurio ya wananchi na matokeo yake ni dhihirisho la matakwa na rai za wananchi, na watu wote wanapaswa kuyaheshimu.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya udharura wa kufanyika uchaguzi sahihi na wenye ushindani na kuongeza kuwa ushindani hauna maana ya uhasama na kutuhumiana, au mtu kuthibitisha dhati yake na kuwafutilia mbali wengine. Vilevile uchaguzi si kutoa ahadi zinazokiuka sheria kwa ajili ya kuwavutia wananchi.
Amewataka pia maafisa husika na wagombea kuheshimu sheria na masharti ya uchaguzi sahihi na kusema kuwa, wasimamizi wa uchaguzi kuanzia Wizara ya Mambo ya Ndani, Serikali na Baraza la Kulinda Katiba, wanapaswa kufanya jitihada kubwa za kulinda kura za wananchi na kusimamia uchaguzi sahihi; na watu wote wanapaswa kuelewa kwamba hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha chaguzi sahihi zaidi ya 30 zilizofanyika hapa nchini katika kipindi cha miaka 32 iliyopita na kusema kuwa, katika chaguzi mbalimbali zilizofanyika katika kipindi cha uhai wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) au baada yake hakuna uchaguzi ambao haukuwa sahihi au matokeo yoyote yaliyobadilishwa, bali matokeo yote yaliakisi raia na chaguo la wananchi.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia baadhi ya masuala yanayohusiana na wagombea wa uchaguzi ujao wa Bunge hapa nchini na kuwataka wananchi wote kuyatilia maanani. Amesema wagombea wanawajibika kuingia katika medani ya zoezi hilo kwa lengo la kutoa huduma, kwani mtu atakayeingia katika medani hiyo kwa shabaha ya kupata madaraka na nguvu, kupata utajiri au sababu nyingine zisizokuwa sahihi hatakuwa ametoa huduma kwa wananchi na nchi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja mahusiano ya wagombea na vituo vya utajiri na madaraka kuwa ni jambo lenye uharibifu mkubwa na kusema kuwa hii ndio mbinu inayotumika katika demokrasia ya dunia ya sasa hususan huko Marekani ambako wagombea katika chaguzi mbalimbali huingia katika zoezi hilo kwa himaya na misaada ya kifedha ya makampuni, mashirika na matajiri na baada ya kushinda uchaguzi huwa wadaiwa wa makampuni na matajiri hao, na badala ya kuhudumia wananchi na taifa hutunga sheria zinazolinda maslahi ya wenye madaraka na utajiri.
Ayatullah Khamenei amekutaja kuitumia mali ya umma katika uchaguzi kuwa ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kufuatiliwa sana na wananchi. Amesema kutumia mali ya umma katika uchaguzi kuna matatizo makubwa zaidi. Vilevile amewataka wananchi kuwa makini katika kuchagua wagombea mbalimbali na akasema kuwa kuna njia mbili za kuweza kuainisha vyema ambazo ni ama mtu kufanya uchunguzi yeye mwenyewe kuhusu wagombea mbalimbali au kuuliza watu ambao ni huja baina ya mtu na Mungu wake.
Vilevile ameelezea matumaini yake kwamba kwa rehema zake Allah mahudhurio makubwa ya wananchi na kuchagua kwa njia sahihi kutapelekea kuundwa Bunge lenye hadhi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei ameutaja uchaguzi ujao wa Bunge hapa nchini pia kuwa una umuhimu na taathira kubwa kwa mataifa ya Kiislamu na kuongeza kuwa vyombo habithi vya ubeberu ikiwemo Marekani, Uingereza, Wazayuni na wengineo wanafanya juhudi za kuchafua uchaguzi huo na kuyavunja moyo mataifa mengine.
Amesisitiza kuwa taifa la Iran limekuwa mbele ya mataifa yote katika masuala ya uchaguzi na ya kimapinduzi na hapana shaka kwamba mataifa mbalimbali yatafuatilia uchaguzi ujao hapa nchini kwa makini. 932083




captcha