IQNA

Ayatullah Khamenei:

Mwamko wa Kiislamu hautambui Shia au Suni

22:47 - January 30, 2012
Habari ID: 2265193
Ayatullah Khamenei amesema kuwa miongoni mwa mbinu chafu zinazotumiwa na maadui ni kuzusha hitilafu katika umma wa Kiislamu. Amesema kuwa harakati ya mwamko wa Kiislamu haiwahusu Shia na Suni bali wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu wamejitosa katika medani ya mapambano kwa umoja na mshikamano.
Mamia ya vijana kutoka nchi 73 duniani wakiwemo vijana kutoka Misri, Tunisia, Libya, Lebanon, Yemen, Bahrain na Palestina asubuhi ya leo Jumatatu wamekutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika anga ya kimaanawi na iliyojaa hisia za Kiislamu na kimapinduzi.
Baada ya hotuba zilizotolewa na wawakilishi wa vijana wa nchi mbalimbali za Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei amehutubia hadhara hiyo akisema kuwa harakati ya mapambano ya mataifa ya Kiislamu dhidi ya tawala za kidikteta na tegemezi ni jambo lenye baraka nyingi na umuhimu mkubwa na ni utangulizi wa harakati ya mapambano dhidi ya udikteta wa kimataifa wa kanali fasidi na ovu ya Kizayuni na kibeberu. Ameongeza kuwa katika upeo wa wazi wa harakati hiyo yenye baraka, umma wa Kiislamu utarejea tena katika kilele cha heshima, uhuru na nguvu.
Mwanzoni mwa mkutano huo Bwana Dhiyauddin Moro ambaye ni miongoni mwa vijana wanamapinduzi wa Tunisia amezungumzia sifa za mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo ambayo ilikuwa ya kwanza kufanya mapinduzi katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kusema mapinduzi hayo yalijitegemea na kuongozwa na wananchi na hakuna kundi lolote la kisiasa lililokuwa na nafasi katika kutokea kwake.
Amesisitiza kuwa kung'olewa madarakani serikali ya Bin Ali si mwisho wa harakati hiyo ya wananchi wa Tunisia na kusema wananchi wa nchi hiyo wanasisitiza juu ya kutimizwa malengo ya mapinduzi na vijana wanamapinduzi wanaitambua kadhia ya Palestina na kukombolewa kwake kuwa ndio kadhia kuu ya mapinduzi yao.
Bwana Dhia al Sawi kutoka Misri pia amehutubia hadhara hiyo akiashiria baadhi ya tetesi na propaganda zinazotolewa kuhusu utambulisho wa mapinduzi ya wananchi wa Misri na kusema kuwa wananchi wa Misri walianza mapinduzi yao katika misikiti wakitoa nara za "Allahu Akbar", kaulimbiu za Kiislamu na nara za kupinga Uzayuni. Ameongeza kuwa lengo la mapinduzi ya Misri halikuwa kupata uhuru na uadilifu wa kijamii pekee bali lengo la mwisho ni kujitawala kikamilifu na kujiondoa katika makucha ya kuwa mshirika wa Marekani na Uzayuni.
Dhia al Sawi amesema kuwa kuung'oa madarakani utawala wa Hosni Mubarak ilikuwa hatua ya kwanza ya mapinduzi ya wananchi na Wamisri wameazimia kukamilisha malengo yote ya mapinduzi yao ikiwa ni pamoja na kufutwa mkataba wa kuaibisha wa Camp David na kusafisha kabisa mabaki ya utawala wa zamani.
Kijana mwingine aliyehutubia hadhara hiyo alikuwa Abdullah Abduh Allaw aliyewakilisha vijana wanamapinduzi wa Yemen. Allaw ameashiria msukumo wa Kiislamu katika mapinduzi ya wananchi wa Yemen na akasema kuwa: "Tumekuja katika Iran ya sayansi na teknolojia, Iran ya ustawi na Iran ya mapambano na kusimama kidete ili tufaidike na uzoefu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na Marekani, dhulma na udikteta."
Bwana Ahmad Hassan Hajiri, kijana mwanamapambano wa Bahrain pia amehutubia hadhara hiyo na kusoma mashairi yaliyobainisha hisia safi na za kimapinduzi za wananchi wa Bahrain na jinsi vijana na mashahidi wa mapinduzi hayo walivyoachwa peke yao.
Mzungumzaji aliyefuatia alikuwa Muhammad Ali Muhammad Awadh wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas). Muhammad Awadh ameashiria kuwa suala la Palestina limepewa kipaumbele katika Mkutani wa Kimataifa wa Vijana na Mwamko wa Kiislamu na akasema ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kutangazwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds kumetia damu mpya katika harakati ya kupigania malengo ya Palestina.
Kwa upande wake Khalid al Salim mwakilishi wa vijana wanamapinduzi wa Libya ameyataja mapinduzi hayo kuwa yalikuwa mapinduzi ya "Takbira". Amesema mapinduzi ya Libya yalianza kwa takbira na yataendelea kwa takbira. Amesisitiza juu ya udharura wa wananchi wa Libya kustafidi na uzoefu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kukabiliana na Marekani na akaongeza kuwa mapinduzi ya wananchi wa Libya yanashabihiana sana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika upande wa kuungwa mkono sana na wananchi.
Mzungumzaji wa mwisho kati ya wawakilishi wa vijana wa nchi mbalimbali wanaoshiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Vijana na Mwamko wa Kiislamu mjini Tehran alikuwa Fatima Mughnia, binti wa Imad Mughnia aliyekuwa kamanda wa ngazi za juu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Fatima amesisitiza kuwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini ulikuwa mwanzo na chachu ya mwamko wa Kiislamu na mapinduzi yanayoshuhudiwa sasa katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.
Baada ya hotuba za wawakilishi hao wa vijana wa nchi mbalimbali Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amehutubia hadhara hiyo akiwataja vijana wa nchi za Kiislamu kuwa ni wabeba bishara kubwa ya mustakbali mwema wa umma wa Kiislamu. Ameongeza kuwa mwamko wa vijana katika ulimwengu wa Kiislamu umezidisha matumaini ya mwamko wa mataifa yote ya Waislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema historia ya mwanadamu iko katika kipindi cha mabadiliko makubwa ya kihistoria na kuongeza kuwa mwanadamu wa sasa amevuka aidiolojia za kimaada za kimaxi, demokrasia ya kiliberali, nationalism na usekulari na sasa ameingia katika kipindi kipya ambacho alama yake kubwa zaidi ni mataifa mbalimbali kuelekea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kutaka auni na msaada kutoka kwa nguvu yake isiyokuwa na kikomo na kutegemea wahyi na ufunuo.
Ayatullah Khamenei amezungumzia udhibiti wa kanali ya udikteta yenye utata, hatari, habithi, ya kishetani ya Wazayuni na madola ya kibeberu duniani na akasema kuwa mapambano ya mataifa ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika dhidi ya madikteta vibaraka ni sehemu ya mapambano ya mwanadamu dhidi ya udikteta wa kimataifa wa Wazayuni, na kwa kuvuka kipindi hiki cha kihistoria jamii ya mwanadamu itakuwa imeondoka katika udhibiti wa udikteta hatari, na mababadiliko hayo makubwa yatapelekea kupatikana uhuru wa mataifa mbalimbali na kutawala thamani za kiroho za dini ya Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa ahadi ya kweli ya Mola Karima.
Ameashiria pia baadhi ya watu wanaoona kuwa ni muhali kuishinda kanali hiyo ya udikteta wa kimataifa ya Wazayuni na akasema kuwa huko nyuma pia iwapo mtu angezungumzia ushindi wa vijana wenye imani wa Hizbullah dhidi ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel au madhila ya sasa ya taghuti wa Misri (Hosni Mubarak) na mageuzi ya kustaajabisha ya kaskazini mwa Afrika, watu wengi wasingemwamini; kama ambavyo baadhi ya watu hawaamini macho yao mbele ya mapambano, ushindi na maendeleo makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; hakika qudra na nguvu kubwa ya Mwenyezi Mungu imedhihiri katika ushindi na matukio hayo ya kustaajabisha.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mahudhurio na kusimama kidete kwa mataifa mbalimbali katika medani kunatayarisha uwanja mzuri wa kupatikana nusra ya Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa katika kivuli cha kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu, Wazayuni, shetani mkubwa Marekani na madola ya Magharibi hii leo yanajihisi kuwa dhaifu mbele ya mwamko wa Kiislamu, na hisia hiyo ya udhalili na kushindwa itaendelea siku baada ya siku.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa mabadiliko yaliyotokea katika nchi za Kiislamu ni mwanzo wa njia ya wokovu na ufanisi na kuongeza kuwa, jambo muhimu ni kutoutambua ushindi uliopatikana kuwa ndio mwisho wa njia, bali tunapaswa kudumisha mapambano dhidi ya madhalimu wa kimataifa na vibaraka wao kwa kudumisha jihadi, kutumia azma ya mataifa na kumtegemea Mwenyezi Mungu Muweza.
Ameashiria pia maendeleo makubwa ya kisayansi na kielimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyanja za nyuklia, bioteknolojia, tiba na nyanja nyinginezo na akasema, vijana wenye imani wa nchi hii wamepata maendeleo hayo makubwa yanayoweza kuwa somo kwa vijana wa mataifa mengine ya Kiislamu licha ya vizuizi vya maadui.
Amezungumzia pia njama zinazofanywa na madikteta wa kimataifa kwa ajili ya kueneza fikra mbili zisizokuwa sahihi katika mataifa ya Kiislamu na akasema: "Maadui wa umma wa Kiislamu wameyabakisha nyuma mataifa ya Waislamu kwa karibu karne mbili zilizopita kupitia njia ya kudunga fikra ya kujihisi kuwa duni na dhaifu katika mataifa ya Kiislamu na fikra kwamba madola makubwa duniani hayashindiki; hata hivyo umma wa Kiislamu umeamka na kuelewa kuwa fikra hizo mbili si sahihi na kwamba mataifa ya Waislamu yanaweza kuhuisha tena fahari na adhama ya ustaarabu wa Kiislamu."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema karne hii ni karne ya Uislamu na masuala ya kiroho na akaongeza kuwa Uislamu, kutumia mantiki, masuala ya kiroho na uadilifu kwa pamoja, huyapa mataifa mbalimbali hadiya na zawadi, na mafunzo ya Mwenyezi Mungu yanasisitiza juu ya Uislamu unaoambatana na mantiki, kutafakari na kutaamali, Uislamu wa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, Uislamu wa jihadi na Uislamu wa kuchapakazi.
Akizungumzia juhudi zinazofanywa na ubeberu kwa ajili ya kufidia hasara na kipigo ulichopata kutokana na harakati za mapambano ya mataifa katika nchi za Misri, Tunisia, Libya na nchi nyingine za Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema adui anapanga njama, hivyo mataifa ya Kiislamu hususan tabaka la vijana wa umma wa Kiislamu ambao ndio injini ya mwamko wa Kiislamu wanapaswa kuwa macho na tahadhari kikamilifu na kwa kutumia uzoefu wa watu wengine wasiruhusu kanali ya kimataifa ya udikteta kupora mapindizu yao na kupotosha njia za sasa na za mustakbali.
Amekumbusha tajiriba ya miaka 32 ya Jamhuri ya Kiislamu katika kupambana na njama za Marekani na maadui wengine wa Uislamu na akasema kuwa, mabeberu wamefanya kila wawezalo kwa ajili ya kuishinda Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini hadi sasa wamekuwa wakipata pigo kali kutoka kwa taifa la Iran na wataendelea kufeli na kushindwa.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa miongoni mwa mbinu chafu zinazotumiwa na maadui ni kuzusha hitilafu katika umma wa Kiislamu. Amesema kuwa harakati ya mwamko wa Kiislamu haiwahusu Shia na Suni bali wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu wamejitosa katika medani ya mapambano kwa umoja na mshikamano.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria masuala yanayoyakutanisha pamoja mataifa ya Waislamu na kusema kuwa mataifa ya Waislamu yanatofautiana katika baadhi ya mambo kwa kutokana na tofauti zao za kijiografia, kihistoria na kijamii na hakuna kigezo kimoja kwa ajili ya nchi zote za Kiislamu; hata hivyo jambo muhimu ni kuwa mataifa hayo yote yanapinga udhibiti wa kishetani wa Wazayuni na Wamarekani na hayawezi kustahamili suala la kuwepo donda la kansa la Israel.
Akitoa mfano, Ayatullah Khamenei ameashiria njama zinazofanywa na vyombo vya habari duniani kwa ajili ya kuwatenga wananchi wa Bahrain na akasema kuwa vyombo vya habari vya nchi za Magharibi au tegemezi kwa Magharibi vinatumia njama ya kuzusha hitilafu kwa shabaha ya kuidhihirisha kadhia ya Bahrain kuwa ni kadhia ya Shia na Suni ilhali hakuna tofauti yoyote kati ya harakati za mwamko wa Kiislamu katika nchi mbalimbali.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kumtegemea Allah, kulinda umoja na mshikamano ndio siri ya ushindi. Ameashiria amri ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake akimtaka asimame kidete na imara na akasema kuwa umma wa Kiislamu utadumisha njia yake chini ya kivuli cha amri hiyo ya Mwenyezi Mungu bila ya kusita wala kusimama.
Amesema mustakbali wa umma wa Kiislamu uko wazi, na huku ashiria uwezo na nguvu kazi ya kibinadamu, kimaada na isiyo ya kimaada ya ulimwengu wa Kiislamu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa mataifa ya Kiislamu yako chini ya mwavuli mmoja wa kulingania watu kuelekea kwa Mwenyezi Mungu licha ya tofauti zao na vijana wa umma wa Kiislamu watashuhudia kipindi cha izza, nguvu na utukufu wa umma wa Kiislamu kwa idhini yake Mwenyezi Mungu na kuhamisha fahari hiyo kubwa kwa vizazi vijavyo.
Mwanzoni mwa mkutano huo Katibu Mkuu wa Mkutano wa Kimataifa wa Vijana na Mwamko wa Kiislamu Dakta Ali Akbar Velayati amesema kuwa vijana 1200 wanamapinduzi kutoka nchi 73 duniani wanashiriki katika mkutano huo. Amesema kuwa kamati sita za kitaalamu za mkutano huo zinajadili na kuchunguza maudhui kama “misingi ya kinadharia na kifikra na sababu za mafanikio ya mwamko wa Kiislamu”, “utawala wa Uislamu, vigezo, mafanikio na vijana”, “ubeberu wa kimataifa, Marekani na Wazayuni katika kukabiliana na wimbi la mwamko wa Kiislamu”, “vijana, mapambano ya Palestina na mwamko wa Kiislamu”, “uchunguzi wa fursa na vitisho vinavyoukabili mwamko wa Kiislamu” na “mustakbali wa mwamko wa Kiislamu”.
Velayati amesema washiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Mwamko wa Kiislamu wamesisitiza juu ya udharura wa kukabiliana na njama za ubeberu wa kimataifa hususan propaganda chafu na urongo wa vyombo vya habari vya mabeberu kuhusu malengo ya harakati za Kiislamu na vilevile juhudi za kueneza demokrasia ya kidini na kupigania uadilifu na uhuru. 943679



captcha