IQNA

Ayatullah Khamenei:

Iran italisaidia taifa lolote litakalosimama kupambana na utawala ghasibu wa Israel

7:19 - February 04, 2012
Habari ID: 2267623
Sambamba na siku hizi za kuadhimisha mwaka wa 33 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khameni amehutubia Swala ya Ijumaa mjini Tehran akitoa uchambuzi kamili kuhusu matunda na mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuzungumzia masuala muhimu ya ndani, vitisho vya maadui na hali ya kieneo na kimataifa na vilevile uchaguzi ujao wa Bunge la 9 la Iran.
Mwanzoni mwa hotuba ya kwanza ya Swala ya Ijumaa, Ayatullah Ali Khamenei amewapongeza wananchi kwa maadhimisho ya Alfajiri Kumi (siku kumi za kuanzia siku aliyorejea nchini Imam Khomeini akitokea uhamishoni hadi kufikia ushindi Mapinduzi ya Kiislamu) na vilevile sherehe za ushindi wa mapinduzi hayo na akasema ni wajibu kwa wananchi wote kushukuru neema hiyo kubwa ya Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa katika siku hizi pia kuna udharura wa kulishukuru taifa la Iran ambalo katika kipindi chote cha miaka 33 iliyopita limeonyesha uaminifu, kujitolea, ushujaa, uungwana, maarifa na kuona mbali na kuhudhuria daima katika medani ya mapambano.
Ameashiria pia mazingira ya sasa ya maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu yanayotofautiana na yale ya miaka iliyopita kutokana na mapinduzi yaliyofanywa na wananchi katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika hususan huko Misri, Tunisia na Libya na akasema kuwa mabadiliko hayo ni hadia kubwa na tukio lenye baraka na la kufurahisha kwa taifa la Iran ambalo kwa ushindi wa mapinduzi hayo limeondoka kwa kiasi fulani katika hali ya upweke.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendeleza hotuba yake kwa kuashiria sera kuu za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kusema mapinduzi hayo yamen’goa madarakani utawala uliokuwa dhidi ya Uislamu na wa kidikteta na kuasisi utawala wa Kiislamu na kidemokrasia.
Ayatullah Khamenei ametaja suala la kuondolewa hali ya utegemezi kwa wageni na kuleta hali ya kujitegemea katika nyanja zote, kuondoa mbinyo na ukandamizaji na kuleta uhuru, kuondoka katika hali ya uduni na kudhalilishwa kihistoria na kupata izza na heshima ya kitaifa na kuondoa hali ya udhaifu wa nafsi na kujiona duni na kuimarisha moyo kujiamini kitaifa kuwa ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema kuwa moja ya mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kubadilika kwa taifa la Iran kutoka katika hali ya kutengwa na taifa lisilokuwa na nafasi yoyote katika masuala ya kisiasa na nchi na kuwa taifa pevu na lenye uchambuzi wa kisiasa na taathira katika masuala ya nchi. Amesisitiza kuwa nara na kaulimbiu za mapinduzi zinazotolewa hivi sasa ndizo zilezile zilizokuwepo mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na suala hili ni ishara ya usalama na kutoondoka katika njia sahihi mapinduzi hayo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa nara za mapinduzi ni mithili ya alama za ishara za kuelekea kwenye malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa nara na kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu hazijabadili na suala hili lina maana kwamba viongozi na wananchi wa Iran hawajaondoka katika njia iliyonyooka ya mapinduzi.
Baada ya kuzungumzia baadhi ya matunda muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Ayatullah Khamenei amezungumzia pia baadhi ya nukta hasi na chanya na akasema: “Sambamba na kuimarisha masuala chanya na mafanikio yetu, hatupaswi kuficha nukta na mambo hasi bali tunapaswa kuondoa mambo hayo hasi ili yasikite mizizi.”
Amesema kuwa kumekuwepo hali ya kupanda na kushuka katika harakati ya miaka 33 ya Mapinduzi ya Kiislamu lakini harakati hiyo kamwe haijasimama katika mchakato wake wa kuelekea kwenye malengo makuu na daima imekuwa ikisonga mbele.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kushinda changamoto mbalimbali ni moja kati ya matunda muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu madola makubwa duniani yamekuwa yakifanya jitihada za kusimamisha harakati ya taifa la Iran, kuyapigisha magoti Mapinduzi ya Kiislamu na kulifanya taifa la Iran lijutie maamuzi yake kwa kutumia vizuizi mbalimbali kama kuitwisha Iran vita vya miaka 8, kufanya operesheni za kigaidi hapa nchini, mashinikizo ya kisiasa na vikwazo vya aina mbalimbali, lakini licha ya changamoto hizo zote utawala wa Kiislamu hapa nchini umeendeleza njia yake kwa nguvu zaidi na kuvishinda vikwazo hivyo vyote. Ayatullah Khamenei amesema kupanuliwa huduma za daraja ya kwanza kwa wananchi kote nchini ni miongoni mwa mafanikio ya utawala wa Kiislamu. Ameashiria maendeleo ya kisayansi na kielimu yaliyopatikana hapa nchini baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusema maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia ni miongoni mwa mafanikio muhimu kwa sababu elimu hutayarisha uwanja mzuri wa kupata nguvu na uwezo na ni msingi wa maendeleo ya pande zote ya nchi.
Ameyataja maendeleo ya kisayansi ya miaka 33 hapa nchini kuwa ni ya kustaajabisha. Amesema kuwa maendeleo hayo ya kielimu yamepatikana katika nyanja mbalimbali japokuwa yamekuwa maarufu zaidi katika baadhi ya nyanja kama teknolojia ya nyuklia.
Akiashiria maendeleo ya kustaajabisha ya kisayansi katika nyanja za elimu ya masuala ya anga, tiba, radiopharmaceuticals, bioteknolojia, teknolojia ya nano, maendeleo ya seli shina na cloning, dawa zilizodhidi ya saratani, utengenezaji wa kumpyuta kabambe (supercomputer) na nishati za kisasa, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa vituo maarufu na vyenye hadhi kubwa zaidi vya sayansi duniani vimethibitisha maendeleo hayo ya Iran, na kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2011 ya moja ya vituo hivyo vya sayansi, ustawi wa kielimu wa Iran umekuwa kwa kasi zaidi kuliko nchi nyingine yoyote duniani.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa ni kwa msingi wa ripoti hiyo ndio maana Iran imeshika nafasi ya kwanza katika maendeleo ya kielimu kwenye eneo la Mashariki ya Kati na nafasi ya 17 duniani.
Amesema kwa mujibu wa ramani ya maendeleo na ustawi hapa nchini, Iran inapaswa kushika nafasi ya kwanza katika masuala ya kielimu Mashariki ya Kati katika mwaka 1404 (miaka 14 ijayo), lakini imeshika nafasi hiyo mapema hata kabla ya wakati uliokadiriwa katika ramani ya maendeleo ya taifa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa maendeleo ya taifa katika ujenzi wa miundombinu ya masuala ya kiufundi na uhandisi wa sekta ya viwanda, barabara na usafirishaji na mawasiliano na viwanda ni miongoni mwa mafanikio ya utawala wa Kiislamu hapa nchini. Ameongeza kuwa inasikitisha kuwa licha ya maendeleo hayo makubwa lakini hadi sasa hakujatolewa ripoti nzuri na za wazi kwa wananchi kuhusu maendeleo hayo.
Ayatullah Khamenei ameitaja kazi ya kuhamisha thamani za Mapinduzi ya Kiislamu na kuzikabidhi kwa kizazi cha pili na cha tatu cha mapinduzi kuwa ni miongoni mwa hatua chanya za utawala wa Kiislamu hapa nchini. Amesema kielelezo cha wazi cha suala hilo ni wasomi kama Shahidi Mustafa Ahmadi Roshan na Rezai Nejad na kuongeza kuwa, licha ya kwamba wasomi hao vijana hawakudiriki kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini wala vita vya kulazimishwa, lakini walifanikiwa kupata daraja za juu za kielimu kwa kuelewa vyema wajibu wao wa kimapinduzi na Kiislamu na walidumisha njia yao licha ya vitisho walivyokabiliana navyo.
Amesisitiza kuwa kuwa Shahidi Ahmadi Roshani na Rezai Nejad ni kizazi cha tatu cha Mapinduzi ya Kiislamu na kusema harakati kubwa ya vijana baada ya kuuawa shahidi Ahmadi Roshani ya kutangaza kwamba wako tayari kudumisha njia ya kielimu na shahidi huyo ilikuwa harakati yenye umuhimu mkubwa na mfano mwingine wa kuhamisha thamani za Mapinduzi ya Kiislamu kwa kizazi cha tatu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa sambamba na maendeleo hayo, kumekuwepo baadhi ya watu walioondoka katika mkondo wa Mapinduzi ya Kiislamu lakini mafanikio yamekuwa makubwa zaidi ya nakisi na kasoro kama hizo.
Miongoni mwa mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu yaliyotajwa na Kiongozi wa Mapinduzi ni ustawi mkubwa wa taifa la Iran na uwezo wake wa kuwa na taathira katika masuala ya Mashariki ya Kati na hata duniani, muundo imara wa nchi na utawala wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na uadui wa aina mbalimbali na ustawi wa pande zote wa vyuo vikuu na vyuo vya kidini. Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yote ya kielimu, kijamii na kiufundi yamepatikana katika kipindi cha vikwazo vya pande zote vya maadui dhidi ya Iran, suala ambalo lina umuhimu mkubwa na linazidisha matumaini.
Ameendeza hotuba yake kwa kuashiria baadhi ya nukta hasi na za udhaifu na kusema, moja na mambo hayo ni kuelekea baadhi ya viongozi upande wa masuala ya kidunia, umaada, kujilimbikizia mali, na ubwanyeye, suala ambalo limekuwa na taathira mbaya na kuenea pia kati ya wananchi na jamii.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kusikitishwa na moyo wa israfu katika jamii na amesisitiza kuwa kuna ulazima wa kufanyika juhudi za kupunguza tabia ya israfu na tamaa za dunia na hatimaye kuondoa dosari hiyo katika jamii.
Ayatullah Khamenei amekutaja kutokuwepo maendeleo yanayotarajiwa katika masuala ya kimaadili, kiroho na katika kutakasa nafsi sambamba na maendeleo yaliyopatikana katika nyanja za sayansi na elimu na kutofikiwa uadilifu wa kijamii unaokusudiwa na dini ya Kiislamu kuwa ni miongoni mwa dosari zilizopo na akusema kuwa, kuna udharura wa kufanyika jitihada za hima kubwa kwa jili ya kuondoa nakisi hizo.
Amekumbusha wajibu wa viongozi na wananchi kwa ajili ya kudumisha harakati ya kufikia malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na thamani zake na akasema kuwa moja ya wajibu muhimu ni kuwajibika hususan miongoni mwa viongozi.
Amewataka viongozi wanaohudumia wananchi ndani ya Serikali, Bunge na Vyombo vya Sheria kutotupiana lawama, kwani wajibu wa kila chombo kuanzia Kiongozi Mkuu hadi nguvu kuu tatu za dola umeainishwa katika katiba na kila chombo kinapaswa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa kisheria.
Amesema hata kama kutakuwepo tatizo linalohusiana na Kiongozi Mkuu basi anapaswa kulikubali kwa moyo mkunjufu na kufanya jitihada za kuondoa tatizo na nakisi hiyo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewatahadharisha viongozi wasighafilike na masuala, thamani na malengo makuu kwa sababu ya kujishughulisha na mambo yasiyokuwa ya msingi na akawata walinde umoja na mshikamano. Amesema viongozi wa nguvu tatu kuu za dola na viongozi wa taasisi nyinginezo wanalazimika kulinda umoja na mshikamano wao hata kama watahitilafiana katika mitamo; wanapaswa na kushirikiana na kuwa pamoja katika malengo ya utawala wa Kiislamu.
Amesema kuwa umoja na mshikamano kati ya viongozi wa nchi, kati ya wananchi wenyewe na kati ya wananchi na viongozi ndio tiba mujarabu ya matatizo mengi ya nchi.
Katika sehemu nyingine ya hotuba zake za Swala ya Ijumaa Ayatullah Khamenei amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itasimama na kuunga mkono taifa au kundi lolote litakalosima kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel. 946334






captcha