IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Jamhuri ya Kiislamu daima itakuwa pamoja na mapambano ya wananchi wa Palestina

16:59 - February 12, 2012
Habari ID: 2272880
Waziri Mkuu halali wa Palestina Ismail Hania asubuhi ya leo amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei.
Katika mazungumzo hayo Ayatullah Khamenei amesema kuwa suala la mataifa mbalimbali hususan Waislamu kusaidia mapambano ya Kiislamu ya Palestina ni miongoni mwa mambo ya kistratijia ya makundi ya mapambano. Amesisitiza kuwa ushindi uliopatikana katika miaka ya hivi karibuni huko Palestina na hata sehemu ya sababu za mwamko wa sasa wa Kiislamu katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ni matokeo ya kusimama imara wananchi na makundi ya mapambano ya Palestina, na hapana shaka kwamba ushindi wa siku za usoni na kutimia kwa ahadi za Mwenyezi Mungu pia kutategemea mapambano na kusimama imara huko.
Ameashiria mapambano ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza na ushindi wao dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vya siku 22 na kusema, hapana shaka kwamba mrundikano wa hisia za mataifa mbalimbali ya eneo la Mashariki ya Kati katika kadhia ya Ghaza pia umekuwa na taathira katika mlipuko wa ghafla wa volcano ya mwamko wa Kiislamu katika eneo hili.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa harakati yoyote inayodhoofisha mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Palestina inatia dosari mustakbali. Amesisitiza juu ya kuwa macho mbele ya ushawishi na kupenya watu wanaolegeza kamba na wanaotaka suluhu na Wazayuni ndani ya harakati za mapambano, kwa sababu maradhi hudhihiri mwilini taratibu.
Ayatullah Khamenei amemwambia Ismail Hania kwamba: "Hatuna shaka yoyote kuhusu misimamo yako imara na ya ndugu zetu wanamapambano, na watu hawatarajii lolote kutoka kwenu ghari ya kusimama kidete."
Ameashiria pia hatima iliyomkuta Yasir Arafat ambaye baada ya kupendwa na watu kwa miaka mingi kutokana na kusimama kwake imara alikuja kutupiliwa mbali na kuchukiwa na mataifa ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika baada ya kutoka katika njia ya mapambano. Ameongeza kwamba mapambano na kusimama kidete huvutia nyoyo za wananchi na ni hazina kubwa ambayo inapaswa kulindwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitambua kadhia ya Palestina kuwa ni kadhia ya Kiislamu na maudhui inayoihusu. Amesema kuwa Iran imesimama imara na ina misimamo ya kweli katika kadhia ya Palestina na daima itakuwa pamoja na wananchi wa Palestina na makundi ya mapambano.
Kwa upande wake Waziri Mkuu halali wa serikali ya Palestina Ismail Hania ameelezea kufurahishwa kwake na kukutana na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na akatoa mkono wa pongezi kutokana na maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Hania amesema maadhimisho ya mwaka huu ya Mapinduzi ya Kiislamu yamefanyika wakati dunia na eneo hili vinashuhudia matukio na mabadiliko makubwa hususan mwamko wa Kiislamu.
Ameishukuru serikali na taifa la Iran kutokana na misaada yake kwa kadhia ya Palestina na akasema kuwa: "Jana wakati nilipokuwa katika helikopta nilishuhudia kwa karibu mamilioni ya wananchi katika sherehe za tarehe 11 Februari za Mapinduzi ya Kiislamu mjini Tehran na sisi tunalitambua taifa la Iran kuwa ni hazina ya kistratijia kwa ajili ya maudhui ya Palestina."
Bwana Ismail Hania amesisitiza pia juu ya stratijia tatu za serikali ya kisheria ya Palestina na kusema kukombolewa ardhi zote za Palestina, sisitizo juu ya mapambano na kutokubali mazungumzo ya suluhu na utawala ghasibu wa Israel na sisitizo kwamba kadhia ya Palestina ni suala la Kiislamu ni stratijia tatu kuu za makundi ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina.
Waziri Mkuu halali wa serikali ya Palestina amesisitiza juu ya udharura wa kuwa na imani na ahadi za Mwenyezi Mungu, ushindi wa taifa la Palestina na kuangamizwa utawala wa Kizayuni na amemhutubu Kiongozi Muadhamu kwa kusema: "Kama ulivyosema siku chache zilizopita, tumo katika kipindi cha (vita vya) Badr na Khaibar na wala hatuko katika kipindi cha kuzingirwa Waislamu katika pango la Shiibi Abi Twalib." 951902


captcha