Matini Kamili ya Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Munasaba wa Mwaka Mpya wa 1391 Hijria Shamsia (20 Machi 2012) ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Ewe Mgeuzaji wa nyoyo na basari! Ewe Mpangiliaji wa Usiku na Mchana!
Ewe Mbadilishaji wa mwaka na hali! Badilisha hali zetu kuwa bora ya hali.
Ewe Mola wangu, jaalia kwa ajili ya Hujja Wako mwana wa Hassan (Imam Mahdi AS) rehema Zako ziwe juu yake na wazazi wake katika saa hii na katika kila saa; uwe Walii kwake, Mtunzaji wake, Kiongozi wake, uwe Mwenye kumnusuru, Mwenye kumuongoza njia na Uwe jicho lake hadi utakapomfikisha kwenye ardhi Yako akiwa mtiifu na umneemeshe humo kwa muda mrefu.
Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba umpe katika nafsi yake mambo yanayotuliza jicho na kufurahisha nafsi, na kizazi chake, na wafuasi wake, na watu anaowaongoza, na watu wake maalumu, na watu wake wote kiujumla na adui yake na binaadamu wote.
Ninatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuwadia sikukuu ya Nairuzi na kwa kuanza mwaka mpya. Mkono wangu wa baraka uwaendee wananchi wenzangu wote azizi nchini, na Wairani wote walioko katika kila kona ya dunia na kwa mataifa yote yanayoadhimisha sikukuu ya Nairuzi. Mkono wangu wa baraka hasa hasa nautuma kwa familia azizi za mashahidi, majeruhi wa vita, aila zao, watu wote wanaojitolea katika njia ya haki, na watu wote wanaofanya kazi kwa bidii na idili kubwa katika nyuga tofauti. Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa matumaini makubwa, aijaalie (siku ya leo) kuwa siku njema kwa taifa la Iran, alipe taifa hili furaha, nishati na nyoyo kunjufu katika mwaka huu mpya na azifelishe njama na malengo yote ya maadui wa taifa hili Inshaallah.
Mwaka uliopita (wa Hijria Shamsia) - mwaka 1390 - ulikuwa ni mmoja ya miaka iliyojaa matukio mengi ya kila namna duniani, katika eneo hili na pia humu nchini. Kwa kweli unapoyaangalia matuko hayo utaona kijumla kwamba yamekuwa ni kwa faida ya taifa la Iran na yamelisaidia taifa hili kufikia malengo yake. Wale watu ambao wana fikra mbaya kuhusiana na taifa la Iran, kuhusiana na Iran na kuhusiana na kila kitu cha Iran na ambao hawalitakii kheri taifa hili, huko katika nchi za Magharibi hivi sasa kuna matatizo chungu nzima. Katika eneo hili pia, yale mataifa ambayo siku zote Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikiyaunga mkono, yameweze kufikia kwenye malengo yao makubwa, yamefanikiwa kuwang'oa madarakani madikteta, yamepitisha sheria mpya zenye misingi ya Kiislamu katika nchi zao, na kumzingira adui nambari moja wa umma wa Kiislamu na taifa la Iran - yaani utawala wa Kizayuni wa Israel. Humu nchini pia mwaka 1390 (Hijria Shamsia) ulikuwa mwaka wa kudhihiri nguvu za taifa la Iran kwa maana halisi ya neno. Katika upande wa kisiasa pia wananchi wa Iran mwaka huo walijitokeza kwa wingi mno katika matukio tofauti iwe ni katika maandamano ya Bahamn 22, (Februari 11, 2012) au uchaguzi wa Bunge wa Esfand 12 (Machi 2, 2012); walijitokeza kwa wingi mno kwenye matukio hayo kwa namna ambayo wliweza kuonesha kwa njia bora kabisa nguvu za taifa la Iran kitu ambacho ni mara chache kimewahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya eneo hili.
Licha ya kuweko uadui mkubwa kiasi chote hiki, propaganda mbaya kiasi chote hiki, mashambulizi yote haya ya kiadui ya watu wasiolitakia kheri taifa hili, lakini taifa la Iran katika miaka yote hii limeweza kujitokeza kwa wingi mno na kuthibitisha uwepo wake katika nyuga tofauti tena kwa hamasa kubwa na pia kuonesha jinsi lilivyo imara katika nyanja mbali mbali za kielimu na kijamii na kisiasa na kiuchumi. Alhamadulillah mwaka huo licha ya kuweko tabu na mashaka mengi, lakini ulikuwa ni mwaka wenye matunda mengi mazuri. Kama ambavyo pia imewahi kusemwa huko nyuma, hali na mazingira yaliyokuwepo yalikuwa ni hali na mazingira ya Badr na Khaybar yaani mazingira ya kukubali mashaka na matatizo na kuyashinda.
Kama ilivyotangazwa mwanzoni mwa mwaka uliopita, yaani mwaka 1390 kwamba huo ulikuwa ni mwaka wa Jihadi ya Kiuchumi. Ijapokuwa weledi na watambuzi wa mambo walikuwa wanajua kuwa jina hilo, msimamo na kaulimbiu hiyo ilikuwa ni jambo la lazima kwa ajili ya mwaka 1390 (Hijria Shamsia) lakini baadaye jambo hilo lilithibitishwa pia kupitia njama za maadui katika mwaka huo. Maadui zetu tangu awali kabisa ya mwaka huo walianza kutekeleza uadui wao dhidi ya taifa la Iran katika upande wa kiuchumi, lakini taifa la Iran, viongozi nchini, matabaka mbali mbali ya wananchi, vyombo mbalimbali nchini wote walikuwa makini na wameweza kwa werevu wa hali ya juu kukabiliana vizuri na vikwazo hivyo vya maadui na kwa kiasi kikubwa kuzishinda athari za vikwazo hivyo na kuivunja nguvu silaha hiyo ya adui. Mwaka 1390 (Hijria Shamsia) ulikuwa mwaka wa kazi kubwa za kielimu nami Inshaallah katika hotuba yangu (ya leo ya mwaka mpya) nitazungumzia na kulifafanulia taifa azizi la Iran baadhi ya maendeleo ya kielimu na kiuchumi na jitihada mbali mbali zinazoendelea kufanyika. Mwaka 90 ulikuwa ni mwaka wa changamoto, ulikuwa ni mwaka wa nishati na jitihada kubwa, ulikuwa ni mwaka ambao kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu taifa la Iran limeweza ndani yake kushinda changamoto zilizokuwepo.
Hivi sasa tumo katika mwaka mwingine na tunataraji kuwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, kwa mara nyingine tena taifa la Iran litaendelea na jitihada, idili na juhudi zake kwa umakini wa hali ya juu na katika mwaka huu pia litaweza kupata maendeleo makubwa. Kwa ninavyoona mimi, na baada ya kuletewa ripoti na kushauriana na watu weledi na watambuzi wa mambo ni kwamba changamoto kubwa ambayo tunayo mwaka huu - yaani katika mwaka huu ulioanza leo na ulioanza sasa hivi - ni changamoto ya kiuchumi. Jihadi ya kiuchumi si kitu ambacho kinaweza kumalizika. Kufanya jihadi ya kiuchumi na kushiriki kijihadi katika nyuga za kiuchumi, ni jambo la dharura kwa taifa la Iran.
Mimi mwaka huu napenda kuyagawanya mafungu mbali mbali masuala yanayohusiana na jihadi ya kiuchumi. Moja ya sehemu muhimu ya masuala ya kiuchumi inahusiana na suala la uzalishaji wa ndani. Kama kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na kwa njia na azma isiyotetereka ya taifa na kwa juhudi za viongozi nchini - kama kwa kuzingatia yote hayo - tutaliimarisha zaidi na kwenda nalo vizuri suala la uzalishaji wa ndani kwa sura na namna ambayo linastahiki kuwa, basi bila ya shaka yoyote tutaweza kuzishinda kwa kiasi kikubwa sana njama za maadui dhidi yetu. Hivyo sehemu muhimu katika jihadi ya kiuchumi ni suala la uzalishaji wa ndani ya taifa letu. Kama taifa la Iran - kwa hima yake, kwa nia yake, kwa utambuzi wake, kwa weledi wake, kwa ushirikiano na msaada wa viongozi nchini, kwa mipangilio mizuri na sahihi - litaweza kutatua tatizo la uzalishaji wa bidhaa za ndani, na kama litapiga hatua kubwa zaidi katika medani hiyo, basi bila ya shaka yoyote tutaweza kuzishinda kikamilifu changamoto zote tunazosababishiwa na adui. Hivyo suala la uzalishaji wa ndani, ni suala muhimu sana.
Kama tutaweza kuimarisha na kustawisha uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi, basi tutaweza kutatua tatizo la mfumuko wa bei, tutaweza kutatua suala la ukosefu wa kazi na tutaweza kuuimarisha uchumi wetu wa ndani kwa maana halisi ya neno. Ni wakati huo na ni baada ya kuona hali hiyo ndipo adui atakata tamaa na kuvunjika moyo kikamilifu. Na wakati adui atakapovunjika moyo basi njama za adui, hila za adui, kedi za adui nazo zitakoma.
Hivyo ninatoa mwito kwa viongozi wote nchini, kwa wahusika wote katika medani ya kiuchumi na wananchi wetu wote azizi kuufanya mwaka huu kuwa mwaka wa kustawisha bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi yetu. Hivyo, kaulimbiu ya mwaka huu itakuwa ni "Uzalishaji wa Taifa, Kuunga Mkono Kazi na Rasilimali za Iran." Sisi tunapaswa kuhakikisha kuwa tunaunga mkono kazi na mfanya kazi wa Kiirani, tuunge mkono rasilimali ya Muirani pamoja na mwenye rasilimali na jambo hilo litawezekana tu kwa kutia nguvu uzalishaji wa taifa. Jukumu la serikali katika jambo hilo ni kuunga mkono uzalishaji wa ndani, viwanda na kilimo. Jukumu la watu wenye rasilimali na wafanyakazi ni kulitia nguvu gurudumu la uzalishaji na kuwa makini katika kazi zao za uzalishaji. Jukumu la wananchi - ambapo kwa mtazamo wangu mimi ni muhimu zaidi kuliko jambo lolote - ni kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani. Sisi tunapaswa tujizoeshe na tuufanye huu kuwa ndio utamaduni wetu, tulifanye jambo hili kuwa ni jukumu na wajibu wetu kwamba kila tunapoona bidhaa (kutoka nje) lakini ikawa mfano wa bidhaa hiyo ipo na inazalishwa humu nchini, basi tutumie ile inayozalishwa humu nchini na tulipe uzito wa hali ya juu suala la kuacha kutumia bidhaa za nje; tena katika nyuga zote, katika upande wa matumizi yetu ya kila siku na katika pande kubwa zaidi na muhimu zaidi. Tunataraji kwamba, kama tutakuwa na tabia hiyo, na kama tutakuwa na fikra na msimamo huo, basi taifa la Iran katika mwaka 1390 (Hijria Shamsia) pia litaweza kuzishinda njama za maadui na kuzifelisha pia hila na kedi za watu wasiolitakia kheri taifa hili katika upande wa kiuchumi.
Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu alijaalie taifa la Iran lifanikiwe katika suala hili na katika masuala yote mengine. Aifanye roho ya Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) ifurahi na iwe radhi nasi. Ninamuomba Mwenyezi Mungu azifufue roho njema za mashahidi wetu azizi pamoja na mawalii Wake.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
974390