IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jamhuri ya Kiislamu inalinda haki za taifa la Iran mithili ya simba

20:47 - March 22, 2012
Habari ID: 2294072
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumanne jioni amehutubia mjumuiko mkubwa wa wafanya ziara na majirani wa Haram ya Imam Musa Ridha AS mjini Mash-had katika siku ya kwanza ya msimu wa machipuo iliyokwenda sambamba na kuanza mwaka mpya wa wa Kiirani wa 1391 Hijria Shamsia na kusema Jamhuri ya Kiislamu inalinda haki za taifa la Iran mithili ya simba.
Kwa mujibu wa tovuti ya Kiongozi Muadhamu, katika hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kubainisha mafanikio mbali mbali liliyopata taifa la Iran katika mwaka uliopita wa 1390 Hijria Shamsia katika kukabiiliana na majigambo ya kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiusalama ya maadui wa taifa la Iran, amesisitiza kuwa, hatua ya taifa la Iran ya kulinda vilivyo na kwa ghera kubwa utajiri wake wa mafuta ndilo jambo lililopelekea kuongezeka uadui wa mabeberu wa dunia dhidi ya Mfumo wa Kiislamu nchini Iran. Amesema Jamhuri ya Kiislamu inalinda haki za taifa la Iran mithili ya simba.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza hotuba yake mbele ya mkusanyiko huo mkubwa wa wafanya ziara na majirani wa Haram ya Imam Musa Ridha AS mjini Mash-had kwa kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa Wairani wote kwa mnasaba wa kuwadia sikukuu ya Nairuzi.
Vile vile amechora na kutoa taswira ya kina kuhusiana na nukta za udhaifu na nukta madhubuti katika kazi za taifa la Iran pamoja na mipango na njama za watu wanaolitakia mabaya taifa hili katika mwaka uliopita wa 1390 Hijria Shamsia ili kwa njia hiyo iweze kuoneka kwa uwazi kabisa nafasi ya Wairani na maadui wao katika mapambano hayo ya kiistratijia.
Amesema, lengo kuu la mabeberu la kujizatiti kijeshi katika eneo hilo na majigambo na makelele yao ya kipropaganda, kisiasa, kiuchumi pamoja na vitisho vya kijeshi na kiusalama vya Marekani na mabeberu wengine dhidi ya Iran kuwa ni kutaka kuwatia woga wananchi wa Iran, kuwakatisha tamaa na kuwakwamisha katika juhudi zao na kuongeza kuwa, katika mwaka 1390 Hijria Shamsia, mabeberu walitumia nguvu zao zote kujaribu kulithibitishia taifa hili shujaa, lililo hai na lililojaa nishati kwamba Wairani hawawezi kufanya chochote, lakini wananchi wa Iran kwa kutegemea mafundisho waliyopata kutoka kwa Imam mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) mara kwa mara wamekuwa wakiwaelewesha kivitendo walimwengu wote pamoja na mabeberu wote ambao uadui wao dhidi ya taifa la Iran umewafanya kuwa vipofu, kwamba Wairani wanaweza kufanya lolote wanaloamua.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia ukweli kuwa nukta nzuri na madhubuti katika matendo na kazi za taifa la Iran ni mengi mno ikilinganishwa na udhaifu wake na kwamba ushirikiano unaostahiki kupongezwa uliooneshwa na wananchi wa Iran kwa viongozi wao umepelekea kupatikana matunda mazuri ya kiuchumi katika mwaka uliopita wa 1390 Hijria Shamsia ambapo zoezi la kutoa ruzuku kwa malengo maalumu ni miongoni mwa mafanikio makubwa zaidi yaliyopatikana katika uwanja huo.
Vile vile ametoa ushahidi kupitia mtazamo wa pamoja wa wataalamu wote wa kiuchumi kuhusiana na udharura wa kutekelezwa mpango wa kutoa ruzuku kwa malengo maalumu akisisitiza kwamba, mwaka 1390 Hijria Shamsia, Serikali na Bunge licha ya kuweko mazingira magumu na tata sana yaliyosababishwa na vikwazo vya mabeberu dhidi ya taifa hili, lakini ziliweza kutekeleza awamu muhimu na ya kuzingatiwa ya kazi hiyo kwa uungaji mkono na ushirikiano mzuri wa wananchi ingawa tab'an bado kazi haijaisha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kugawanywa kiuadilifu ruzuku na kuboreshwa hali ya maisha ya watu wa matabaka dhaifu kwamba ni miongoni mwa matunda mazuri ya zoezi hilo na kuongeza kuwa, marekebisho ya kiasi fulani katika gurudumu la uzalishaji na kupiga hatua kuelekea kwenye kuweka mlingano mzuri katika matumizi na ubora wa bidhaa za ndani ni miongoni mwa malengo mengine ambayo mwaka jana yalifanikishwa nchini Iran kwa hima ya wananchi na viongozi wao katika upande wa kazi za uzalishaji wa taifa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia usimamiaji wa ubebaji na usafirishaji wnishati, matumizi mazuri na kupunguza matumizi ya mafuta katika kiwango kinachokaribiana na uzalishaji wa ndani kuwa ni miongoni mwa matunda mazuri yaliyopatikana nchini Iran mwaka jana na kuongeza kuwa, kazi hiyo imefanyika humu nchini katika mazingira ambayo Iran iko chini ya vikwazo na kazi hiyo kwa hakika imefanikiwa kufelisha na kuvunja njama za maadui dhidi ya taifa hili.
Maendeleo ya taifa la Iran katika upande wa sayansi na teknolojia na athari nzuri za mafanikio hayo katika masuala ya kiuchumi nchini ni nukta nyingine muhimu ambayo imebainishwa na Kiongozi Muadhamu wakati alipokuwa akizungumzia mafanikio liliyopata taifa la Iran katika mwaka uliopita wa 1390 Hijria Shamsia mbele ya wafanya ziara na majirani wa Haram ya Imam Ridha AS mjini Mash-had.
Aidha ameashiria hisia maalumu na za siku zote zilizopo nchini Iran kwa ajili ya kupigania maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia na kusisitiza kuwa, kufanikishwa lengo hilo kuna maana ya kuimarishwa misingi ya uwezo na nguvu za kiuchumi na utajiri wa kisiasa nchini. Vile vile ametoa ushahidi kutoka katika nyaraka na ripoti za vituo vyenye itibari ya kielimu duniani na kusisitiza kuwa, wastani wa maendeleo ya kielimu nchini Iran ni mkubwa sana ikilinganishwa na kile ambacho hadi hivi sasa wananchi wameelezwa na ambacho wanakijua na kukitambua.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa, ripoti zenye itibari za taasisi muhimu za kimataifa zinaonesha kuwa, kutokana na kukuwa kwake kielimu kwa asilimia 20, Iran ni nchi yenye kasi kubwa zaidi ya kukua kielimu duniani na kwamba mwaka 1390 Hijria Shamsia, Iran ilipanda na kuwa ya kwanza kwa maendeleo ya kielimu katika nchi za Mashariki ya Kati na ilikuwa katika daraja la 17 kwa maendeleo ya kielimu kati ya nchi zote za duniani. Amesema, maendeleo hayo makubwa sana ya kielimu yamepatikana katika hali ambayo maadui wanafanya kila njia kuizuia Iran isipate maendeleo ya kielimu ikiwa ni pamoja na kutumia vikwazo ambavyo kwa madai yao wanadai kuwa ni vikwazo vilivyolenga kuilemaza kikamilifu Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia maendeleo ya wasomi vijana wa Kiirani katika teknolojia ya biolojia, teknolojia ya Nano na teknolojia ya anga za mbali na kuongeza kuwa, vijana walioliletea fakhari kubwa taifa la Iran, mwaka 1390 Hijria Shamsia walifanikiwa kurutubisha urani kwa asilimia 20 na kwa hatua yao hiyo wakamuweka kinywa wazi adui.
Ameongeza kuwa, katika mwaka 1388 Hijria Shamsia Wamarekani pamoja na kwamba walikuwa wanajua ni kiasi kikubwa kiasi gani Iran inahitajia dawa lakini pamoja na hayo walitaka Iran iwape rushwa na kwa kutumia mabavu Wamarekani walitaka kuipokonya Iran urani iliyokuwa tayari imejirutubishia kwa asilimia ndogo kwa madai ya kuipatia Iran urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20 tena kupitia nchi nyingine. Lakini vijana wa Kiirani walitegemea uwezo na akili yao ya kupigiwa mfano na wakafanikiwa kurutubisha urani kwa asilimia 20 humu humu nchini na hivi sasa Iran inao uwezo wa kutengeneza anuwai kwa anuwai ya dawa zinazotumia mionzi zinazohitajiwa na maelfu ya wagonjwa kwa kutumia fueli nyuklia iliyozalishwa humu humu nchini.
Kuzalishwa sahani za fueli nyuklia ndani ya Iran ni uhakika mwingine ambao Ayatulla Udhma Khamenei ameuzungumzia na kuutolea ushahidi wa mafanikio ya kielimu waliyopata wananchi wa Iran katika mwaka uliopita wa 1390 Hijria Shamsia; maendeleo ya kupigiwa mfano ambayo yaliifanya Iran ing'are kielimu na kwa maadui mwaka huo ukawa wa kuzidi kuvunjika moyo na kukata tamaa.
Ameongeza kuwa, mabeberu walikuwa wanatwambia kwamba tuwape urani tuliyoirutubisha kwa asilimia ndogo ili na wao watupe urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20 katika nchi nyingine na halafu asilimia hiyo 20 ya urani iliyorutubishwa itengenezewe sahani za fueli nyuklia katika nchi nyingine (kama njia ya kuikwamisha Iran isiwe na teknolojia hiyo) lakini vijana wa Kiirani wameweza kufanya wenyewe kazi zote hizo bila ya kutegemea madola hayo ya kigeni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuongezeka kwa asilimia 6 uzalishaji wa dawa zenye michanganyo mipya ya kisasa na kuongezeka huduma za kielimu kuwa ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini Iran katika mwaka 1390 Hijria Shamsia.
Aidha ameashiria safari yake ya wiki iliyopita ya kukagua Kituo cha Utafiti wa Sekta ya Mafuta cha Iran na kuongeza kuwa, katika kutembelea kwake kituo hicho aliona kwa karibu maendeleo makubwa iliyopiga Iran kwenye sekta hiyo katika hali ambayo huko nyuma ilikuwa mtu hata hawezi kufikiria kuwa Iran ingeliweza kupiga hatua kama hizo za maendeleo. Amesema hali ni hiyo hiyo katika vituo vingine nchini na jambo hilo linaonesha kuwa, maendeleo kama haya ya kustaajabisha hayahusiani na sekta moja tu bali yamekuwa ni jambo la kawaida kwa Iran katika sekta zake zote.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia sifa nyingine maalumu kama vile moyo na fikra ya kijihadi na sifa ya kujiamini ya wasomi vijana wa Kiirani na kuongeza kuwa, wakati alipotembelea Kituo cha Utafiti cha Sekta ya Mafuta nchini kwa mara nyingine uhakika huu ulijitokeza kwamba vijana kwa wazee wenye vipaji mbali mbali nchini Iran wanaviona na kuvihesabu vikwazo vya maadui kuwa ni fursa ya maendeleo na kwamba fikra hii muhimu inayokwenda sambamba na kutegemea vipaji vya vijana na kuongeza wigo wa ushirikiano kati ya Vyuo Vikuu na sekta ya viwanda ni mambo ambayo yanasaidia sana katika kuchanua vipaji na vipawa vya wananchi wa Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei, ameashiria pia athari za moja kwa moja za maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia kwa uchumi wa taifa na kusisitiza kuwa, maendeleo ya namna ni uthibitisho usio na shaka hata kidogo wa kuweko jihadi ya kweli ya kiuchumi nchini Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, makelele ya maadui wasiolitakia mema taifa la Iran yaliyosikika katika kipindi kizima cha mwaka 1390 Hijria Shamsia hayakuwasaidia chochote maadui hao na kusisitiza kwamba, vibaraka wa serikali ya Marekani katika kila kona ya dunia waliingia kazini mwaka huo ili kwa tamaa na ndoto zao waweze kuvifanya vikwazo dhidi ya Iran vizae matunda kwa faida yao na watoe pigo kwa wananchi wa Iran na vile vile wazushe mfarakano kati ya wananchi na utawala wa Kiislamu nchini lakini njama zao zote zimeshindwa kufanikisha waliyoyataka.
Akibainisha mafanikio mengine liliyopata taifa la Iran katika mwaka 1390 Hijria Shamsia, Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia udiplomasia amilifu na makini wa Iran katika masuala ya eneo hili na kuongeza kuwa, mwaka uliopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iligeuka kuwa kituo kikuu kilichopewa umuhimu mkubwa na ulimwengu ulioamka wa Kiislamu.
Vile vile amesema kuhusiana na uwanja wa huduma za kiuchumi, kujenga makumi ya maelfu ya nyumba kwa ajili ya wananchi na kufanya juhudi bila ya kuchoka katika nyuga tofauti kama vile kujenga mabarabara na makazi ya watu vijijini kwamba ulikuwa ni mwanzo mzuri wa muongo wa maendeleo na uadilifu nchini Iran na kuongeza kuwa, matukio kama hayo yanazidi kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa maadui wenye chuki na inadi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja hatua ya wananchi wa Iran ya kujitokeza kwa wingi sana katika uchaguzi wa tarehe 12 mwezi Isfand 1390 Hijria Shamsia (Machi 2, 2012) kuwa ni hatua nyingine ya kupigiwa mfano ya taifa la Iran katika mwaka uliopita na kuongeza kuwa, ana matumaini kwamba wananchi watajitokeza kwa wingi na kwa njia bora pia katika duru ya pili ya uchaguzi huo.
Jambo jingine lililoashiriwa na Kiongozi Muadhamu katika hotuba yake hiyo muhimu ni jinsi duru za kisiasa na vyombo vya kigeni vilivyofanya njama kwa muda wa miezi sita kujaribu kuwavunja moyo wananchi wa Iran na hata kuwatisha wananchi hao kupitia kuwaua kigaidi wasomi wa nyuklia wa Iran ili wananchi wasishiriki kwenye uchaguzi wa Machi 2, 2012; lakini njama zote hizo zilishindwa, na wananchi wa Iran walijitokeza kwa wingi mno katika uchaguzi huo.
Amesema, kushiriki kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi wa bunge wa Machi 2, kumepindukia sana wastani wa kushiriki wananchi katika chaguzi za Bunge kwenye nchi nyingine duniani na huku akiashiria wastani wa kushiriki wananchi wa Marekani katika chaguzi za mabaraza ya Congress, baraza la taifa la baraza la Senate la nchi hiyo ambapo kwa kawaida huwa ni wastani wa asilimia 30 hadi 40 tu ya wapiga kura wanaoshiriki katika chaguzi hizo ameongeza kuwa, hatua ya wananchi wa Iran ya kujitokeza kwa wingi wa zaidi ya asilimia 64 katika uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (bunge la Iran) inazidi kutilia mkazo uhakika halisi wa mambo kati ya chaguzi za nchi hizi mbili, Iran na Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kushiriki kwa wingi wa kupigiwa mfano wananchi wa Iran katika uchaguzi huo kuwa kunatoa ujumbe wa wazi wa kuonesha uhakika wa mambo ulivyo nchini Iran.
Ameongeza kuwa, mabeberu walipiga makelele mengi na kufanya propaganda kubwa kwa miezi mingi ili kuufanya uchaguzi wa Bunge wa Machi 2, 2012 nchini Iran ususiwe na wananchi na hivyo kujaribu kuonesha kuwa kuna mfarakano kati ya wananchi na utawala wa Kiislamu nchini Iran lakini kwa mwamko na hamasa na wananchi, siku ya uchaguzi huo ilikuwa siku muhimu iliyoliletea heshima taifa la Iran na utawala wake wa Kiislamu na kuonesha kivitendo nguvu za taifa hili.
Baada ya kuchora picha ya nafasi ya taifa la Iran na ya adui katika mwaka uliopita wa 1390 Hijria Shamsia, Ayatullah Udhma Khamenei ameanza kuzungumzia swali la kimsingi la kwamba kwa nini kambi ya mabeberu inalifanyia uadui taifa la Iran na mfumo wake wa Kiislamu?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu swali hilo akikanusha visingizio na kulaumu ugeugeu wa mara kwa mara wa madola ya kigeni likiwemo suala la nyuklia na haki za binaadamu na kusisitiza kuwa, sababu kuu ya kushuhudiwa uadui na chuki za mabeberu dhidi ya Iran ni kwamba utawala wa Kiislamu nchini Iran umeweza kulinda kwa njia bora na nzuri kabisa utajiri mkubwa wa mafuta na gesi wa Wairani.
Aidha amezungumzia jinsi nchi za Magharibi zinavyotegemea kupindukia nishati ya mafuta na gesi na kuongeza kuwa, nchi hizo za Magharibi zinajua vyema kuwa akiba zao za mafuta haziwezi kudumu kwa zaidi ya miaka 10 mingine na kwamba baada ya hapo mshipa wao wa maisha utalazimika kutegemea kikamilifu akiba za mafuta za maeneo mengine duniani hasa Ghuba ya Uajemi hivyo kuzidhibiti nchi zenye utajiri mkubwa wa mafuta hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuna umuhimu wa kipekee, wa kiistratijia na wa kufa na kupona kwa madola hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia uhakika kwamba Iran kiujumla ni nchi yenye akiba kubwa zaidi ya mafuta na gesi duniani na kuongeza kwamba, madola ya kibeberu yanataka kudhamini vyanzo vya kiistratijia kwa njia yoyote ile na kufyonza utajiri wa nchi zenye akiba ya mafuta na kuzifanya ziyeyuke kama nta kwa maslahi wa madola hayo, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara mithili ya simba kukabiliana na malengo hayo haramu.
Ameongeza kuwa, wale watu wanaodhani kuwa kulegeza kamba katika suala la nyuklia kutamaliza uadui wa Marekani dhidi ya Iran watambue kuwa wako kwenye mghafala mkubwa kwani katika eneo hili ziko nchi mbali mbali zilizo na silaha za nyuklia lakini Marekani haioneshi hisia zozote kali kuhusiana na nchi hizo, hivyo sababu hasa ya uadui wa maadui wa taifa la Iran si suala la nyuklia wala haki za binaadamu bali ni kutokana na wananchi na utawala wa Kiislamu nchini Iran kusimama imara na kulinda vilivyo utajiri wake wa mafuta na gesi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja dhana waliyo nayo Wamarekani wanaofikiri kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoweka, au itadhoofika au italegeza kamba katika misimamo yake kupitia uadui, vitisho na vikwazo kuwa ni dhana potofu na ni kosa kubwa. Pia amewaonya Wamarekani kwamba yatawakumba madhara ya kosa lao hilo la kihistoria hivyo kabla mambo hayawaharibikia zaidi, waamiliane kwa heshima na taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, nyuma ya pazia la majigambo na makelele mengi yanayotolewa kila leo na Marekani, kumejificha udhaifu mkubwa wa nchi hiyo na huo ni uhakika usiopingika.
Ameongeza kuwa, Rais wa hivi sasa wa Marekani aliingia madarakani kwa kaulimbiu ya mageuzi, na wananchi wa Marekani nao walimpigia kura kwa matumaini kwamba ataweza kuboresha hali yao mbaya ya maisha, lakini hivi sasa katika upande wa kiuchumi, Marekani ina madeni makubwa kupindukia na inakabiliwa pia matatizo mengine mengi, na katika upande wa kijamii pia hadi hivi sasa kunashuhudiwa maandamano ya wananchi chini ya mwavuli wa Harakati ya Kuteka Wall Street ya kupinga mfumo wa kibepari nchini humo na katika upande wa kisiasa aidha, Marekani inakabiliwa na hali mbaya mno huko Iraq, Afghanistan, Pakistan, Misri na katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, upo uwezekano wa Wamarekani kufanya wendawazimu na kujitia hatarini lakini sambamba na Iran kutangaza kwa kusisitiza kuwa haina silaha za atomiki na wala haina mpango kabisa wa kutengeneza silaha hizo za mauaji ya halaiki ya watu, inatangaza bayana kuwa itakabiliana na mashambulizi yoyote yale yanayoweza kufanywa na Marekani au utawala wa Kizayuni kwa kiwango kile kile ambacho Iran itashambuliwa.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amelitaja suala la kushindwa batili katika shambulizi la kambi ya haki kuwa ni sunna ya Mwenyezi Mungu iliyo muhali kubadilika na kusisitiza kuwa, taifa lililo tayari wakati wote, lililo imara na nia na azma ya kweli na lililo na nishati na hamasa ya hali ya juu la Iran, halina mawazo kabisa ya kuvamia na kushambulia nchi nyingine yoyote, lakini limeshikamana vilivyo na misimamo yake ya kulinda uwepo wake, utajiri, utambulisho, Uislamu na Jamhuri yake ya Kiislamu na kwa hakika litavilinda ipasavyo vitu hivyo kwa gharama yoyote ile.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amegusia kauli mbiu ya mwaka huu wa 1391 Hijria Shamsia ambayo ni "Uzalishaji wa Taifa, Kuunga Mkono Kazi na Rasilimali ya Iran" na kuongeza kwamba, watu wote nchini wana jukumu la kuhakikisha kauli mbiu hiyo inafanikiwa.
Aidha amesisitizia wajibu wa Mfuko wa Ustawi wa Taifa wa Iran kuunga mkono na kutia nguvu uzalishaji wa bidhaa za ndani akiitaja hiyo kuwa ni nukta muhimu sana ya kazi na majukumu ya Serikali katika kuifanya kaulimbiu hiyo ifanikiwe.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, Majlisi (Bunge) nayo inapaswa kushirikiana na Serikali katika kustawisha uzalishaji wa taifa na ilifanye jukumu hilo kuwa miongoni mwa ajenda zake kuu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuzalisha bidhaa za ndani zenye ubora wa hali ya juu, zinazopendeza na za kudumu sambamba na kufanya bei yake kuwa rahisi kadiri inavyowezekana kuwa ni katika majukumu ya wafanya kazi na watu wenye mitaji na rasilimali zao katika kazi hizo na kuongeza kuwa, katika upande huo pia, Serikali na Bunge nchini Iran zinapaswa kutoa msaada wao mkubwa ili kurahisisha ufanikishaji wa masuala hayo.
Aidha amekosoa ada ghalati ya kuona fakhari kutumia bidhaa za nje waliyo nayo baadhi ya watu nchini na kukumbusha kwamba, baadhi ya bidhaa za humu ndani zinauzwa kwa kutumia nembo za nje kutokana na kuwepo ada na tabia hiyo mbovu wakati jambo hilo ni kwa madhara ya Iran na linatoa pigo kwa maendeleo na mustakbali wa taifa hivyo amewataka wananchi watie hima ya kuachana na tabia hiyo ghalati na washiriki vilivyo katika jihadi ya kiuchumi nchini.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake aliyoitoa kwenye Haram ya Imam Ridha AS mjini Masha-had (kaskazini mashariki mwa Iran) katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 1391 Hijria Shamsia, Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, umoja na mshikamano ni kitu kinachohitajika sana nchini na huku akiwataka watu wote wawe na tabia za kuoneana huruma, kupendana na kushirikiana, amesema, kuweko mawazo na fikra tofauti nchini hakupaswi kupelekea kuzuka hitilafu na mifarakano.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametahadharisha kuwa mizozo katika masuala mbali mbali ya kisiasa na kiuchumi na dhidi ya shakhsia za watu hupelekea kuzuka uadui miongoni mwa watu na kuongeza kuwa, si sahihi kumchukulia mpinzani anayekubaliana na Jamhuri ya Kiislamu na anayetafuta haki lakini ikawa amekosea njia kuwa ni mfano na maadui wenye chuki na inadi na utawala wa Kiislamu nchini.
Aidha ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo visivyo vya hekima na vya kuchochea hitilafu vya baadhi ya duru za Intaneti na kuongeza kuwa, viongozi nchini wana wajibu wa kudhibiti mambo hayo kwa namna yoyote ile.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ametoa mwito kwa watu wote kushikamana na maadili ya Kiislamu na kuheshimu sheria na kuongeza kuwa, Mwenyezi Mungu apishie mbali kutokezea watu wakafikiri kupitia maneno yake hayo kuwa anawaponda na kuwalaumu vijana wanamapinduzi kwani yeye anawaona vijana wote waumini na wanamapinduzi kuwa ni sawa na wanawe wa kuwazaa na kwa hakika anawaunga mkono lakini wakati huo huo anapenda kutahadharisha na kusisitiza kuwa watu wote wanapaswa kuchunga maadili ya Kiislamu na kuheshimu sheria.
Vile vile amelitaka Bunge na Serikali kuchungiana mipaka yao na kwa mara nyingine tena ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuwadia mwaka mpya wa 1391 Hijria Shamsia na kumuomba Mwenyezi Mungu aujaalie mwaka huu kuwa mwaka uliojaa nishati, mafanikio na ustawi kwa taifa la Iran.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu mbele ya mjumuiko huo mkubwa wa wananchi, Ayatullah Vaez Tabasi, Mdhamini na Msimamizi wa Haram Tukufu ya Imam Ridha AS huko Mash-had ametoa hotuba fupi na sambamba na kuashiria mabadiliko makubwa yaliyotokea kwenye kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika eneo la Mashariki ya Kati, kaskazini mwa Afrika na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu, matukio ambayo yamepelekea kuundwa serikali mpya na kupinduliwa baadhi ya madikteta na vibaraka wa nchi za Magharibi, ameyataja matukio hayo makubwa kuwa ni katika matunda na athari za maneno na fikra za Imam Khomeini (quddisa sirruh) na siasa za Jamhuri ya Kiislamu zinazoongozwa kwa busara za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
Vile vile amesema, mustakbali wa Uislamu ni mzuri na ni wenye kutia matumaini. Ameongeza kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kushinda njama zote za maadui licha ya kuweko mashinikizo mengi na vitisho mbali mbali vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni dhidi yake.
974408
captcha