IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Waziri Mkuu wa Uturuki

12:15 - April 01, 2012
Habari ID: 2296136
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Alkhamisi 29 Machi alionana na Waziri Mkuu wa Uturuki Bw. Recep Tayyip Erdogan na ujumbe alioandamana nao ambapo alisisitiza juu ya wajibu wa kuimarishwa zaidi uhusiano wa nchi mbili hizi za Kiislamu kadiri inavyowezekana
Alisema kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini vilivyo kwamba ushirikiano wa nchi hizi mbili una faida kubwa na kwamba katika jambo lolote ambalo nchi hizi zinashirikiana basi huwa ni kwa faida ya Iran na Uturuki na ni kwa manufaa pia ya ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi mmoja maalumu wa Haram ya Imam Ridha AS mjini Mash-had, kaskazini mashariki mwa Iran, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria nafasi kubwa sana iliyopo kwa ajili ya kupanuliwa ushirikiano wa nchi mbili kwa njia bora zaidi hususan katika upande wa mafuta na gesi na kuongeza kuwa, Iran ni nchi tajiri sana duniani katika upande wa vyanzo vya mafuta na gesi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia hali tata sana iliyopo katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika hivi sasa na kusisitiza kuwa, kwa rehema za Mwenyezi Mungu hadi hivi sasa matukio yote yaliyotokea kwenye eneo hili yamekuwa ni kwa faida ya Uislamu na Waislamu na Inshaallah katika siku za usoni pia hali itakuwa vivyo hivyo.
Ameongeza kuwa, suala muhimu la kufanya hivi sasa katika mazingira haya tata na nyeti ni kuhakikisha kuwa nchi zilizo huru zinachukua misimamo iliyo sahihi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia jinsi madola ya kibeberu duniani na hasa Marekani yanavyoziangalia nchi za eneo hili kuwa ni kama nyenzo na vyombo tu vya kufanikishia malengo yao haramu na kukumbusha kuwa, hakuna taifa lolote lile linalohesabiwa na Marekani kuwa ni taifa huru.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, Wamarekani wanaamiliana na nchi zote duniani kwa namna hiyo hiyo, hivyo kuna wajibu wa kuzingatia kwanza maslahi ya nchi za Kiislamu katika maamuzi yoyote yanayochukuliwa na mataifa ya Kiislamu.
Aidha ameashiria kuweko wanasiasa wenye misimamo ya Kiislamu katika nafasi za juu za uongozi nchini Uturuki na kusisitiza kwamba, ni jambo lililo wazi kabisa kwamba jambo hilo halizifurahishi hata kidogo Marekani na nchi za Magharibi lakini kwa upande wake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafurahi sana kuona ndugu zake Waislamu wako katika nyadhifa za juu kabisa kwenye uongozi wa Uturuki kwa kiwango kile kile ambacho mabeberu wanachukizwa na jambo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia hali ya kisiasa nchini Syria na huku akiashiria kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga kwa nguvu zake zote mpango wowote ule unatoka kwa Wamarekani kuhusiana na kadhia ya Syria amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuliunga mkono na kulitetea taifa la Syria kutokana na kuwa kwake katika njia ya muqawama wa kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba Tehran inapinga uingiliaji wa aina yoyote ile wa vikosi vya kigeni katika masuala ya ndani ya Syria.
Ameongeza kuwa, sisi siku zote hizi tumekuwa tukiunga mkono marekebisho nchini Syria na tayari mabadiliko na marekebisho ya kisiasa yameanza kufanyika nchini humo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uturuki Bw. Recep Tayyip Erdogan ameelezea kufurahishwa kwake sana na kupata kwake fursa ya kuonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na huku akiashiria uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Iran na Uturuki amesema kuwa, Uturuki inaamini kwamba uhusiano huo mkongwe na wa kihistoria unapaswa kutumika vizuri kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa nchi mbili hasa hasa katika upande wa kushirikia kwenye masuala ya kimsingi kabisa.
Aidha Waziri Mkuu wa Uturuki ameutaja muundo wa ujumbe alioandamana nao katika safari yake ya kutembelea Iran kuwa unaonesha jinsi Uturuki inavyolipa uzito wa hali ya juu suala la kustawisha uhusiano kati yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na huku akiashiria hali inayotawala hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu amesema, eneo hili hivi sasa limo katika hali tata na nzito sana na kwamba ana matumaini Waislamu wataweza kuvuuka kipindi hiki kwa salama.
976290
captcha