Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu vina uzoefu mkubwa na wenye thamani wa miaka 8 ya kujitetea kutakatifu na tajiriba hiyo ya thamani inapaswa kutumiwa na kungaliwa upya.
Amesema kuwa tajiriba ya miaka ya kujitetea kutakatifu ni ya aina yake katika historia ya nchi hii. Ameongeza kuwa katika kipindi hicho cha miaka 8 madola yote makubwa duniani ya Mashariki na Magharibi na nchi waitifaki wao yalisimama katika safu moja dhidi ya Iran na kuupa utawala wa Baathi wa Iraq silaha za kisasa kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa nchi za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu hazikusita hata kuupa silaha za kemikali utawala wa Baathi wa Iraq kwa shabaha ya kuupigisha magoti mfumo wa Kiislamu nchini Iran.
Ayatullah Ali Khamenei ameongeza kuwa licha ya njama na misaada hiyo yote madola makubwa hayakuweza kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na ukurasa huo wa historia ya Iran ni tajiriba na uzoefu wenye thamani kubwa mikononi mwa jeshi la nchi hii.
Amesema kuwa saada na maendeleo vinapatikana kwa kuwa na subira na mapambano kwa ajili ya kuvuka kwa mafanikio vipindi mbalimbali vya historia. Ameongeza kuwa taifa la Iran lenye uzoefu wenye thamani kubwa kama Mapinduzi ya Kiislamu, vita vya kujitetea kutakatifu na nafasi nzuri ya sasa, litaweza kuvuka kwa fahari kipindi cha sasa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria vitisho vinavyotolewa na maadui wa taifa la Iran na kusema kuwa, vitisho hivyo ni kielelezo cha nguvu na uwezo wa Mfumo wa Kiislamu hapa nchini, kwani kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isingekuwa na nguvu na taathira kubwa, basi wale wanaolitakia mabaya taifa la Iran wasingepaparika huku na kule wakijaribu kutoa pigo dhidi ya Iran.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei ametilia mkazo umuhimu wa nguvu kazi katika vikosi vya jeshi la Iran na kusisitiza juu ya udharura wa kutotosheka na maendeleo ya sasa na kulindwa moyo wa kujitetea kutakatifu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, mkuu wa vikosi vya majeshi ya Iran Jenerali Feiruzabadi alitoa ripoti kuhusu utayarifu wa kujihami wa jeshi hilo na mipango yake katika mwaka huu mpya. 978690