IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kuondoka askari wa Marekani nchini Iraq ni miongoni mwa mafanikio ya serikali ya nchi hiyo

17:48 - April 23, 2012
Habari ID: 2311032
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki aliyeko safarini hapa nchini na ujumbe unaoandamana naye.
Ayatullah Khamenei ameashiria uwezo unaoongezeka siku baada ya siku wa Iraq katika ulimwengu wa Kiarabu na eneo la Ghuba ya Uajemi na akasema suala hilo linaifurahisha mno Jamhuri ya Kiislamu. Ameongeza kuwa juhudi za kuzidisha uwezo wa Iraq hususan kupitia njia ya kuzidisha jitihada za kielimu na kuanzisha harakati ya ujenzi wa maeneo yote ya Iraq zitazidisha mafanikio na nafasi nzuri ya serikali ya Iraq.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa baadhi ya masuala yaliyotokea katika miezi ya hivi karibuni ni dhihirisho la uwezo wa taifa na serikali ya Iraq katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu. Ameongeza kuwa kuondoka kikamilifu wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ni miongoni mwa masuala na matukio hayo muhimu sana na ni mafanikio makubwa ambayo yamepatikana kutokana na kusimama kidete serikali na kudhihirisha irada na azma ya taifa zima la Iraq.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kufanyika mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Kiarabu mjini Baghdad ni miongoni mwa mambo yanayotayarisha uwanja wa kupata nguvu nchi ya Iraq. Ameongeza kuwa baadhi ya pande zilifanya njama kubwa za kuidhihirisha Iraq kuwa iko nje ya ulimwengu wa Kiarabu lakini baada ya kufanyika mkutano wa viongozi wa nchi za wanachama katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Baghdad, sasa Iraq inaongoza jumuiya hiyo na Waziri wake Mkuu ndiye kiongozi wake.
Ameashiria pia historia na nafasi ya siku yingi ya Iraq katika ulimwengu wa Kiarabu na akasisitiza kuwa, kwa kutilia maanani historia hiyo na vipawa vya kimaumbile na kibinadamu vya Iraq, halitakuwa jambo gumu kwa nchi hiyo kupata tena nafasi yake halisi iliyokuwa nayo huko nyuma.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo kwamba uwezo unaoongezeka kila siku wa Iraq una maadui na ameongeza kuwa, uwezo wa kila nchi unahitajia mambo na nyenzo kadhaa, muhimu zaidi ikiwa ni maendeleo ya kisayansi na kielimu, ujenzi na kuwahudumia wananchi.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria pia uzoefu na tajiriba nzuri ya Iran katika harakati ya maendeleo ya sayansi na matunda makubwa ya wasomi hapa nchini na akasema kuwa, harakati kubwa ya kielimu inapaswa kuanzishwa huko Iraq nchi ambayo ni kituo kikuu cha vipawa vya kielimu katika ulimwengu wa Kiarabu, na vyuo vikuu na wasomi wanapaswa kuelekezwa katika upande wa jihadi ya kielimu.
Kuhusu suala la ujenzi wa Iraq, Ayatullah Khamenei amesema, kuna udharura wa kuanzisha harakati ya ujenzi mpya wa nchi hiyo na kutoa huduma kwa wananchi kote nchini kupitia njia ya kuwatayarisha vijana na kubuni nyanja zinazohitajika kwa ajili ya lengo hilo.
Mwishoni mwa mazungumzo hayo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa mustakbali wa Iraq utang'ara zaidi kuliko hali inayoshuhudiwa kwa sasa nchini humo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki amesema kuwa amefurahishwa na kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameashiria mazungumzo yake na viongozi mbalimbali hapa nchini na akasema kuwa kwa baraka zake Allah, uhusiano wa Iran na Iraq umeimarika zaidi katika nyanja mbalimbali na jumbe za masuala ya biashara na viwanda zimekuwa zikifanya safari katika nchi hizi mbili.
Waziri Mkuu wa Iraq amesema anatarajia kuwa mazungumzo ya Tehran yatatayarisha uwanja mzuri wa kupanua zaidi ushirikiano wa Iran na Iraq. 992209


captcha