Amesema kuwa kati ya minyororo mingi ya nuru ya kubaathiwa mtukufu huyo jamii ya mwanadamu ya leo inahitaji zaidi vitu viwili ambavyo ni kuhuishwa tena fikra na kusafishwa akhlaki na maadili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka kwa taifa la Iran na umma wa Kiislamu kwa ujumla kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu ya kupewa utume Nabii Muhammad (saw) na akasema kuwa, kasi ya mataifa ya Kiislamu kuelekea kwenye dini ya Nabii Muhammad (saw) ni kielelezo kwamba baada ya uzoefu wa muda mrefu, mataifa mbalimbali yameelewa kwamba mifumo ya kimaada ya mashariki na magharibi haiwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu na kwamba ni mafundisho ya shakhsia huyo pekee ndiyo yanayoweza kumfikisha mwanadamu kwenye saada na maendeleo ya kweli.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mzizi wa matatizo ya jamii ya mwanadamu ni kuwa mbali na masuala mawili muhimu ya kubaathiwa Mtume ambayo ni fikra na kutakasa nafsi. Ameongeza kuwa lengo kuu la kubaathiwa na kutumwa mtukufu huyo ni kuwaokoa wanadamu kutoka kwenye matatizo na udhaifu wa kiakhlaki, na kutimia kwa jambo hilo kunatayarisha uwanja nzuri wa kuondolewa matatizo makuu ya mataifa mbalimbali.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhuishwa nguvu ya akili na kutafakari ni miongoni mwa malengo mengine muhimu na ya kimsingi ya kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Ameongeza kuwa hii leo jamii ya mwanadamu inahitajia mno kutafakari, kutumia akili na mantiki na kutafuta mzizi wa matatizo mbalimbali yanayoyazonga mataifa mbalimbali kutoka pembe zote.
Amekumbusha mauaji na dhulma ya waziwazi inayofanywa na madola makubwa katika baadhi ya nchi za eneo hili na kusema kuwa, mwanadamu hana nafasi yoyote katika mtazamo uliojaa giza wa madhalimu wa kimataifa, na katika kadhia ya matatizo ya kiuchumi ya nchi za Magharibi dunia inashuhudia kwamba, madola ya kibeberu yanafanya jitihada za kutatua matatizo ya wamiliki wa mabenki na makampuni ya mfumo wa kibepari na si kwa ajili ya kuondoa matatizo ya wananchi.
Ayatullah Khamenei ameyataka tena mataifa mbalimbali kutafakari kuhusu ukweli huo wa wazi na kusema kuwa, chanzo cha matatizo hayo yote ni udhibiti wa mfumo wa kibepari juu ya dunia na kuwepo kambi mbili za mabeberu wanaodhibiti na watu wanaokubali kudhibitiwa; na ufumbuzi wa suala hilo ni mataifa mbalimbali kujiondoa katika hali ya kudhibitiwa na kutokuwa na harakati.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria jitihada kubwa zinazofanywa na mabeberu wa kimataifa kwa ajili ya kudhibiti na kupotosha mapinduzi ya mataifa ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na akasema kuwa, mataifa mbalimbali yanapaswa kusimama kidete kwa kutegemea hiba ya kutafakari, akili yaliyotunukiwa na Mola Karima na kwa kutarajia ahadi ya msaada wake Mwenyezi Mungu, na kujiamualia mustakbali wao kwa kupambana na mabeberu hao.
Amesema kuwa heshima na uwezo wa taifa kubwa la Iran ni mfano wa wazi wa matokeo ya kusimama kidete na kupigana jihadi. Ameashiria ushirikiano wa madhalimu wa kimataifa katika kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu na akasema: “Katika kipindi chote cha miaka 33 iliyopita taifa angavu na nchi hii ya Iran imekuwa ikishambuliwa kwa njama za pande zote za madola yote ya kibeberu duniani ili asaa kigezo hicho bora na hai cha kusimama imara na maendeleo (Jamhuri ya Kiislamu) kisiwe mfano wa kuigwa na mataifa mengine; hata hivyo na kwa baraka zake Mwenyezi Mungu mara hii pia njama zote za mabeberu hao za kutaka kulifuta taifa la Iran katika medani zitashindwa na kugonga mwamba.”
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kutimia kwa ahadi ya nusra na msaada wa Mwenyezi Mungu kunahitajia jihadi, harakati na kuwa tayari kukabiliana na hatari. Amesoma aya kadhaa za Qur’ani zinazozungumzia maudhui hiyo na kuongeza kwamba, kuwa muumini peke yake hakutoshi kwa ajili ya kutimia ahadi ya ushindi, bali jihadi na subira pia vinahitajika.
Amewahutubu maadui wa utawala wa Kiislamu akisema: “Jifunzeni kutokana na tajiriba iliyofeli ya kukabiliana na taifa shupavu na lenye subira la Iran na tambueni kwamba kiburi, kujiona ya kwamba mko juu ya watu wengine na matarajio yasiyokuwa na maana mkabala wa taifa lililojitambua na kujifunza kusimama kidete na umoja kutoka kwenye Qur’ani, haviwezi kufua dafu.”
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria siasa za maadui wa Uislamu za kuwafanya Shia na Suni waogopane na kusisitiza juu ya umuhimu wa umoja katika ulimwengu wa Kiislamu. Amekosoa vikali fitina za kuzusha hitilafu na mifarakano zinazofanywa na baadhi ya watu na kusema: “Watu ambao kimsingi hawaukubali Uislamu na hawaujui Ushia wala Usuni wamekuwa wakieleza wasiwasi wao kuhusu suala la kuenea Ushia na hivyo kuzusha moto wa mifarakano kwa mujibu wa matakwa ya mashirika ya kijasusi ya mabeberu.”
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei ameyausia mataifa ya Waislamu kutumia akili na mantiki, kuungana na kusimama kidete na akasema anatarajia kuwa chini ya kivuli cha baraka zake Mwenyezi Mungu, umma wa Kiislamu utawashinda maadui na kutimiza kikamilifu malengo ya kubaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad (saw).
Mwanzoni mwa kikao hicho kilichohudhuriwa na Rais wa Jamhuri, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu, Rais Mahmoud Ahmadinejad alitoa hotuba fupi akiwapongeza Waislamu kwa mnasaba wa siku ya leo ya kuadhimisha tukio la kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Amesema kuwa mwanadamu wa leo anahitajia sana maarifa ya Mwenyezi Mungu na ujumbe wa tukio la kubaathiwa Mtume wa mwisho Muhammad (saw) kuliko wakati wowote mwingine.
Amesema imethibitika kuwa madola ya kimaada hayawezi kudhamini mahitaji ya jamii ya mwanadamu na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa ahadi za Mwenyezi Mungu na chini ya kivuli cha mwamko na jihadi ya mataifa mbalimbali, jamvi la mabeberu na Wazayuni litakunjwa na kutafunguliwa njia ya amani, utulivu na maendeleo ya mwanadamu.
1032607