IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Nguvu zote tatu za dola ziko katika handaki moja la kulinda Uislamu, taifa na uhuru wa Iran

21:53 - June 27, 2012
Habari ID: 2356111
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo (Jumatano 27 Juni) amehutubia mkutano wa maafisa wa Vyombo vya Sheria hapa nchini akisema kuwa kuboresha kazi za chombo hicho kwa lengo la kutekeleza uadilifu katika jamii ndio lengo muhimu zaidi.
Ayatullah Khamenei amebainisha masuala muhimu kwa ajili ya kufikia lengo hilo na kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi zote hususan nguvu tatu kuu za dola katika hali ya sasa ni wajibu na jambo la dharura. Amesema Serikali, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na Vyombo vya Sheria vyote viko katika handaki moja la kulinda Uislamu, taifa la Iran na uhuru na utambulisho wa nchi hii mkabala wa njama za pande zote zinazofanywa na madola ya kibeberu, na pande zote hizo zinapaswa kusaidiana na kujiepusha na masuala yanayozusha hitilafu.
Katika mkutano huo ambao umefanyika kwenye Haram ya Imam Ridhaa (as) mjini Mash'had kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kuuawa shahidi Ayatullah Muhammad Behesti aliyekuwa Mkuu wa Vyombo vya Sheria hapa nchini, Ayatullah Khamenei amesema kuwa kuboreshwa Vyombo vya Sheria na kutimiza uadilifu mahakamani kama unavyohimiza mfumo wa Kiislamu, kutatayarisha uwanja wa kutatuliwa matatizo mengi na kuondolewa ufisadi. Ameongeza kuwa kwa kutilia maanani suhula zinazopatikana hapa nchini hapana shaka kuwa tunaweza kutimiza lengo kubwa la kuboresha Vyombo vya Sheria kwa kufanya juhudi kubwa na kutumia suhula zilizopo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha miundombinu inayohitajika kwa ajili ya kuboresha Vyombo vya Sheria hapa nchini na kusema: "Kubuniwa mpango kamili na wa pande zote ni miongoni mwa kazi muhimu zaidi za kuboresha chombo hicho."
Amesema kuwa kubuni mpango kamili ni kazi muhimu sana lakini muhimu zaidi ni utekelezaji wake na harakati yenye kasi kubwa ya kuufanyia kazi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa maana ya harakati yenye kasi kubwa si kufanya kazi ovyo bila ya mantiki, kwa msingi huo kuna ulazima wa kazi hiyo kufanyika kwa uangalifu na kwa makini lakini bila ya kuchelewa.
Ayatullah Khamenei amesema, kuwa makini katika kutoa hukumu mahakamani ni moja kati ya mahitaji muhimu ya koboreshwa Vyombo vya Sheria. Ameongeza kuwa hukumu zinazotolewa na mahakama zinapaswa kuwa makini kwa kadiri kwamba zikiwekwa mbele ya wataalamu wa masuala ya fiqhi (sheria za Kiislamu) na masuala ya sheria basi majaji waliotoa hukumu hizo hawatakuwa na wasiwasi wa aina yoyote.
Ayatullah Khamenei amesema uamuzi wa kuwepo umakini katika kutoa hukumu mahakamani unapaswa kuenea katika mahakama zote kwani kutenguliwa mara kwa mara maamuzi ya mahakama za mwanzo ni ishara ya kuwepo mapungufu na kasoro katika hukumu na maamuzi hayo.
Amesisitiza juu ya ulazima wa kupunguzwa matumizi ya jela kama adhabu kwa watu wanaopatikana na hatia ikiwa ni kama sera kuu ya sasa ya Vyombo vya Mahakama na kusema kuwa, adhabu ya kifungo jela inapaswa kupunguzwa kadiri inavyowezekana kwa sababu jela ni jambo lisilotakikana na lenye taathira mbaya kwa wafungwa, familia zao na hata mazingira ya kazi ya watu hao.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kulinda heshima za watu ni miongoni mwa mambo muhimu na kusisitiza kuwa, kwa bahati mbaya sehemu kubwa ya suala hili inafungamana na tetesi na uvumi unaotolewa na baadhi ya magazeti na mitandao ya intaneti, na Vyombo vya Sheria havipaswi kuathiriwa na uvumi huo kwa njia yoyote ile.
Amesisitiza pia juu ya umuhimu wa kutayarishwa maafisa kwa ajili ya vyeo vya uongozi na majukumu ya ngazi za juu katika taasisi ya Vyombo vya Sheria kwa ajili ya kuboresha kazi za taasisi hiyo.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa ushirikiano wa nguvu tatu kuu za dola (Serikali, Bunge na Mahakama) ni miongoni mwa mahitaji ya kipindi cha sasa hapa nchini. Amesema kuwa hii leo madola ya kidhalimu duniani yameelekeza nguvu zao katika suala la kukwamisha na kutia doa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na harakati yake kubwa ambayo inatoa ilhamu kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema mwamko wa sasa katika ulimwengu wa Kiislamu na hamu kubwa ya watu wengi ya kuelekea kwenye thamani za Kiislamu ni matokeo ya harakati inayosonga mbele ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Kiislamu. Ameongeza kuwa mafanikio ya aina yoyote au maendeleo ya kisayansi ya utawala wa Kiislamu hapa nchini, harakati kubwa za kijamii za wananchi kama uchaguzi unaoshirikisha idadi kubwa ya wananchi na vilevile kusimama kidete na mapambano ya Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya dhulma za ubeberu, yote hayo yanayahamasisha mataifa mbalimbali kwa ajili ya kudumisha uhuru wao kwa misingi ya Uislamu; kwa msingi huo madola makubwa ya kidhalimu yameelekeza nguvu zao zote kwa taifa la Iran ili yalemaze na kuatilisha kituo hicho kikuu cha harakati ya mwamko.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema makelele mbalimbali ya kipropaganda dhidi ya utawala wa Kiislamu wa Iran hususan katika uwanja wa masuala ya haki za binadamu na nishati ya nyuklia yanatathminiwa katika fremu hiyo. Amesisitiza kuwa madola hayo ya kibeberu ambayo yanawaongopea walimwengu kwa kujipajika jina la 'jamii ya kimataifa', yanafanya njama kubwa za kutenganisha baina ya Jamhuri ya Kiislamu na nguzo yake kuu yaani wananchi.
Akifafanua zaidi njama hiyo Ayatullah Khamenei amesema kuwa mlengwa mkuu wa vikwazo vya madola hayo ya kibeberu ni wananchi wa Iran ili mashinikizo hayo yawachoshe wananchi na hatimaye wajitenge na utawala wa Kiislamu; hata hivyo na kwa baraka zake Mwenyezi Mungu njama hizo pia zitashindwa kwa sababu mabeberu hao hawajawatambua vyema wananchi na viongozi wa Iran.
Amesema wananchi wa Iran wametambua vyema njama hizo za maadui na kwa sababu hiyo wamekuwa wakihudhuria kwa wingi katika medani mbalimbali huku viongozi wa nchi wa wakifanya jitihada kubwa kutekeleza vyema majukumu yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia njama za pande zote za Marekani za kutaka kuizingira Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema kuwa wao wenyewe Wamarekani wanazongwa na matatizo makubwa na yasiyokuwa na tiba huku Iran ikiwa na suhula zote zinazohitajika kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Khamenei amesema suhula na utajiri wa ndani ya nchi, wananchi wema, nguvu ya kibinadamu na kutokuwa na deni la kimataifa ni miongoni mwa nukta chanya za Iran. Ameongeza kuwa katika hali ya sasa adui ametumbukia katika medani kwa nguvu zake zote ili apunguze uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu wa kutumia rasilimali hizo, lakini kwa upande mwingine viongozi wa Iran wanafanya jitihada kubwa kwa ajili ya kuzima njama hizo.
Ayatullah Khamenei amesema katika hali kama hiyo ni wajibu na jambo la dharura kuwepo ushirikiano kati ya taasisi zote na nguvu tatu kuu za dola.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mtengano wa aina yoyote kati ya taasisi na nguvu tatu kuu za dola utakuwa na madhara kwa nchi, kwa msingi huo pande hizo zote zinapaswa kushirikiana.
Ayatullah Khamenei amesema Serikali, Bunge na Mahakama vyote viko katika handaki moja nayo ni handaki ya kulinda Uislamu, taifa la Iran na uhuru na utambulisho wa nchi hii; kwa msingi huo ni jambo la msingi na muhimu kusaidiana na kuondoa hitilafu kati yao.
Amesema iwapo kila moja kati ya pande hizo itaingilia daima kazi za upande mwingine, tatizo haliwezi kutatuliwa, hivyo basi kila upande kikiwemo Chombo cha Sheria unapaswa kutekeleza kikamilifu wajibu na kazi zake na kushirikiana na pande nyingine.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena juu ya suala la kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwasaidia watu wanaofanya juhudi kubwa katika njia ya haki. Vilevile amemshukuru Mkuu wa Vyombo vya Sheria, maafisa, majaji na wafanyakazi wote wa chombo hicho kwa jitihada zao kubwa.
Mwanzoni mwa mkutano huo Mkuu wa Vyombo vya Sheria nchini Iran Ayatullah Amoli Larijani alitoa ripoti kuhusu utendaji wa miaka mitatu wa chombo hicho.



captcha