IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Juhudi za wanawake wasomi za kuhuisha utambulisho wa Kiislamu ni huduma kubwa zaidi kwa umma wa Kiislamu

12:32 - July 12, 2012
Habari ID: 2366818
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo amehutubia hadhara ya wasomi na wanajihadi wa kike wa ulimwengu wa Kiislamu akiitaja nafasi na mchango wa wanawake katika harakati kubwa ya mwamko wa Kiislamu kuwa hauna mbadala.
Ameashiria uzoefu mkubwa wa mahudhurio ya wanawake wa Iran katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kudumishwa mapinduzi hayo hapa nchini na akasisitiza kuwa kudumishwa, kuimarishwa na kupanuliwa zaidi mahudhurio hayo ya wanawake katika harakati yenye baraka ya mwamko wa Kiislamu kutafuatiwa na ushindi mwingi kwa mataifa ya Waislamu.
Ayatullah Ali Khamenei ametaja mahudhurio ya wanawake wasomi na Waislamu kutoka nchi 85 duniani katika Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake na Mwamko wa Kiislamu kuwa ni fursa muhimu sana kwa ajili ya kutambuana na kujuana. Amesema kuwa kujuana na ushirikiano uliopatikana katika mkutano huu ni utangulizi wa kuanzisha harakati yenye taathira na itakayobakia siku zote katika mwenendo wa kuhuisha utambulisho na shakhsia ya wanawake Waislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia jitihada za pande zote za miaka 100 za nchi za Magharibi kwa ajili ya kuwaweka wanawake Waislamu mbali na utambulisho wao wa Kiislamu na akasema juhudi zinazofanywa na wanawake Waislamu kwa ajili ya kuhuisha utambulisho huo ni huduma kubwa zaidi kwa umma wa Kiislamu, kwa sababu kuwa na utambulisho, kuwa makini na kuona mbali kwa wanawake Waislamu kutaacha taathira kubwa katika harakati za mwamko wa Kiislamu na kuupa umma wa Kiislamu izza na heshima.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa, mtazamo wa Magharibi kwa mwanamke ni mtazamo wa kudhalilisha na kuongeza kuwa, katika utamaduni wao Wamagharibi wanamtambua mwanamke kuwa ni bidhaa na chombo cha kushibisha matakwa ya mwanaume na wanatumia kila kitu kwa ajili ya kutimiza lengo hilo; na wakati huo huo wanaupachika mtazamo huo ulioporomoka, nakisi na wa kupotosha kuwa ni uhuru, kama ambavyo wanazitaja jinai mbalimbali kama mauaji, uporaji wa utajiri wa mataifa na nchi mbalimbali, kutuma majeshi katika nchi hizo na kuanzisha vita kwa kutumia majina ya hadaa kama operesheni za ukombozi, kutete haki za binadamu na demokrasia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mtazamo wa Uislamu kwa mwanamke unakabiliana na ule wa Magharibi. Ameongeza kuwa Uislamu una mtazamo wenye izza, heshima na wa ustawi kwa mwanamke na unampa mwanamke utambulisho na shakhsia huru na inayojitegemea.
Akiashiria tajiriba na uzoefu wenye mafanikio wa wanawake wasomi na wenye imani wa Iran katika nyanja mbalimbali za kielimu, kisiasa na masuala ya uendeshaji, Ayatullah Khamenei amesema kuwa mwanamke katika mazingira ya Kiislamu hupata ustawi wa kielimu na shakhsia kubwa na ya kisiasa na kuwa katika safu ya mbele katika masuala muhimu zaidi ya kijamii; hata hivyo hubakia kuwa mwanamke na kujifaharisha kwa masuala hayo.
Amesema kuwa kusambaratika familia huko Magharibi na ongezeko la watoto wasiokuwa na utambulisho ni miongoni mwa matokeo ya mtazamo wa utamaduni wa Magharibi kwa mwanamke. Ameongeza kuwa Magharibi itapata kipigo kikubwa zaidi kutokana na suala hili na hatimaye kusambaratika katika mwenendo wa hatua kwa hatua wa taathira za matukio ya kijamii.
Ayatullah Ali Khamenei amesema, katika mtazamo wa Uislamu mwanamke na mwanaume wana sifa za pamoja za kibinadamu na kuongesza kuwa, kila mmoja kati ya mwanamke na mwanaume ana mchango na nafasi yake makhsusi katika kudumisha uumbaji, kulea na kustawisha mwanadamu na katika harakati ya historia kwa mujibu wa maumbile yake ya kimwili, na hapana shaka kuwa nafasi ya mwanamke yaani kudumisha kizazi cha mwanadamu ni muhimu zaidi kuliko ya mwanaume.
Ameongeza kuwa sheria za Uislamu kuhusu familia na mipaka ya mahusiano ya kingono vinapaswa kuchunguzwa na kufahamika kwa mujibu wa mtazamo huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuweka wazi na kudhihirisha nafasi ya mwanamke katika mtazamo wa Kiislamu ndio wajibu mkubwa zaidi wa wanawake wasomi na bingwa wa dunia ya Kiislamu. Amezungumzia mchango mkubwa wa wanawake katika matukio ya miaka 33 ya hivi karibuni nchini Iran na kusema kuwa mchango wa wanawake katika mageuzi ya kijamii, mapinduzi na harakati za mwamko wa Kiislamu pia ni muhimu sana, kwa sababu mahala popote wanawake wanaposhiriki katika harakati ya kijamii sambamba na kuwa makini, harakati hiyo hupata dhamana ya ushindi; na uhakika huu unazidisha udharura wa kudumishwa na kuimarishwa mahudhurio ya wanawake katika matukio ya Misri, Libya, Yemen, Bahrain na katika maeneo mengine ya dunia ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mwamko wa Kiislamu ni harakati ya kustaajabisha na isiyokuwa na kifani. Amesisitiza kuwa harakati hiyo inaweza kubadili mkondo wa sasa wa historia kwa sharti la kutambua vyema hatari na vizingiti vinavyoikabili.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza mapinduzi ya mataifa ya Waislamu huko kaskazini mwa Afrika na maeneo mengine kunakoshuhudiwa mwamko wa Kiislamu na akasema kuwa, mabeberu wanaoongozwa na Marekani na Uzayuni ambao wameshtushwa na harakati hiyo kubwa wanafanya kila wawezalo kuzima harakati hiyo na kudandia mawimbi yake.
Amesema miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na mabeberu hao kuzima harakati ya mwamko wa Kiislamu ni kupunguza ari za mataifa mbalimbali ya kudumisha mahudhurio yao katika medani za mapambano na kuwashughulisha watu wa matabaka mbalimbali na masuala ya hadaa au yenye kuzusha hitilafu. Amesisitiza kuwa iwapo mataifa ya Waislamu yatapambana na njama hizo na kuendelea kuwepo katika medani za mapambano, hapana shaka kwamba yatapata ushindi dhidi ya ulimwengu wa kibeberu; kwa sababu nguvu ya panga za mabeberu wote huwa butu mbele ya mahudhurio na imani ya mataifa mbalimbali.
Ameashiria pia njama za mara kwa mara na zilizoshindwa za maadui wa Uislamu na Iran katika kipindi chote cha miaka 33 iliyopita na kusema kuwa, katika siku hizi Wamagharibi wamekuwa wakipiga makelele mengi kuhusu suala la kuiwekea vikwazo Iran lakini hawaelewi kuwa wao wenyewe waliipa Iran kinga na chanjo kutokana na vikwazo vyao vya miaka 30 iliyopita dhidi ya nchi hii.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa taifa la Iran katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita limekabiliana na njama na vikwazo vyote kwa nafsi, mali na kila kilochoazizi kwa kadiri kwamba hii leo Iran ya Kiislamu imekuwa imara mara mia moja zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Ameashiria pia maendeleo makubwa ya Iran katika nyanja mbalimbali na kuwaambia wanawake wasomi wa dunia ya Kiislamu kwamba, hii leo mwanamke Muislamu wa Iran ana mahudhurio ya kujifaharisha katika nyanja zote za maendeleo na ustawi na wanawake wasomi hapa nchini ni miongoni mwa wanawake wenye imani kubwa na wanamapinduzi zaidi wa Kiirani. Ameongeza kuwa Magharibi inafanya jitihada za kudhihirisha uhakika huo kinyume chake kwa kutumia maelfu ya propaganda chafu na hujuma ya vyombo vya habari.
Ayatullah Khamenei amekumbusha njama zilizofeli za Magharibi kwa ajili ya kuizuia Jamhuri ya Kiislamu isiliunge mkono taifa la Palestina na akasema kuwa, Iran itaendelea kuwa bega kwa bega na pamoja na ndugu zake Waislamu licha ya mijada ya kupotosha kuhusua masuala ya Shia na Suni. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kwa baraka zake Mwenyezi Mungu, taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwa pamoja na kulitetea taifa la Palestina, mataifa yote yaliyoamka na kufanya mapinduzi na pamoja na watu wote wanaopambana na Marekani na Uzayuni, na katika suala hili haitajali yeyote au nguvu ya dola lolote.
Katika hadhara hiyo Bibi Hijazi, Katibu wa Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake na Mwamko wa Kiislamu ametoa hotuba fupi akisema kuwa wanawake 1200 wasomi na wanaharakati wa masuala mbalimbali kutoka nchi 85 duniani wameshiriki katika mkutano huo. Vilevile ametoa ripoti fupi kuhusu mijadala ya vikao vya kamisheni za mkutano huo wa kimataifa.
Vilevile Dakta Ali Akbar Velayati ambaye ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu amezungumzia mikutano minne ya kimataifa kuhusu mwamko wa Kiislamu iliyofanyika hadi hivi sasa tangu mwaka jana na akasema jumuiya hiyo inafanya jitihada za kuimarisha mazungumzo ya mwamko wa Kiislamu kupitia njia ya kuitisha mikutano hiyo.
Mwanzoni mwa mkutano huo washiriki kadhaa wa Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake na Mwamko wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali walitoa mitazamo yao mbele ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. 1050665
captcha