IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Mashinikizo ya adui hayatailazimisha Iran kubadili mahesabu yake

13:56 - July 26, 2012
Habari ID: 2377890
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo (Jumanne) amehutubia hadhara ya viongozi na maafisa wa mfumo wa Kiislamu hapa nchini na kusema kuwa siri ya harakati inayosonga mbele kwa kasi ya taifa na utawala wa Kiislamu hapa nchini katika kipindi cha miaka 32 iliyopita ni kuweka mbele malengo aali sambamba na kutilia maanani uhakika wa mambo.
Amezungumzia uwezo mkubwa wa taifa na utawala wa Kiislamu wa Iran na kubainisha udharura na njia za kukabiliana na changamoto tata za adui.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa ni jambo la dharura kuwa na ufahamu wa kina wa muundo nyeti sana wa kupigania malengo aali sambamba na kutilia maanani uhakika wa mambo. Ameongeza kuwa kuoanisha baina ya malengo sambana na kuzingatia uhakika wa mambo ni harakati ya jihadi katika fremu ya tadbiri ambayo sharti lake ni kuwa macho wananchi wote na viongozi na kushirikiana katika nyanja zote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria changamoto mbalimbali zilizoukabili mfumo wa Kiislamu hapa nchini tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na mauaji ya kigaidi, uasi wa kikaumu, vita vya kulazimishwa vya miaka 8, vikwazo vya mara kwa mara, matatizo ya mwezi Tir mwaka 1378 na matukio ya mwaka 1388 Hijria Shamsia na akasema kuwa, uwezo mkubwa wa taifa la Iran umeuwezesha utawala wa Kiislamu kuvuka changamoto zote hizo kwa mafanikio, kuwa imara na kupata nguvu zaidi katika kila kipindi kuliko kipindi cha kabla yake.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa sharti la kuvuka kwa mafanikio mashaka na matatizo makubwa katika harakati inayosonga mbele ya utawala wa Kiislamu nchini Iran ni kulindwa muundo wa kushikamana na malengo aali sambamba na kutilia maanani ukweli wa mambo na mtazamo sahihi kuhusu uwezo na suhula za nchi na taifa la Iran.
Akipinga madai ya baadhi ya watu anaosema kuwa kulinda malengo aali hakuoani na suala la kutilia maanani uhalisia wa mambo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, thamani na malengo mengi ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini ni miongoni mwa matakwa ya wananchi kwa msingi huo malengo hayo ni katika mambo halisi ya jamii.
Amesema kuwa heshima ya kitaifa, maisha yanayoambatana na imani, kushirikishwa wananchi katika uendeshaji wa masuala ya nchi, maendeleo ya pande zote, kujitegemea kiuchumi na kisiasa na kuwa na heshima kimataifa ni miongoni mwa matakwa halisi ya wananchi. Ameongeza kuwa matakwa hayo ya taifa ni sehemu ya malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na suala hilo linaonesha kuwa kushikamana na malengo hakupingani na suala la kutilia maanani uhalisia wa mambo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kushikamana na malengo aali bila ya kujali uhakika wa mambo na pasi na kutumia mbinu za kimantiki ni ndoto tupu. Ameongeza kuwa ili thamani na malengo hayo yasibakie kuwa nara tupu, viongozi pamoja na wananchi wanapaswa kuyafuatilia kwa njia madhubuti na ya kimantiki.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kupuuza uhakika wa mambo katika jamii hupelekea kufanya makosa katika kutoa maamuzi na makosa katika kuchagua njia. Ameongeza kuwa tunapaswa kufanya harakati zetu kwa mujibu wa kuzingatia uhakika wa mambo na ni muhimu sana kujiepusha kuteleza na sehemu gani tunaweza kuteleza katika njia hiyo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha baadhi ya mifano ya kuteleza na kusema maadui wa Mapinduzi ya Uislamu wanafanya njama za kuwaingiza viongozi na wananchi wa Iran katika makosa ya kimahesabu kwa kubuni mambo na kuyaonesha kuwa ni uhakika halisi.
Katika uwanja huo Ayatullah Khamenei ameashiria juhudi zinazofanywa na maadui za kutaka kudhihirisha uwezo wa taifa la Iran kuwa ni mdogo na kukuza uwezo wa kambi ya ubeberu na akasema: "Iwapo tutatekwa na harakati hizo za adui na tukakosea katika kutathmini uwezo wetu au katika kumuainisha adui, basi tutakuwa tumepotea njia."
Amekutaja kuikumbatia dunia na udhaifu katika upande wa matamanio ya kinafsi kuwa ni miongoni mwa vielelezo vya kuteleza ambavyo husababisha makosa wakati wa kutilia maanani hali halisi ya mambo na katika kuchagua njia sahihi.
Ayatullah Khamenei amesema, kuwa na fikra ya kufikia malengo aali bila ya kutoa gharama ni miongoni mwa maeneo ya kuteleza. Ameongeza kuwa kutilia maanani baadhi ya uhakika wa mambo na kufumbia mambo mengine ni kuteleza kwingine na lazima tuwe macho katika suala hilo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kutilia maanani uhakika wote wa mambo hapa nchini kunatia matumaini makubwa na kuongeza kuwa mambo hayo yanaonesha kwamba japokuwa njia ya taifa la Iran kuelekea kwenye malengo yake aali ina changamoto nyingi lakini hakuna mkwamo katika njia hiyo.
Ameashiria njama za maadui za kutaka kuonesha kwamba taifa la Iran limegonga mwamba na kuongeza kuwa: "Wanasema waziwazi kuwa viongozi wa Iran wanapaswa kulazimishwa kutazama upya katika mahesabu yao kwa kuzidisha mashinikizo na vikwazo; hata hivyo kutazama ukweli wa mambo kunatufanya tusibadili mahesabu yetu bali kunatupelekea kudumisha njia ya taifa la Iran kwa matumaini zaidi."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha baadhi ya ukweli wa mambo kuhusu hali ya sasa na akasema kukabiliana kwa madola kadhaa ya kibeberu na Jamhuri ya Kiislamu na mashinikizo yao makubwa yanayoongezeka kila siku ni uhakika ambao haupaswi kufumbiwa macho.
Amesema kuwa nchi hizo za kibeberu ambazo zina uwezo mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na wa vyombo vya habari zinatumia vyombo vyao vya habari na vya propaganda vyenye nguvu kwa ajili ya kujitangaza kuwa ndio jamii ya kimataifa, suala ambalo halina ukweli wowote.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa nchi hizo chache za kibeberu zina majeshi ambayo kama si kuungwa mkono na Marekani basi majeshi hayo ni sawa na sifuri na hayana nafasi yotote katika mahesabu ya kimataifa.
Ameongeza kuwa uhakika mwingine wa mambo ni kuwa uadui wa nchi hizo kadhaa za kibeberu dhidi ya utawala wa Kiislamu nchini Iran unahusiana na asili ya kuwepo utawala huu lakini zinafanya juhudi za kudhihirisha kwamba sababu ya uhasama wao dhidi ya taifa la Iran ni suala la nyuklia na eti kutetea haki za binadamu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa kutokana na faili jeusi la haki za binadamu la Marekani, Uzayuni, Uingereza na mabeberu wengine, hakuna mtu anayeamini madai yao ya uongo katika uwanja huo.
Ayatullah Khamenei amesema ukweli wa mambo ni kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya taifa la Iran yameiondoa nchi hii muhimu katika makucha ya mabeberu na kuzusha mwamko mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa sababu hiyo mabeberu wanafanya jitihada za kutoa pigo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kutoa somo kwa mataifa mengine ili yasiifanye Iran kuwa kigezo bora cha kuiga.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, moja ya hakika zilizopo hivi sasa ni kuwa changamoto za sasa mbele ya utawala wa Kiislamu wa Iran si jambo jipya. Ameongeza kuwa wakati fulani meli za Iran katika Ghuba ya Uajemi zilikuwa zikishambuliwa na bandari za mafuta na viwanda vilikuwa vikipigwa mabomu na maadui, lakini hii leo maadui hao wanaoitakia mabaya Iran ya Kiislamu hawathubutu kukaribia ardhi ya Iran.
Ameyataka maendeleo ya daima ya utawala wa Kiislamu wa Iran katika nyanja mbalimbali hususan katika taaluma ngumu na zinazohodhiwa na nchi kadhaa tena katika mazingira ya vikwazo na vitisho kuwa ni miongoni mwa hakika za wazi. Amesema kuongezeka uwezo na hali ya kujiami kwa utawala wa Kiislamu hapa nchini mkabala wa vitisho mbalimbali ni miongoni mwa hakika za wazi. Amesema ukweli ni kuwa kambi inayokabiliana na mfumo wa Kiislamu wa Iran ikiongozwa na Marekani na Wazayuni imedhoofika mno ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kuongezeka hatari inayoukabili utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya matukio na mapinduzi ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, kushindwa utawala huo katika vita vya siku 33 huko Lebanon na vile vya siku 22 huko Ghaza, hatima ya Marekani huko Iraq, na matatizo yake yasiyoisha huko Afghanistan na kushindwa kwa siasa za serikali ya Washington katika Mashariki ya Kati ni mifano ya wazi ya kudhoofika kambi ya mabeberu hao.
Ayatullah Khamenei amesema, migogoro iliyopo katika nchi za Magharibi zinazopinga utawala wa Kiislamu nchini Iran ni miongoni mwa hakika ambazo haziwezi kufumbiwa macho. Amesema kuwa hatari kubwa ya mgogoro wa kiuchumi ndani ya Umoja wa Ulaya na eneo la sarafu ya Euro, ukosefu wa uthabiti katika nchi kadhaa za Ulaya na kuondoka madarakani serikali kadhaa, nakisi kubwa ya bajeti ya Marekani na kujitokeza harakati ya 99 inayopinga ubepari ni matukuio muhimu ambayo hayapaswi kupuuzwa.
Amesema matatizo ya kiuchumi ya nchi za Magharibi yanatofautiana sana na matatizo ya kiuchumi ya Iran, kwa sababu matatizo ya Iran ni kama matatizo ya vifundo vya kamba ya mpanda mlima ambaye yuko katika harakati ya kupanda juu kuelekea kileleni; mpanda mlima huyo hupata mashaka lakini harakati yake inasonga mbele, tofauti na matatizo ya kiuchumi ya Magharibi ambayo ni mithili ya basi lililofunikwa na kusimama chini ya lindi kubwa la mlima wa theluji.
Ayatullah Khamenei amesema mabadiliko yaliyotokea huko kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati ni miongoni mwa hakika zinazopaswa kuzingatiwa. Ameongeza kuwa uwezo ulioimarika zaidi wa utawala wa Kiislamu hapa nchini pia ni miongoni mwa hakika muhimu sana.
Ameashiria utajiri mkubwa wa mafuta, gesi na madini hapa nchini na akaongeza kuwa nguvu kazi ya kibinadamu na jamii ya watu milioni 75 hususan tabaka la vijana wenye nishati na wasomi ni miongoni mwa hakika na masuala yenye umuhimu mkubwa yanayoleta maendeleo na ustawi.
Katika uwanja huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria sera za uzazi wa mpango na kusisitiza juu ya kutazamwa upya sera hizo. Amesema kuwa katika kipindi cha miaka ya mwanzoni mwa muongo wa 70 ilikuwa sahihi kutekelezwa mpango huo kwa kuzingatia maslahi, lakini ilikuwa makosa kuendelezwa utekelezaji wa mpango huo katika miaka ya baadaye.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa uchunguzi wa kisayansi na wa wataalamu unaonesha kuwa, iwapo sera hizo za uzazi wa mpango zitadumishwa tutakabiliana na tatizo la kuzeeka na hatimaye kupungua kwa idadi ya watu katika jamii; kwa msingi huo viongozi wa asasi husika wanalazimika kutamaza upya siasa na sera za uzazi wa mpango hapa nchini na vyombo vya habari pamoja na wanazuoni wa kidini wanapaswa kufanya jitihada za kuzungumzia suala hilo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa maadui wa Iran watapata kiburi zaidi iwapo viongozi hapa nchini watalegeza kamba kwa sababu yoyote ile. Amesema katika kipindi ambacho baadhi ya maafisa hapa nchini walikuwa wakijikomba kwa nchi za Magharibi na Marekani, alijitokeza mtu ambaye ni kielelezo cha shari na kujipa ruhusa ya kuitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni mhimili wa shari.
Vilevile ameashiria kipindi ambacho baadhi ya maafisa hapa nchini walilegeza kamba katika suala la nishati ya nyuklia na kusema: "Katika kipindi hicho Wamagharibi walikuja mbele zaidi kutokana na kulegeza kamba kwa baadhi ya maafisa hapa nchini hadi nikalazimika kuingilia kati".
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa wakati huo Wamagharibi walivimba kichwa kwa kadiri kwamba hata wakati maafisa wetu walipotosheka kuwa na mashinepewa (centrifuge) tatu tu Wamagharibi walipinga suala hilo, lakini hii leo kuna mashinepewa elfu 11 hapa nchini.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa iwapo kulegeza kamba huko kungeendelea, hii leo tusingekuwa na maendeleo haya katika medani ya nyuklia wala nishati na ubunifu wa kisayansi.
Amesema kuwa silaha ya vikwazo huwa butu pale kunapofanyika mapambano yenye mipango mizuri dhidi ya silaha hiyo. Ameongeza kuwa mashinikizo ya kiuchumi ya hivi sasa dhidi ya utawala wa Kiislamu hapa nchini ni mithili ya njia ya kupita na kipindi ambacho nchi hii itakivuka, kwani kudumu kwa mashinikizo hayo kwa kipindi kirefu hakutakuwa na maslahi kwa nchi za Magharibi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel pekee ndio wanaofaidika na mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na amesisitiza kuwa nchi nyingine zimeburutwa tu katika kadhia hii ama kwa mashinikizo au kwa kuona haya, na hali hii haitaendelea.
Amesema kuondolewa nchi 20 katika kundi la nchi zilizoanza kutekeleza vikwazo vya mafuta dhidi Iran na juhudi za baadi ya nchi za kutaka kukwepa vikwazo hivyo ni ishara kwamba hali hii haitaendelea kuwepo. Ameongeza kuwa mambo haya yote yanaonesha kwamba tunapaswa kudumisha njia ya mapambano kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, kuwa tayari kukabiliana na changamoto na kutumia tadbiri na mantiki.
Amesema kutumia vyema uwezo na suhula za nchi mbele ya changamoto mbalimbali kunadhihirisha hali halisi ya vita vya Badr na Khaibar na kuongeza kuwa, masuala ya nchi yanapaswa kuangaliwa kwa mtazamo huo na kwa kuoanisha baina ya malengo aali na uhakika wa mambo yanayohamasisha na kutia moyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa uchumi ni maudhui muhimu sana kwa nchi hii na harakati yake ya kupiga hatua za maendeleo. Amesisitiza kuwa lengo la mashinikizo ya kiuchumi ya adui katika kipindi cha sasa ni kutoa pigo kwa ustawi na hali bora ya taifa na kuwasababishia matatizo wananchi kwa shabaha ya kuwatenganisha na mfumo wa Kiislamu.
Ayatullah Ali Khamenei amesema tangu miaka kadhaa iliyopita ilidhihirika waziwazi kwamba mipango ya njama za adui imejikita katika uchumi wa Iran na kwa sababu hiyo kaulimbiu za miaka ya hivi karibuni kama vile "Marekebisho na Kigezo cha Matumizi", Hima na Kazi Ziada", "Jihadi ya Kiuchumi, Uzalishaji wa Kitaifa na Kuhami Kazi na Rasilimali za Kiirani" zilikuwa ni kwa shabaha ya kuanzisha cheni na mnyororo wa kiuchumi ili kuratibu harakati ya taifa katika masuala ya uchumi.
Amesisitiza juu ya udharura wa kukabiliana na mashinikizo ya kiuchumi kwa kutekeleza kifungu cha 44 cha katiba, kuwezesha sekta ya watu binafsi, kupunguza utegemezi wa taifa kwa mafuta, kutumia vyema wakati na suhula mbalimbali na kujiepusha na mabadiliko ya ghafla ya sheria.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa hii leo kuleta mlingano katika utumiaji ni harakati ya kijihadi na amezitaka taasisi zote za serikali na siziso za serikali na vilevile wananchi wote kutilia maanani sana suala la kujiepusha na israfu na kufanya jitihada za kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.
Ayatullah Khamenei ametumia fursa ya mkutano huo ambao umefanyika katika siku ya nne ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwakumbusha viongozi na wananchi wa Iran juu ya utukufu wa siku zenye baraka za mwezi huu.
Mwishoni mwa hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo suala la umoja na mshikamano na amewaambia viongozi kwamba wananchi wameshikamana na kwamba viongozi wanapaswa kulinda umoja na mshikamano huo kwa kujiepusha na hitilafu zisizo na faida.
Mwanzoni mwa mkutano huo Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu amesisitiza kuwa serikali inaheshimu thamani na misingi mikuu ya taifa kama tauhidi, uadilifu, uhuru, utukufu wa mwanadamu, ustawi na kutoa huduma kwa wananchi. Vilevile ametoa ripoti ya utendaji wa serikali yake kwenye nyanja mbalimbali katika kipindi cha miaka saba iliyopita. 1061752





captcha