Ameashiria mchango wa uchumi unaotegemea elimu na sayansi katika kustawisha utambulisho wa kitaifa, uwezo wa kisiasa na uhuru wa nchi na akasema Iran ya sasa imo katika kipindi cha kihistoria na nyeti na hapana shaka kwamba kutambua kwa njia sahihi majukumu yetu na kuyatekeleza kutalifikisha taifa la Iran katika mustakbali unaotoa bishara njema na kwenye malengo tunayoyakusudia.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa Iran inapiga hatua za maendeleo na hakuna mkwamo na tatizo lisiloweza kutatuliwa katika njia ya harakati inayosonga mbele ya taifa la Iran.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia baadhi ya mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kipropaganda katika njia ya harakati ya nchi hii kuelekea kwenye thamani na malengo yake aali na akasema kuwa, taifa la Iran limeazimia hasa kufikia malengo yake kwa hima na ari kubwa.
Amesema kuwa taifa la Iran liko katikati ya medani na matatizo na mashinikizo yanayofanywa hayawezi kulizuia kufika kwenye malengo yake.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, uwanja wa sasa ni medani inayotia hamasa na wakati huo huo inaambatana na mashaka. Ameongeza kuwa uwanja wa sasa wa Iran ya Kiislamu ni kama medani ya mashindano ya michezo ambayo mbali na kuambatana na uchovu na wasiwasi lakini kuhudhuria katika medani hiyo kunatia hamasa na wanamichezo wanajikita katika medani hiyo kwa shauku na ari kubwa.
Ayatullah Khamenei amesema moja ya njia za kuvuka salama kipindi muhimu cha sasa ni kutilia maanani uchumi wa kimuqama na kimapambano. Amesisitiza kuwa uchumi wa kimapambano si nara tupu bali ni hakika inayopaswa kutimizwa.
Amesema kuwa miongoni mwa vielelezo bora na vyenye taathira katika uchumi wa kimapambano ni makampuni yanayozalisha bidhaa kwa kutegemea sayansi na elimu ambayo yanaweweza kuimarisha zaidi uchumi wa kimapambano.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ustawi halisi wa kiuchumi ni ule unaopatikana kwa uzalishaji wa utajiri kupitia njia ya elimu na sayansi na kuongeza kuwa, iwapo makampuni yanayozalisha bidhaa kwa kutegemea sayansi na elimu yatapewa mazingatio makubwa na kuungwa mkono katika pande zote, hapana shaka kwamba uchumi wa nchi hii utachanua kutokana na kuzalishwa utajiri kupitia njia za elimu na sayansi.
Ayatullah Khamenei amesema, kutengeneza utajiri kupitia rasilimali na vyanzo vinavyoisha kama mafuta ni kujidanganya. Ameongeza kuwa uuzaji mafuta ghafi ni mtego tuliorithi kutoka kwenye miaka mingi ya kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu na inasikitisha kwamba nchi hii imenasa katika mtego huo; kwa msingi huo zinapaswa kufanyika juhudi za kuliokoa taifa kutoka kwenye hali hiyo.
Amesema kuwa ni jambo muhimu sana kuwa na imani na kufikia daraja ya kuvifunga kwa hiari yetu wenyewe visima vya mafuta na kuacha kuuza malighafi na madini. Amesisitiza kuwa suala hilo litawezekana kwa kutegemea elimu na kupitia makampuni yanayozalisha bidhaa kwa kutegemea sayansi na teknolojia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza hatua zilizochukuliwa na ofisi ya Rais inayoshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya kuunga mkono na kusaidia makampuni yanayozalisha bidhaa kwa kutegemea sayansi na elimu na akasema kuwa, kuna baadhi ya mapungufu na matatizo ambayo yanapaswa kuainishwa na kutatuliwa haraka.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria baadhi ya mambo yaliyotajwa na wahakiki na wavumbuzi na akasema, taasisi za serikali zinalazimika kutayarisha uwanja mzuri wa kuanzishwa makampuni yanayozalisha bidhaa kwa kutegemea elimu ya sayansi kwa kufuatilia mambo yote yanayobuniwa na kuwatambua wataalamu wenye vipawa vya kifikra na kuwaunga mkono.
Amezungumzia pia jinsi baadhi ya nchi za kigeni zinavyowekeza katika kutafuta na kuchukua vipawa na wasomi ndani wa Iran na akasisitiza juu ya udharura wa kuzuiwa suala hilo kwa kutumia njia za kimantiki, kutoa vivutio na kutoa misaada ya dharura. Amesema kuwa moja ya matatizo yaliyopo kuhusu makampuni yanayozalisha bidhaa kwa kutegemea elimu na sayansi ni kutotekelezwa sheria za kuyaunga mkono na kuyasaidia makampuni hayo. Amesema sheria hizo zinapaswa kutekelezwa haraka sana.
Ayatullah Khamenei pia amesisitiza juu ya udharura wa kuanzishwa benki ya kukusanya ripoti kwa ajili ya kutambua uwezo wa kielimu wa Iran, kuainisha udhaifu, kupanua uwanja wa shughuli za makampuni yanayozalisha bidhaa kwa kutegemea sayansi na teknolojia na kuimarisha sekta binafsi katika makampuni hayo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kujenga misingi ya uchumi kwa kutegemea uzalishaji wa utajiri kupitia makampuni yanayozalisha bidhaa kwa kutegemea elimu kutatayarisha uwanja wa kupata nguvu halisi ya kiuchumi, kuimarisha moyo wa kujiamini, kujitegemea, utambulisho wa kitaifa na hatimaye nguvu ya kisiasa. Amesema tunapaswa kuwahamasisha wasomi na wenye mitaji kuunda makampuni yanayozalisha bidhaa kwa kutegemea sayansi na teknolojia kwa kutayarisha mazingira mazuri.
Kabla ya hotuba ya kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wasomi, wahakiki na wataalamu 10 katika nyanja za sayansi na teknolojia na viongozi na wanaharakati wa makampuni yanayozalisha bidhaa kwa kutegemea sayansi na teknolojia walieleza mitazamo yao kuhusu kazi za makampuni hayo, sayansi na teknolojia na baadhi ya masuala yanayohusiana na kadhia hiyo. 1065516