Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo alasiri ya jana alipohutubia mamia ya Wairani waliokuwa mateka wa kivita katika jela za utawala wa zamani wa Saddam Hussein na kuongeza kuwa, kughusubiwa ardhi ya Kiislamu ya Palestina na kuwekwa humo Wazayuni ni msingi wa muundo wenye dosari wa Mashariki ya Kati na msingi wa matatizo ya miongo kadhaa ya mataifa ya eneo hilo. Ameongeza kuwa iwapo njama hiyo isingekuwepo basi pia kusingekuwepo vita, hitilafu na uingiliaji wa madola ya kibeberu na madhalimu unaoshuhudiwa sasa katika eneo hili. Ameelezea kusikitishwa na mtetemeko wa ardhi uliotokea Azarbaijan mashariki hapa nchini na kusema mwaka huu pia taifa la Kiislamu la Iran litatoa pigo kubwa kwa maadui wa Uislamu katika Siku ya Kimataifa ya Quds.
Ayatullah Khamenei amesema Wazayuni na watetezi wao wanafanya jitihada kubwa za kuyafanya mataifa mbalimbali yalisahau suala la Palestina lakini ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kusimama kidete mbele ya hadaa na njama hiyo.
Amezungumzia jinsi Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu alivyokuwa akilipa umuhimu maalumu suala la Palestina tokea mwanzoni mwa harakati za Kiislamu na kusema kuwa, Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ulizifanya jitihada za mabeberu za kutaka watu wasahau kadhia ya kughusubiwa Palestina zikabiliwe na kikwazo cha kihistoria.
Ameashiria njama zinazofanywa kwa ajili ya kuwasahaulisha watu kadhia ya Palestina na akasema: "Katika fremu hiyo baadhi ya watu wanazungumzia suala la Shia na Suni na hilali ya Kishia, ilhali imepita miaka 60 sasa huku taifa la Palestina likiendelea kushinikizwa tena mbele ya macho ya watu hawa lakini hawapazi sauti dhidi ya suala hilo."
Amehoji kwa kusema: Je, kutajwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imehuisha suala la Palestina kwamba ni hatari kwa ulimwengu wa Kiislamu na kunyamazia kimya maafa yanayofanywa na Wazayuni si usaliti?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kusimama kidete dhidi ya njama za kutaka kuwasahaulisha watu kadhia ya Palestina na Quds Tukufu na akaongeza kuwa: "Kadhia ya Quds kwa Iran si suala la kitaktiki na mbinu bali linatokana na itikadi halisi ya Kiislamu, na sisi tunakutambua kukombolewa nchi hiyo ya Kiislamu kutoka kwenye mikono na makucha na maghasibu wa Kizayuni na waungaji mkono wao wa Kimataifa kuwa ni wajibu wetu wa kidini, na mataifa na nchi nyingine za Kiislamu pia zinapaswa kuitazama kadhia ya Palestina kwa jicho hilo."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kama ambavyo nyota ya asubuhi ya matumaini ilivyong'ara wakati wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, katika hamasa ya kujilinda kutakatifu na wakati wa kurejea nyumbani mateka wa kivita kutoka Iraq, mara hii pia alfajiri ya matumaini katika suala la Palestina itachomoza na hatimaye ardhi hiyo ya Kiislamu itarejea kwa taifa la Palestina na mwanaharamu na dola bandia la Kizayuni litafutwa katika jiografia.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Kiongozi wa Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mtetemeko wa ardhi ulioyakumba baadhi ya maeneo ya mkoa wa Azarbaijan Mashariki na kufariki dunia baadhi ya wananchi kuwa ni tukio chungu, la kusikitisha na kuumiza taifa na amewataka viongozi na wananchi kutoa misaada kwa wananchi wenzao na kupunguza mashaka na matatizo yao. 1080052