IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Mataifa mbalimbali yamechoshwa na mfumo wenye dosari nyingi wa kimataifa

23:54 - August 30, 2012
Habari ID: 2401934
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amehutubia mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi 120 wanachama katika Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) mjini Tehran.
Katika hotuba hiyo muhimu mbele ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa nchi za mabara matano ya dunia, Ayatullah Ali Khameni ameashiria hali nyeti ya sasa na harakati ya dunia ya kuvuka kipindi muhimu sana cha kihistoria na ishara za kuibuka mfumo mpya wenye pande kadhaa mkabala wa mfumo wa kibeberu wenye mwelelekeo wa kambi moja na akaeleza fursa zinazotoa bishara njema kwa nchi huru na thamani kuu za nchi wanachama katika jumuiya ya NAM na vilevile ishara za kufikia kikomo subira ya walimwengu hususan mataifa ya Magharibi kuhusu mfumo wenye dosari, uliochakaa, usiokuwa wa kiadilifu na usio wa kidemokrasia wa muundo wa sasa wa kimataifa.
Amesisitiza kuwa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) inapaswa kuwa na nafasi mpya katika kuunda mfumo mpya wa kimataifa na wanachama wa jumuiya hiyo wanaweza kuwa na mchango na nafasi ya kihistoria itakayokumbukwa milele kwa ajili ya kuokoa ulimwengu kutoka katika hali ya ukosefu wa amani, vita na ubeberu.
Ayatullah Khamenei ameashiria hotuba iliyotolewa na waasisi wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote ambaao walisema msingi wa kuanzishwa jumuiya hiyo si umoja wa kijiografia, kaumu au dini bali ni “umoja katika mahitaji” na akasema: “haja hiyo bado ipo hivi sasa licha ya maendeleo yaliyopo na kupanuka zaidi nyezo za ubeberu.”
Amekumbusha mafundisho ya dini ya Uislamu ambayo inatambua maumbile ya wanadamu wote kuwa ni sawa licha ya tofauti zao za kikaumu, kilugha na kiutamaduni na akasema kuwa, ukweli huo unaong’ara una uwezo mkubwa wa kuwa msingi na nguzo ya kuunda jamii huru, zenye fahari, maendeleo na uadilifu na unaweza kuwa msingi wa ushirikiano wa kidugu kati ya mataifa mbalimbali.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa unaojengeka juu ya msingi huo wa mawasiliano baina ya nchi kwa mujibu wa maslahi sahihi na ya pande zote utakuwa na maslahi ya kibinadamu na kuongeza kuwa, mfumo huo aali unakabiliana na mfumo wa kibeberu ambao katika karne za hivi karibuni madola ya kibeberu ya Kimagharibi na hii leo dola la kidhalimu la Marekani linaohubiri na kuuongoza.
Ayatullah Ali Khamenei amesema malengo makuu ya Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote yangali hai licha ya kupita miongo sita sasa tangu jumuiya hiyo ianzishwe na akasema, kutimizwa kwa malengo hayo ni jambo linalotia matumaini na lenye matunda licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi. Amesema kuwa dunia iliopata ibra na tajiriba ya kihistoriaa ya kushindwa siasa za kipindi cha vita baridi na siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za baada ya kipindi hicho inaelekea katika mfumo mpya wa kimataifa unaozishirikisha pande zote na kutoa haki sawa kwa mataifa mbalimbali; na katika hali kama hii kuna udharura wa kuwepo mshikamano na umoja kati ya nchi wanachama wa NAM.
Amesema kulindwa mshikamano na mfungamano kati ya wanachama wa jumuiya ya NAM katika mipaka ya thamani na malengo ya jumuiya hiyo ni miongoni mwa matunda makubwa. Ameongeza kuwa kwa bahati nzuri mustakbali wa matukio ya kimataifa unatoa bishara njema ya kijitokeza mfumo wa kambi kadhaa ambamo ndani yake kambi za kijadi za nguvu zitapoteza nafasi zao kwa majmui ya nchi, tamaduni na staarabu mbalimbali zenye mielekeo mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, na mabadiliko hayo yanazipa fursa nchi wanachama wa NAM ili ziweze kuwa na nafasi kubwa na yenye taathira katika nyanja za kimataifa na kutayarisha uwanja mzuri wa kuwepo uongozi wa kiadilifu na unaoshirikisha pande zote kote duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, hali ya sasa ni fursa isiyokariri kwa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote. Amewaambia viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kwamba kauli yetu ni kwamba usukani wa kuendesha masuala ya dunia haupaswi kushikwa na udikteta wa nchi kadhaa za Magharibi. Tunapaswa kuwa na uwezo wa kuzishirikisha pande zote kwa njia ya kidemokrasia katika uendeshaji wa masuala ya kimataifa na kudhamini suala hilo.
Ayatullah Khamenei ameendelea kubainisha matatizo na muundo wenye dosari na usiofaa wa mfumo wa sasa wa kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amesema kuwa Baraza la Usalama lina muundo usiokuwa wa kimantiki, usio wa kiadilifu na usio wa kidemokrasia. Mfumo wa baraza hilo ni udikteta wa wazi na hali iliyochakaa na kupitwa na wakati, amesisitiza Kiongozi Muadhamu.
Amesema kuwa ni kwa kutumia muundo huo usiokuwa sahihi ndiyo maana Marekani na washirika wake wameweza kuitwisha dunia dhulma zao kwa kutumia vazi la maana nzuri na aali. Amesema kuwa, wanasema “haki za binadamu” wakikusudia maslahi ya nchi za Magharibi; wanazungumzia “demokrasia” na kuweka mahala pake uvamizi wa kijeshi katika nchi mbalimbali na wanazungumzia suala la kupambana na ugaidi huku wakiwashambulia kwa makombora na silaha nyinginezo watu wasiokuwa na ulinzi katika vijiji na miji mbalimbali.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hatua ya Marekani na madola mengine ya kibeberu ya kuwagawa watu wa dunia kati ya watu wa daraja la kwanza, la pili na la tatu na akasema, roho za wanadamu katika Asia, Afrika na America ya Latini ni rahisi na zile za watu wa Marekani na Ulaya magharibi ni ghali. Usalama wa Marekani na Ulaya ni muhimu na usalama wa wanadamu wa maeneo mengine hauna umuhimu. Mateso na mauaji ya kigaidi yanapofanywa na Marekani, Wazayuni na washirika wao huhalalishwa na kufumbiwa macho kwa kadiri kwamba vitendo viovu kabisa vinavyofanywa dhidi ya wafungwa wasiokuwa na ulinzi wala wakili wanaoshikiliwa bila ya kufikishwa mahakamani katika jela za siri za Marekani, haviamshi hisia zao.
Ayatullah Khamenei ameashiria maana isiyokuwa sahihi inayotolewa kwa baadhi ya mambo kama wasifu unaotolewa katika mfumo wa kibeberu wa mambo mazuri na yaliyomabaya na kusema, mabeberu hao wanayaita maslahi yao kwa jina la sheria za kimataifa na matamshi yao yasiyokuwa ya kimantiki wanayapachika jina la “jamii ya kimataifa” na kuyatwisha mataifa mengine. Wanatumia kanali yao kubwa ya vyombo vya habari wanayoihodhi kwa ajili ya kubadili uongo na kuuita kuwa ni ukweli, batili wanaidhihirisha kuwa ni haki, dhulma zao wanaziita kuwa ni uadilifu; kila neno la haki linalofichua uongo wao wanaliita kuwa ni uongo na kila harakati ya kudai haki wanaipachika jina la uasi.
Amesema hali hii yenye nakisi na dosari nyingi haiwezi kuendelea kuwapo na mataifa yote yamechoshwa na muundo huu wenye makosa wa kimataifa. Amesema kuwa Harakati ya 99 iliyoanzishwa na wananchi wa Marekani dhidi ya vituo vikuu vya utajiri na nguvu nchini humo na malalamiko na upinzani wa wananchi wa nchi za Ulaya magharibi dhidi ya siasa na sera za kiuchumi za serikali katika nchi zao ni ishara ya kufikia kikomo subira na ustahamilivu wa mataifa mbalimbali mbele ya hali hiyo. Amesisitiza kuwa kwa msingi huo kuna udharura wa kutafutwa tiba ya hali hiyo isiyokuwa ya kimantiki.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mshikamano madhubuti, wa kimantiki na wa pande zote wa nchi wanachama wa NAM katika kutafuta njia ya kutibu matatizo hayo una taathira kubwa. Ameashiria suala la ukosefu wa usalama na amani ya kweli kuwa ni miongoni mwa masuala tata ya dunia ya leo. Amesema kuwa suala la kutokomezwa silaha za maangamizi ya umati na zinazosababisha maafa ni dharura na takwa la watu wote na nchi zinazojilimbikizia silaha za kuwaangamiza wanadamu katika maghala yao ya silaha hazina haki ya kujitangaza kuwa ni vinara wa usalama na amani duniani.
Ayatullah Khamenei amesema nchi zinazomiliki silaha za nyuklia hazina azma ya kweli ya kuondoa zana hizo za maangamizi katika sera zao za kijeshi. Ameongeza kuwa fikra yoyote inayodhani kuwa silaha za nyuklia ni wenzo wa kuondoa vitisho na kigezo muhimu cha nafasi ya kisiasa na kimataifa cha nchi inayomiliki silaha hizo haiwezi kukubalika. Amesema kuwa silaha za nyuklia hazidhamini usalama na amani na wala si alama ya uwezo wa kisiasa bali ni tishio kwa viwili hivyo; na matukio ya muongo wa 90 wa karne ya 20 yameonesha kwamba, kumiliki silaha hizo za nyuklia hakuwezi kulinda utawala kama Urusi ya zamani.
Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakutambua kutumia silaha za nyuklia, za kemikali na kadhalika kuwa ni madhambi makubwa yasiyosameheka na kwa msingi huo ilitoa kaulimbiu ya “Mashariki ya Kati isiyokuwa na silaha za nyuklia” na inashikamana nayo barabara.
Hata hivyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutoa kaulimbiu hiyo haina maana ya kufumbia macho haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya kiraia na kuzalisha fueli ya nyuklia. Amesema, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, utumiaji wa nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani ni haki ya nchi zote na watu wote wanapaswa kuwa na uwezo wa kutumia nishati hiyo katika matumizi mbalimbali muhimu ya nchi na mataifa yao na kutotegemea nchi nyingine katika kutumia haki hiyo.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria harakati inayotia shaka ya nchi kadhaa za Magharibi zinazomiliki silaha za nyuklia na zilizotumia silaha hizo kwa ajili ya kuhodhi uzalishaji na uuzaji wa fueli ya nyuklia na akasema: “Mchezo mchungu wa kuchekesha wa zama hizi ni kuwa, serikali ya Marekani ambayo ndiyo inayomiliki silaha nyingi zaidi za maangamizi na za nyuklia na silaha nyingine za mauaji ya halaiki mbayo pia ndio nchi pekee iliyotumia silaha hizo dhidi ya binadamu, hii leo zinataka kubeba bendera ya kupinga uenezaji wa silaha za nyuklia, ilhali Marekani na washirika wake wa Kimagharibi hawawezi kustahamili kuona nchi zinazojitegemea zikitumia nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani na zinapiga vita hata suala la uzalishaji wa fueli ya nyuklia kwa ajili ya kutengeneza madawa (Radiopharmaceutical) na matumizi mengine ya kiraia.”
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria visingizio vya uongo vya Marekani na nchi kadhaa za Magharibi kuhusu wasiwasi wao juu ya eti uzalishaji wa silaha za nyuklia nchini Iran na akasema: “Ninasisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia na kamwe haitafumbia macho haki ya taifa lake ya kutumia nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia. Kaulimbiu yetu ni ‘Nishati ya Nyuklia kwa Ajili ya Wote, na Silaha za Nyuklia si kwa Yeyote’. Tunashikamana barabara na mambo hayo mawili.”
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kuvunja mzingiro wa nchi kadhaa za Magharibi katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia sambamba na kuheshimu makubaliano ya kuzuia uzalishaji na uenezaji wa silaha za nyuklia (NPT) kuna faida kwa nchi zote zinazojitegemea zikiwemo nchi wanachama katika Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote. Ameongeza kuwa tajiriba na uzoefu wa miongo mitatu ya kusimama kidete mbele ya madola ya kibeberu na mashinikizo ya pande zote ya Marekani na waitifaki wake umeifikisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kiwango cha kuamini kwamba, mapambano ya taifa lolote lenye umoja na azma kubwa yanaweza kushinda uhasama na uadui wote na kufungua njia yenye fahari ya kufikia malengo makubwa.
Amesema kuwa maendeleo ya pande zote ya Iran katika kipindi cha miongo miwili ya hivi karibuni tena chini ya vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi na hujuma za kipropaganda ni kielelezo kikubwa cha matokeo ya kusimama imara kwa taifa la Iran. Ameongeza kuwa, vikwazo ambavyo waropokaji wanaviita kuwa ni vya kudumaza, si tu kwamba havikuidumaza Iran wala havitaweza kufanya hivyo, bali pia vimezidisha kasi ya hatua za Iran, vimeimarisha hima ya taifa na kutia nguvu imani ya wananchi wa Iran kwamba uchambuzi wao ulikuwa sahihi na vikwazo hivyo vinaimarisha zaidi ari na azma ya taifa hilo. Amesisitiza kuwa taifa la Iran limekuwa likishuhudia kwa macho msaada wa Mwenyezi Mungu katika changamoto hizo.
Suala jingine lililozungumziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hadhara ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa nchi wanachama wa NAM ni kadhia muhimu sana lakini inayoumiza jamii ya mwanadamu yaani kadhia ya Palestina.
Ayatullah Khamenei amezungumzia njama hatari za nchi za Magharibi zikiongozwa na Uingereza katika kughusubu nchi inayojitegemea na yenye utambulisho wa wazi wa kihistoria ya Palestina na jinai za viongozi wa kisiasa na kijeshi wa utawala ghasibu wa Kizayuni katika kipindi cha zaidi ya miaka 65 iliyopita. Amesema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umeanzisha vita vya maafa makubwa, kuwaua wananchi, kukalia kwa mabavu ardhi za Kiarabu, kupanga ugaidi wa kiserikali katika Mashariki ya Kati na duniani na umekuwa ukifanya mauaji ya kigaidi, vita na shari nyinginezo kwa miaka mingi sasa, unalituhumu taifa la Palestina linalopigania haki zake kuwa ni magaidi huku kanali ya vyombo vya habari vya Kizayuni na vyombo vingine vya habari vya Magharibi na vibaraka vikikariri uongo huo mkubwa. Vilevile viongozi wa kisiasa wanaodai kushika bendera ya kutetea haki za binadamu, wanaunga mkono utawala huo ghasibu kwa kufumbia macho jinai zake za kutisha na kudhihiri kama wakili wa upande wa utetezi.
Amesisitiza kuwa njia zote zilizopendekezwa na kutekelezwa na nchi za Magharibi na washirika wao kwa ajili ya kutatua kadhia ya Palestina ni makosa matupu na haziwezi kufanikiwa. Ayatullah Khamenei ameashiria tena njia ya kiadilifu na ya kidemokrasia ya utatuzi wa kadhia ya Palestina iliyopendekezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema, kwa mujibu wa njia hiyo, Wapalestina wote sawa wale wanaoishi katika ardhi ya nchi hiyo au wale waliofukuzwa nchini kwao na kukimbilia nchi nyingine lakini wamelinda utambulisho wao wa Kiplestina, Waislamu, Wakristo na Wayahudi, wote wanapaswa kushiriki katika kura ya maoni itakayosimamiwa kwa uangalizi mkubwa na kuchagua muundo wa mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo; hapa ndipo amani itakapopatikana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake katika hadhara ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa jumuiya ya NAM kwa kutoa nasaha kwa wanasiasa wa Marekani ambao daima wamekuwa wakiutetea na kuulinda utawala ghasibu wa Israel. Amewaambia utawala huo umewasababishia matatizo mengi, kuwaingiza katika gharama kubwa na kuchafua sura yenu mbele ya mataifa ya Mashariki ya Kati huku ukiwatambulisha kama washirika katika jinai za Wazayuni maghasibu. Hebu chunguzeni pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu suala la kuitisha kura ya maoni na jiokoeni kutoka kwenye mkwamo usiokwamuka wa sasa kwa kuchukua uamuzi wa kishujaa. Hapana shaka kwamba watu wa Mashariki ya Kati na wanafikra huru kote duniani watakaribisha hatua hiyo.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amezungumzia umuhimu wa mkutano wa viongozi wa nchi wanachama katika Harakazi ya Nchi Zisizofungamana Siasa za Upande Wowote wa Tehran katika kipindi cha sasa na akasema, kwa kushirikiana na kutumia vyema uwezo wao mkubwa, wanachama wa jumuiya hiyo wanaweza kuwa na mchango wa kihistoria utakaokumbukwa milele katika kuokoa dunia kutokana na ukosefu wa amani, vita na ubeberu.
Amesema sharti la kufikiwa lengo hilo kubwa ni kuwepo ushirikiano wa pande zote kati ya nchi wanachama na kupeana uzoefu na tajiriba. Amesisitiza kuwa: “Tunapaswa kuimarisha azma zetu, kuendelea kuwa waamininifu kwa malengo yetu na tusiogope hasira za madola ya kidhalimu wala kughurika na tabasamu zao. Irada na matakwa ya Mwenyezi Mungu na kanuni za maumbile zitatuunga mkono, na tutazame kwa jicho la ibra kushindwa kwa tajiriba ya kambi ya ukomunisti miongo miwili iliyopita na kufeli kwa siasa zinaoitwa za demokrasia ya kiliberali za Magharibi katika kipindi cha sasa. Tunapaswa kuyatambua matukio ya kuporomoka madikteta waliokuwa tegemezi kwa Marekani na washirika wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko kaskazini mwa Afrika na vilevile mwamko wa Kiislamu katika nchi za eneo hilo kama fursa kubwa.”
Mwishoni mwa hotuba yake mbele ya hadhara ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa nchi 120 wanachama katika Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo udharura wa kuundwa sekretarieti madhubuti ya harakati hiyo na akasema, tunaweza kutafakari kuhusu suala la kuzidisha nafasi ya kisiasa ya jumuiya ya NAM katika uendeshaji wa masuala ya kimataifa; tunaweza kutayarisha hati ya kihistoria kwa ajili ya kufanya mabadiliko katika uendeshaji huo na kutayarisha nyenzo zake za utekelezaji na tunaweza kuanzisha harakati ya kuelekea kwenye ushirikiano mkubwa wa kiuchumi na kubuni kigezo cha mahusiano ya kiutamaduni baina yetu. 1088072

captcha