IQNA

Katika mazungumzo yake na Makamu wa Rais wa Indonesia:

Kiongozi Muadhamu atahadharisha juu ya njama hatari za kuzusha hitilafu za kikaumu na kidini katika nchi za Kiislamu

15:29 - August 31, 2012
Habari ID: 2402121
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameonana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Indonesia na ujumbe unaoandamana naye hapa mjini Tehran.
Katika mazungumzo hayo Ayatullah Khamenei ameashiria thamani asili za Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) na uwezo mkubwa na suhula nyingi za nchi wanachama na akasema kuwa, lengo kuu la kuanzishwa harakati ya NAM halikuwa kuanzisha jumuiya ya kiheshima tu bali waasisi wake walikusudia kuanzisha jumuiya yenye taathira na hai na malengo hayo yanapaswa kuhuishwa.
Amesema kuwa nchi wanachama wa jumuiya ya NAM ikiwemo Indonesia ambayo ni miongoni mwa waasisi wake, zinapaswa kushirikiana na kutumia uwezo wao na kuwa na taathira na mchango mkubwa katika masuala muhimu ya kieneo na kimataifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa suala la kutumia uzoefu na maendeleo ya nchi wanachama wa jumuiya ya NAM ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika jumuiya hiyo. Amesema kuwa maendeleo ya nchi zinazojitawala za Kiislamu yana maadui na tunapaswa kuwa macho mbele ya njama zao.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa moja ya njama hatari za maadui ni kuzusha hitilafu na mapigano ya kimadhehebu hususan kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni. Ameongeza kuwa vitendo hivyo vinafanyika kwa uungaji mkono wa baadhi ya nchi kubwa za kibeberu na kwa kutumia vibaraka wao na mifano ya suala hilo inaonekana katika nchi za Pakistan na Afghanistan.
Amesema kuwa makundi kama al Qaida na Taliban yalianzishwa kwa himaya na msaada wa washirika wa Marekani na sasa Washington inazishambulia kwa mabomu nchi za Pakistan na Afghanistan kwa kisingizio cha kukabiliana na makundi hayo, japokuwa lengo halisi ni kuzidhibiti nchi hizo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametahadharisha kuhusu njama hatari za kuzusha vita vya kikaumu na kimadhehebu katika nchi za Indonesia, Misri na Libya na ametilia mkazo udharura wa kuwepo ushirikiano mkubwa zaidi kati ya nchi za Kiislamu.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa IndonesiaPrf. Boediono ameeleza kufurahishwa kwake na jinsi mkutano wa NAM ulivyofanyika kwa mafanikio makubwa mjini Tehran na kusisitiza kuwa, uwanja wa ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na Indonesia ni mkubwa sana. Boediono amesema, katika mazungumzo yaliyofanyika kati ya Iran na Indonesia imeamuliwa kwamba sekta ya binafsi na ya wafanyabiashara wa nchi hizi mbili iimarishwe zaidi na kufanyike uchunguzi zaidi kuhusu njia za kupanua ushirikiano wa kiuchumi wa pande mbili.
Vilevile Makamu wa Rais wa Indonesia amesisitiza juu ya umuhimu wa uwezo wa nchi wanachama katika jumuiya ya NAM kwa ajili ya kuwa na taathira kubwa zaidi katika masuala ya kimataifa.
Kuhusu masuala ya kaumu na madhehebu tofauti ya Indonesia Prf. Boediono amesema serikali ya Jakarta daima imekuwa ikitafuta njia za kuanzisha njia bora za kuishi kwa amani watu wa kaumu na madhehebu yote nchini humo.
Makamu wa Rais wa Indonesia pia ameashiria utaalamu wake katika masuala ya uchumi na akamwambia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwamba: “Nimesoma mitazamo yako kuhusu uchumi wa kimapambano na nimevutiwa mno na mitazamo hiyo mipya.” 1088458
captcha