IQNA

Amiri Jeshi Mkuu:

Jamhuri ya Kiislamu haitakubali matakwa ya dola lolote kubwa

22:55 - September 19, 2012
Habari ID: 2415562
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo amehutumia mjumuiko wa maelfu ya askari wa Jeshi la Ulinzi katika Divisheni ya Kaskazini na familia zao ambako ameashiria kukita mizizi, kuimarika umbo la mti wenye baraka wa Mapinduzi ya Kiislamu, kunawiri na matunda yanayoshuhudiwa katika matawi yake na kusema kuwa, kuendelea kwa harakati hiyo kunahitajia kazi, bidii kubwa, azma na hima ya wananchi wote.
Amezungumzia awamu mbalimbali za mapambano ya taifa la Iran na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: "Iran azizi na taifa letu kubwa linapiga hatua katika njia ya fahari na yenye mwisho mwema tangu miaka 33 iliyopita kwa baraka za mwamko wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema njia yenye mashaka lakini iliyojaa nishati na harakati ya miongo mitatu iliyopita ni tarjumi na maelezo ya aya za Qur'ani Tukufu zinazosema kuwa, hakika pamoja na dhiki kuna faraja. Ameongeza kuwa, mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa katika baadhi ya nchi za eneo hili ni tukio lenye baraka lakini Mapinduzi ya Kiislamu ya taifa la Iran yana sifa za kipekee katika upande wa upana, kukita mizizi na kupigania thamani na malengo yake.
Amesema kuwa miongoni mwa sifa hizo za kipekee ni umoja wa wananchi wote katika kaulimbiu na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu, nishati na vuguvugu kubwa la kimapinduzi lililoenea kote nchini na kuhudhuria kwa wananchi wenye imani thabiti na walio tayari kwa ajili ya kusabilia maisha yao katika medani ya mapambano. Amesisitiza kuwa mahala popote mataifa yanapojitokeza katika medani ya mapambano kwa imani na moyo wa kujitolea, hakuna dola lolote linaloweza kukabiliana nao, kwa sababu kwa mujibu wa suna na kanuni ya Mwenyezi mMungu, damu hushinda panga.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuhudhuria kwa wingi wananchi katika medani mbalimbali ndio nguzo imara ya viongozi wa utawala wa Kiislamu katika kusimama kidete mbele ya matakwa haramu ya maadui. Ameongeza kuwa, katika siku hizi baadhi ya nchi zilizofanya mapinduzi zimelazimika kulegeza misimamo yao katika baadhi ya mambo kutokana na mashinikizo ya Marekani, ilhali viongozi wa utawala wa Kiislamu nchini Iran wamesimama ngangari mbele ya mashinikizo kama hayo katika kipindi chote cha miaka 33 iliyopita.
Amesisitiza kuwa, kwa baraka za mahudhurio makubwa ya wananchi katika medani mbalimbali za mapambano, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikubali maneno na matakwa ya dola lolote kubwa na inachukua maamuzi kwa mujibu wa maslahi ya nchi na taifa japokuwa madola yote ya kibeberu duniani yatakasirishwa na maamuzi hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kueleweka zaidi pande mbalimbali za thamani za Mapinduzi ya Kiislamu ni maendeleo makubwa. Amesema, kadiri wakati unavyopita ndivyo maana ya thamani kama "Jamhuri ya Kiislamu, demokrasia ya Kiislamu, uhuru na kujitawala" vinavyoeleweka vyema zaidi kwa wananchi, wasomi na wanasiasa na kudhihirika wazi kanuni za njia ya kufikiwa malengo na thamani hizo; hii ni pamoja na kuwa katika miaka hiyo yote harakati imedumishwa kwa mujibu wa thamani hizo, suala ambalo ni maendeleo makubwa.
Ayatullah Khamenei amesema, kukita mizizi na kuimarika jengo la Jamhuri ya Kiislamu ni dalili nyingine ya maendeleo yanayoonekana ya utawala wa Kiislamu hapa nchini. Amesema kuwa, ikilinganishwa na miaka ya awali baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, matumaini ya maadui ya kuangusha utawala uliochaguliwa na wananchi wa Iran yamedhoofika mno na katika sehemu nyingine yamebadilika na kuwa hali ya kukata moyo, na suala hili linadhihirisha uimara wa Jamhuri ya Kiislamu.
Amesema kuwa maendeleo ya kustaajabisha ya Iran katika nyanya mbalimbali za sayansi na teknolojia ni miongoni mwa vielelezo vya kunawiri kwa matawi yenye baraka tele ya utawala wa Kiislamu hapa nchini. Ameongeza kuwa maendeleo yaliyopatikana hapa nchini katika nyanja kama za nyuklia na seli shina ni makubwa mno kiasi kwamba, yamewaacha bumbuazi hata baadhi ya wasomi wakubwa na waliotoa huduma kubwa wa kizazi kilichopita hapa.
Amesisitiza kuwa hivi sasa pia wasomi vijana katika nyanja mbalimbali za sayansi, uvumbuzi na utengenezaji wa masuala mengi ya kielimu wanapiga hatua kubwa za maendeleo ambayo yanawashangaza watu wengi.
Baada ya kubainisha maendeleo makubwa ya nchi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya kudumishwa harakati ya taifa zima ya maendeleo na kusema kuwa, wananchi wote wanapaswa kuwa na imani kwamba, kazi na bidii havitambui suala la kustaafu wala havina mwisho.
Amesema kuwa moja ya mbinu chafu zinazotumiwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na Wazayuni kwa ajili ya kusimaisha njia ya maendeleo ya taifa la Iran ni kudhihirisha sura isiyokuwa sahihi na yenye giza kuhusu hali ya Iran. Ameongeza kuwa sambamba na kupuuza mbinu hizo chafu, taifa linaelewa kwamba, ili kupata mustakbali wenye nuru hapa nchini halipasi kughafilika au kulala.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja familia za askari wa jeshi la Iran kuwa ni washirika wao katika kazi za jihadi na fahari zao. Amesema kuwa jeshi la Iran lina nafasi nyeti katika kujenga jengo la mfumo wa Kiislamu na kazi hiyo muhimu haiwezi kutekelezwa bila ya familia zao.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mfumo mpya wa Kiislamu ni utangulizi wa ustaarabu mpya wa Kiislamu. Vilevile amepongeza subira za familia za mashahidi .
Mwanzoni mwa mkutano huo Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Admeri Sayyari amesema kuwa mkusanyiko wa familia za askari wa jeshi mbele ya Amiri Jeshi Mkuu ni fursa ya kudhihirisha udugu na mshikamano na kuongea kuwa, sehemu kubwa ya mafanikio ya jeshi katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu hadi sasa yametokana na mshikamano na msaada wa familia zao. 1101831
captcha