IQNA

Imam Khamenei: Umoja wa Kiislamu udhihirishwe katika Hija

5:09 - September 25, 2012
Habari ID: 2419043
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa umoja wa umma wa Kiislamu unaoonekana kupitia kwa Mtume Mwisho Muhammad SAW na chuki na hasira za Waislamu wote dhidi ya kambi ya ubeberu vinapaswa kudhihirishwa katika ibada ya Hija ambayo ni kituo cha mkusanyiko wa Waislamu kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Ayatullah Khamenei ambaye mapema leo amehutubia hadhara ya wasimamizi wa msafara wa hija wa Iran ameashiria vitendo vya kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW katika nchi za Magharibi na kudhihiri heshima na adhama ya mtukufu huyo mbele ya wapenzi na hata maadui zake na akasema kuwa, ibada ya hija ya mwaka huu ina nafasi makhsusi na ni tofauti na ya miaka ya huko nyuma.

Ayatullahil Udhma Ali Khamenei amesema kuwa hatua ya mabeberu na vibaraka wao ya kumvunjia heshima Mtume wa rehma, izza na utukufu vinadhihirisha uhasama, chuki na kinyongo cha kambi ya ubeberu dhidi ya Mtume wa Uislamu. Ameongeza kuwa msimamo uliochukuliwa na wanasiasa wa nchi za Magharibi kuhusu dharau hiyo kubwa hauna tofauti na msimamo wa kiadui.

Amesema kuwa suala la kuvunjiwa heshima Mtume Mtukufu SAW na msimamo wa viongozi wa kambi ya ubeberu vimedhihirisha sura yao halisi, kuweka wazi mpambano baina ya haki na batili na kuonesha kwamba, sababu kuu ya uadui wa mabeberu ni Uislamu wenyewe na Mtume wa mwisho Muhammad SAW.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Mtume Muhammad SAW ndiye anayewakutanisha pamoja Waislamu wote wa madhehebu na makundi mbalimbali na kuongeza kuwa, katika suala hili hakuna mjadala kuhusu Suni, Shia, Waislamu wenye misimamo ya wastani au wenye misimamo mikali na wote wamejitokeza katika medani kwa nguvu zao zote kwa sababu Mtume wa Uislamu ndiye nguzo na msingi wa itikadi za Kiislamu.

Amesema kuwa kudhihiri thamani za umoja wa Kiislamu kandokando ya shakhsia kubwa ya Nabii Muhammad SAW na kudhihirisha chuki na hasira dhidi ya maadui wake katika ibada ya Hija ni jambo muhimu na la dharura. Ameongeza kuwa kujibari na kujitenga na Waislamu kuna maana Waislamu wote kuhisi kwamba wanakabiliana na adui mmoja na kujitenga naye kikamilifu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameutaka umma wa Kiislamu kuwa macho mbele ya njama hatari zinazofanywa kwa ajili ya kuzusha hitilafu kati ya Waislamu na akasema kuwa maadui wa dini na mabeberu wanapaswa kuelewa kuwa umma wa Waislamu utakabiliana nao licha ya kuwa na madhehebu tofauti na baadhi ya hitilafu za kinadharia na kiitikadi.
1105960
captcha