IQNA

Ayatullah Khamenei:

Taifa la Iran halitasalimu amri mbele ya madola ya kibeberu

17:23 - October 16, 2012
Habari ID: 2432885
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa nchi za kibeberu za Magharibi hazina ubavu wa kulilazimisha taifa la wanamapambano na angavu la Iran kusalimu amri mbele ya matakwa yao.
Ayatullahil Udhma Ali Khamenei ambaye alikuwa akihutubia wawakilishi wa matabaka mbalimbali ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Khorasani Kaskazini huko kaskazini mashariki mwa Iran ameashiria propaganda za vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na Wazayuni dhidi ya Iran na kusema kuwa, wamekuwa wakieneza propaganda za urongo kuwa lengo la kuzidisha mashinikizo yao dhidi ya Iran ni kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu irejee katika meza ya mazungumzo ilhali Iran haijawahi kuondoka katika meza ya mazungumzo ya masuala mbalimbali likiwemo suala la nyuklia ili ilazimike kurejea kwenye meza hiyo.
Ameongeza kuwa lengo la wanaofanya propaganda hizo za kisiasa ni kulilazimisha taifa la Iran lisalimu amri katika meza ya mazungumzo lakini taifa la wanamapambano, angavu na linaloona mbali la Iran kamwe halitasalimu amri mbele ya matakwa yasiyo ya kimantiki ya nchi za Magharibi.
Amekumbusha jinsi Wazayuni wanavyodhibiti aghlabu ya vyombo vya habari katika nchi za Magharibi na huko Ulaya na kuongeza kuwa, vyombo hivyo vya habari vinabuni habari, kuzielekea upande mmoja na kuwatwisha watu kiasi kwamba hata wanasiasa wa Kimagharibi wanaathirika na propaganda hizo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja maendeleo makubwa yaliyopatikana nchini Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu miaka 33 iliyopita na chini ya kivuli cha mashinikizo, vitisho na njama mbalimbali za maadui kuwa ni dalili ya kuwepo nguvu halisi na chanya ya ndani hapa nchini. Ameongeza kuwa uhakika huu ni kielelezo cha nguvu na uwezo mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu katika kukabiliana na maadui.
Amesema moja ya nyanja za mapambano ya Iran na maadui ni medani ya mazungumzo ya kimataifa ambako viongozi wa Iran ya leo wamekuwa wakitoa matamshi yanayoakisi kukomaa, kamili na sahihi katika meza za mazungumzo mbalimbali na kwenye minasaba tofauti.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, umadhubuti wa ndani unapeleka kuimarika na kupata nguvu ya kidhahiri na kuongeza kuwa, kwa sababu ya uimara na nguvu hiyo ujumbe mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na misimamo yake ya kukabiliana na mabeberu, umeathiri harakati ya mataifa mengine; suala hilo limewatia kiwewe mabeberu na mwenendo huo utaendela kwa baraka zake Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya haja kubwa ya Iran kwa kazi na bidii zaidi na kusema kuwa, wakati wowote adui anapoona udhaifu hapa nchini hujitayarisha kwa ajili ya kufanya hujuma na mashinikizo na wakati anapoona kazi kubwa na zenye taathira huvunjika moyo na kukata tamaa huku akijaribu kuficha uhakika huo; hivyo wananchi wote hususan maafisa na viongozi wa nchi wanapaswa kuimarisha moyo wa matumaini na nishati katika jamii kwa kufanya kazi na bidii zaidi. 1120848

captcha