IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Hitilafu kati ya Shia na Suni zinachochewa katika jamii ya Kiislamu

22:13 - November 19, 2012
Habari ID: 2451389
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Imam Ali Khameni amesema kuwa hitilafu kati ya Shia na Suni si suala jipya bali limekuwepo tokea huko nyuma na kuongeza kuwa, baadhi ya hitilafu hizo zimeongezeka kwa kiwango kisicho cha kawaida katika miaka ya hivi karibuni, suala linaloonesha kwamba hitilafu hizo zinachochewa katika jamii ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo mapema leo Jumatatu alipokutana na wasimamizi wa msafara wa hija wa Iran. Amesema kuwa, hija ya mwaka huu ilikuwa wajibu wa aina yake na amesisitiza juu ya umuhimu wa umoja katika ulimwengu wa Kiislamu. Amesema kuwa umoja, adhama na sura tofauti za ulimwengu wa Kiislamu hudhihiri na kujitokeza zaidi katika msimu wa hija na uwezo huo unapaswa kutumiwa kwa njia inayofaa.
Ayatullah Khamenei ameashiria kuwa faradhi ya hija ni mchanganyiko wa ibada, kunyenyekea, maombi na mahudhurio ya kisiasa na kijamii na akasema kuwa, kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mahujaji wa Kiirani walikuwa wakishughulishwa zaidi na suala la kutekeleza ibada ya hija kwa njia sahihi ilhali mjumuiko huo mkubwa na wa kipekee unajumuisha pia masuala mengine muhimu kama Waislamu wa mataifa mbalimbali, adhama na umoja ambavyo vinaweza kuanzisha harakati mpya ya kumjenga mwanadamu na jamii na umoja na mshikamano wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa mtazamo huo aali unapaswa kuenezwa kwa mahujaji wasio Wairani.
Moja ya mambo yaliyotiliwa mkazo na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni umuhimu wa umoja kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni.
Amesema kuwa hitilafu kati ya Shia na Suni si suala jipya bali limekuwepo tokea huko nyuma na kuongeza kuwa, baadhi ya hitilafu hizo zimeongezeka kwa kiwango kisicho cha kawaida katika miaka ya hivi karibuni, suala linaloonesha kwamba hitilafu hizo zinachochewa katika jamii ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa suala la kusisitiza juu ya umoja na maelewano kati ya Waislamu wa Shia na Suni pekee yake halitoshi na kuongeza kuwa, baadhi ya hitilafu hizo zinatokana na fikra potofu, na mtazamo huo usio sahihi unapaswa kusahihishwa. Amesema sehemu nyingine ya hitilafu hizo inatokana na mienendo isiyo sahihi na suala hili pia linapaswa kushughulikiwa na kutatuliwa.
Jambo jingine lililosisitizwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano wake na maafisa wa msafara wa hija wa Iran ni umuhimu wa kutanzuliwa masuala ya kisiasa ya mahujaji.
Ametaja machafuko ya sasa huko Syria kuwa ni mfano wa matatizo hayo na kusema msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kadhia hiyo uko wazi kabisa. Ameongeza kuwa ukweli wa mambo kuhusu kadhia ya Syria ni kuwa kambi ya ubeberu inataka kukata kizingo cha mnyororo wa mapambano katika eneo la Mashariki ya Kati katika eneo lililo jirani na utawala ghasibu wa Israel.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa, njia ya utatuzi wa mgogoro wa Syria ni kuzuia uingizaji wa silaha ndani ya nchi hiyo. Ameongeza kuwa iwapo wapinzani wa nchi yoyote watapewa silaha kutoka nchi za nje hapana shaka kuwa utawala wa nchi hiyo utakabiliana na waasi hao.
Amesema iwapo wapinzani nchini Syria wataweka chini silaha, kutakuwepo uwezekano wa kuitaka serikali isikilize mitazamo yao na kuwaruhusu waeleze misimamo yao.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewashukuru viongozi wa msafara wa hija kwa huduma nzuri zilizotolewa kwa mahujaji na kusisitiza juu ya udharura wa kuimarishwa zaidi ushirikiano kati ya maafisa hao.
Kabla ya hotuba ya Ayatullah Khamenei, mwakilishi wa Faqihi Mtawala na Amir wa msafara wa hija wa Iran Hujjatul Islam Walmuslimin Qadhi Askari ametoa ripoti kuhusu hatua zilizochukuliwa na ofisi ya hija ya Kiongozi Muadhamu katika masuala ya kiutamaduni, kiroho na kimataifa wakati wa ibada ya hija ya mwaka huu. 1140574

captcha