IQNA

Imam Khamenei:

Unyama mkubwa wa Wazayuni huko Gaza unapaswa kuamsha hisia za Waislamu

22:19 - November 21, 2012
Habari ID: 2452822
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo Jumatano amehutubia hadhara kubwa ya mamia ya wanaharakati wa mradi wa Mti Mzuri wa "Salihiin" akilitaja jeshi la wanamgambo la Basiji kuwa ni katika miujiza ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Ameashiria pia haja ya siku zote ya nchi, taifa, Mapinduzi na historia kwa Basiij na kusisitiza juu ya udharura wa kuboreshwa zaidi shughuli za taasisi hiyo.
Amezitaja jinai na ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika mashambulizi yake dhidi ya watu wa Ukanda Gaza kuwa ni kielelezo cha unyama wa kutisha wa viongozi wa utawala huo. Vilevile amezungumzia uovu mkubwa wa Marekani, Uingereza na Ufaransa wa kuendelea kuunga mkono mauaji yanayofanywa na Israel huko Gaza na akasema kuwa, nchi za Kiislamu hususan zile za Kiarabu zinapaswa kusahihisha mienendo yao katika kadhia hii na mbali na kuwasaidia watu wanaodhulumiwa lakini mashujaa wa Gaza, zifanye pia jitihada za kuvunja mzingiro wa eneo hilo. Vilevile ameutaka umma wa Kiislamu kufuata nyayo za mapambano ya watu wa Gaza na kuelewa kuwa kusimama kidete na mapambano ndio njia pekee ya uokovu na kuwashinda maadui wa Uislamu.
Katika sehemu kubwa ya hotuba yake ya leo Ayatullah Khamenei amezungumzia matukio ya sasa ya Gaza na kusisitiza kuwa ukatili wa Wazayuni katika mashambulizi yao dhidi ya watu wasio na hatia na raia wa Gaza unapaswa kuamsha hisia za ulimwengu wa Kiislamu na kuipa roho mpya harakati adhimu ya mataifa ya Waislamu.
Akiweka wazi athari mbaya za mashambulizi ya sasa ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza, Ayatullah Khamenei amesema, unyama wa kutisha wa viongozi wa utawala huo katika mashambulizi haya unaonesha kuwa, watu hawa wenye hulka za kinyama hawana chembe ya ubinadamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa jinai zinazofanywa na Wazayuni huko Gaza zinaweka wazi utambulisho wa maadui wa ulimwengu wa Kiislamu na sura halisi ya wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika jumuiya za kimataifa.
Ayatullah Khamenei amekosoa vikali uungaji mkono wa wazi wa mfumo wa ubeberu kwa jinai za Wazayuni na kusema: Marekani, Uingereza na Ufaransa hazijaukemea hata mara moja utawala katili na usio na huruma wa Israel na kwa kuunga mkono, kushajiisha na kudumisha jinai hizo zimeonesha jinsi maadui wakubwa na makatili wa umma wa Kiislamu walivyo mbali na maadili na ubinadamu.
Amehoji kwamba, vinara wa ubeberu ikiwemo Marekani ambayo inaunga mkono maafa yanayofanywa na Wazayuni makatili huko Gaza, wanathubutu vipi kuzungumzia kwa jeuri suala la haki za binadamu na kujifanya jaji na hakimu wa nchi na mataifa mengine katika uwanja huo?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mwenendo wa nchi za Kiarabu na Kiislamu pia kuhusu matukio ya Gaza si mzuri kwa sababu baadhi ya nchi hizo zimetosheka tu kwa maneno na hata baadhi yao hazikulaani walau kwa maneo matupu jinai za Wazayuni huko Gaza.
Amesema wale wanaodai kuhubiri umoja na uongozi wa ulimwengu wa Kiislamu wanaingilia na kujishughulisha waziwazi na masuala mengine yanayodhamini malengo yao ya kisiasa, lakini kwa kuwa katika kadhia hii ya Gaza anaonekana Marekani na Uingereza mkabala wao wamejizuia kuwalaani Wazayuni na zaidi wametosheka tu kwa kuwaunga mkono kimaneno watu wa Gaza.
Ayatullah Khamenei amezitaka nchi za Kiislamu hususan zile za Kiarabu kuanzisha harakati moja ya kuwasaidia watu anaodhulumiwa wa Gaza na kufanya juhudi za kukomesha mzingiro wa Wazayuni dhidi ya eneo hilo.
Amepongeza istiqama na ushujaa wa watu na vijana wa Gaza na akasema: Kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu watu hao wamethibitisha tena kuwa, inawezekana kuyashinda makundi makubwa yaliyojizatiti kwa silaha na yanayoungwa mkono na mabeberu kwa kutegemea imani, kusimama kidete na bidii.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kiherehere kilichoupata utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ajili ya kusitisha mapigano huko Gaza na kusema kuwa wale walioanzisha uovu huo wamepata kipigo zaidi kwa kadiri kwamba sasa wanahaha kwa ajili ya kusitisha mapigano mbele ya kundi dogo la watu wa Gaza.
Ayatullah Khamenei amesema, ujumbe wa matukio ya sasa ya Gaza kwa umma wa Kiislamu ni kwamba, nguvu za kimaada na kiroho na uwezo wao wa kujilinda mbele ya maadui wa Uislamu zimeongezeka. Amesema kuwa yanayotokea Gaza yameonesha kuwa, kujilinda na kujihami kwa nguvu na uwezo wote ndio njia pekee ya kushinda njama, uovu na usaliti.
Amesisitiza kuwa ili kuweza kuepuka shari za maadui, ulimwengu wa Kiislamu unalazimika kuzidisha nguvu yake ya imani, azma na irada, kupiga hatua kubwa za maendeleo katika nyanja za sayansi na teknolojia na kuwa na uwezo wa kutengeneza zana zinazohitajika maishani zikiwezo silaha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, taifa la Iran lilipata somo hilo wakati wa Vita vya Kujihami Kutakatifu na kwa sababu hiyo wananchi, vijana na wasomi wa nchi hii wanafanya bidii kubwa kwa ajili ya maendeleo na uwezo wa nchi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, moja ya masomo na darsa za matukio ya sasa ni udharura wa kuwa na umoja na mshikamano wa Kiislamu na pia umoja na mashikamano wa ndani ya kila taifa la Waislamu. Ameongeza kuwa ukweli huo unasadiki pia kwa taifa la Iran.
Katika uwanja huo, Ayatullah Khamenei amebainisha falsafa ya wito wake wa mara kwa mara wa kuwepo umoja na mshikamano hapa nchini na kusema: Wito wa kuwa na umoja unaotolewa siku zote kwa waandishi, wanaharakati wa sekta ya magazeti na kurasa za intaneti, mirengo mbalimbali ya kisiasa na viongozi wa serikali na wasio wa serikali ni kwa sababu umoja una taathira kubwa na muhimu katika uwezo na maendeleo ya nchi na katika kulinda nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongea umoja na mshikamano wa taifa la Iran na kuashiria jinsi viongozi wa vyombo vitatu vikuu vya dola walivyoitikia vyema wito wake wa kushikamana na kuwa na umoja na akasema kuwa, harakati hiyo nzuri na yenye thamani inapaswa kudumishwa.
Amezungumzia pia suala la kusailiwa Rais wa Jamhuri bungeni na kusema, harakati hiyo inapaswa kupongezwa katika mitazamo miwili.
Akifafanua zaidi suala hilo, Ayatullah Ali Khamenei amesema kumsaili Rais wa Jamhuri na viongozi wengine wa serikali ni kielelezo cha kuwajibika kwa wabunge kuhusu masuala ya nchi. Amesema kuwa viongozi wa serikali pia wametangaza utayarifu wao wa kwenda kutoa maelezo na majibu kwa kujiamini na ushujaa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa hatua ya Bunge ya kutekeleza majukumu yake na itikadi ya Serikali juu ya usahihi wa kazi na shughuli zake ni mtihani kwa vyombo vyote viwili, lakini tunaamini kuwa harakati hiyo inatosha na haipasi kuendelea.
Amesema wananchi pia wanaelewa na wanajua kwamba kuendelea harakati hiyo kutahudumia malengo ya adui.
Katika hotuba hiyo Ayatullah Khamenei amesema kuwa kusadifiana Wiki ya Basiji na tukio kubwa la Ashura ni jambo linalotoa darsa na ibra. Ameongeza kuwa, iwapo tukio la kusikitisha lakini lenye ibra na somo la Karbala lisingetukia basi Uislamu ungetoweka; kwa sababu hiyo tukio la Ashura linapaswa kuwa somo na ibra daima na kuwa bendera ya uongofu mbele ya jamii ya Kiislamu.
Amesema kuwa kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu kinakumbusha baadhi ya matukio ya kujitolea mhanga ya masahaba wa Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein (as) na kuongeza kuwa, jeshi la Basiji ni miongoni mwa madhihirisho makubwa na muhimu zaidi ya kujitolea huko. 1142087

captcha