IQNA

Imam Khamenei abainisha sifa za rais ajaye wa Iran

21:13 - April 28, 2013
Habari ID: 2525386
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei Jumamosi hii (27 Aprili) amehutubia hadhara kubwa ya maelfu ya wafanyakazi, wadau wa sekta ya uzalishaji na wafanyakazi bora. Ameashiria haja ya nchi kwa hamasa na harakati kubwa katika medani za uchumi na siasa na kuutaja uchaguzi kuwa ni muhimu na medani ya kudhihiri uwezo na nguvu ya taifa.
Ayatullah Khamenei amewausia wanaotaka kugombea urais kufanya tathmini sahihi kuhusu uwezo wao na nafasi ya utekelezaji hapa nchini na kusisitiza kuwa, nchi na taifa kubwa na shujaa la Iran linahitaji Rais shujaa katika medani za kimataifa na mbele ya mabeberu, mwenye sera nzuri, hekima, tadbiri, mwenye kuamini uchumi wa kimapambano, mwenye maadili na akhlaki njema, asiyejihusisha na masuala yasiyokuwa ya msingi na mwenye nara za kimantiki na zinazooana na hali halisi.

Katika mkutano huo uliofanyika kwa mnasaba wa wiki ya wafanyakazi, Ayatullah Khamenei amesema sifa kubwa zaidi ya wafanyakazi ni kujitolea kikamilifu kwa ajili ya maendeleo na hali bora ya nchi na kuongeza kuwa, wafanyakazi ndio uti wa mgongo wa jamii na iwapo hautakuwepo au ukidhoofika basi nchi itapatwa na maradhi ya kupooza.

Amesisitiza juu ya udharura wa kupewa mazingatio makhsusi suala la kazi na mfanyakazi katika nyanja za utamaduni, utungaji sheria na utekelezaji wake na akasema kuwa iwapo tabaka la wafanyakazi litakuwa na matumaini, hali bora na usalama wa kazi, basi harakati ya nchi katika njia ya maendeleo itakwenda kwa kasi na urahisi zaidi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mchango mkubwa na nafasi maalumu ya wafanyakazi katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na vilevile katika awamu mbalimbali za Mapinduzi ikiwa ni pamoja na katika kipindi cha kujitetea kutakatifu na akasema: Katika kipindi chote cha miaka 34 iliyopita zimefanyika jitihada kubwa za kulifanya tabaka la wafanyakazi likabiliane na Mapinduzi ya Kiislamu na utawala wa Kiislamu lakini wafanyakazi wenye imani madhubuti, wanamapinduzi na mashujaa walisimama kidete mbele ya njama hizo zote na suala hilo ni fahari kubwa kwa tabaka la wafanyakazi.

Amezungumzia hatua ya kuitwa mwaka uliopita kwa jina la Mwaka wa Kuunga Mkono Uzalishaji wa Kitaifa, Kazi na Rasilimali za Kiirani na akasema kuwa, kuunga mkono uzalishaji wa kitaifa si makhsusi kwa ajili ya mwaka mmoja tu bali suala hilo linapaswa kufuatiliwa kwa nguvu kubwa zaidi.

Amelitaja suala la kueneza utamaduni wa kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kuwa ni muhimu sana na kuongeza kuwa, utamaduni huo unapaswa kuenezwa kati ya wananchi na kueleweka kwamba, kutumia bidhaa zilizozalishwa ndani au nje ya nchi kunaweza kumpa au kumnyima pato mfanyakazi wa Kiirani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameliambia taifa la Iran kwamba: ”Takwa langu kwa taifa zima ni kwamba tumieni bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi."

Imam Khamenei amesema asasi za serikali pia haziruhusiwi kukidhi mahitaji yake kwa kutumia bidhaa za nje na kuongeza kuwa, wazalishaji wa ndani wakiwemo viongozi wa taasisi mbalimbali, wafanyakazi na wawekezaji pia wanapaswa kutengeneza bidhaa zenye ubora kamili na wa juu.

Ameashiria pia amri ya Uislamu inayowataka watu wafanye kazi zao kwa ukamilifu sambamba na kuheshimiwa wafanyakazi, kuwadhaminia usalama wa kazi na kulinda rasilimali na akasema kuwa: Uislamu, tofauti na mitazamo ya kiuchumi ya kiliberali na kisoshalisti, umekhitari njia ya kati na kuhimiza mno juu ya mtazamo wa kiutu na uadilifu kuhusu kazi, mfanyakazi na rasilimali.

Imam Khamenei amesema uovu na makosa ya uchumi kibepari umeonekana wazi na kuongeza kuwa, upinzani unaoonekana sasa katika nchi za Ulaya katika medani ya uchumi na hata huko Marekani ni kielelezo kikubwa zaidi cha upotofu na kutokuwa sahihi sera za uchumi wa kibepari.

Ayatullah Khamenei amesema matukio ya sasa huko Ulaya na Marekani ni mwanzo tu na hali ya mambo itakuwa mbaya zaidi kwa sababu uchumi wa kibepari uko katika hali ya kuporomoka.

Ameongeza kuwa matatizo ya sasa ya kiuchumi ya Magharibi ni sehemu ya mporomoko wa ustaarabu wa Magharibi unaojumuisha pia matatizo ya kimaadili na kiutamaduni.

Akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hatua ya mwaka huu kupewa jina la Mwaka wa Hamasa ya Kiuchumi na Kisiasa na akasisitiza kuwa, hamasa ina maana ya harakati ya kijihadi na hai na suala hili linapaswa kupewa mazingatio na wananchi na viongozi; kwa msingi huo kuna udharura wa kutambua nakisi zilizopo na kuweka mipango sahihi kwa ajili ya kutayarisha uwanja mzuri wa hamasa.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, mipango yote ya serikali inapaswa kutilia maanani maisha ya tabaka la watu dhaifu.

Amesema kuwa harakati na hamasa ndio sharti la maendeleo ya nchi na kuongeza kuwa, hamasa ya kiuchumi na ya kisaisa ni mapacha wasiotengana na kila mmoja wao anamlinda na kumuimarisha mwenzake.

Ameashiria njama kubwa zinazofanywa na maadui wa taifa la Iran na kusema, wanatumia mashinikizo ya kiuchumi kwa lengo la kuzusha mgawanyiko na ufa kati ya wananchi na utawala wa Kiislamu hapa nchini na hatimaye kuwavunja moyo wananchi na wakati huo huo wanasema uongo tena kwa jeusi kwamba, hawana uadui na wananchi wa Iran.

Ayatullah Khamenei amesema iwapo harakati kubwa ya kiuchumi itapewa mazingatio makubwa na asasi za utekelezaji na zile za kutunga sheria hapa nchini, basi mashinikizo yote ya kiuchumi yataambulia patupu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa hamasa ya kisiasa ina maana ya kuhudhuria wananchi katika medani ya kisiasa na utawala wa nchi. Ameongeza kuwa mfano wa wazi wa hamasa ya kisiasa ni uchaguzi ujao ambao kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu utafanyika kwa wakati na kuwashirikisha wananchi wengi.

Ayatullah Khamenei amesema maadui wa taifa la Iran wanafanya mikakati ya kupunguza ushiriki wa wananchi katika uchaguzi ujao kwa lengo la kukabiliana na hamasa ya kisiasa na kuongeza kuwa, wapangaji wa nyuma ya pazia wa ubeberu bado hawajajua moyo wa imani na kusimama kidete wa taifa la Iran licha ya kupita miaka mingi ya uadui na uhasama.

Amesema katika kipindi chote cha miaka 34 iliyopita daima taifa la Iran ndilo lililostahiki sifa na pongezi kwani viongozi wa nchi wasingeweza kusimama kidete bila ya msaada na kupata uungaji mkono wa wananchi, na hali hiyo itaendelea.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa uchaguzi ni muhimu na uwanja wa kudhihirisha nguvu na uwezo wa kitaifa. Ameongeza kuwa, taifa lililohai na lenye nishati na linalotegemea matakwa, irada ya Allah na msaada wake litashinda daima katika nyanja mbalimbali ukiwemo uwanja wa uchaguzi.

Ameashiria kauli aliyotoa wiki kadhaa zilizopita kuhusu uwezekano wa kushiriki watu wenye mielekeo mbalimbali wenye imani na Mapinduzi ya Kiislamu katika uchaguzi ujao na akaongeza kuwa, watu wanaoingia katika kinyanganyiro hicho wanapaswa kutathmini vyema uwezo wao na nafasi ya uongozi hapa nchini na kutofanya makosa ya mahesabu. Amesisitiza kuwa taifa la Iran ndilo litakalokuwa na kauli ya mwisho katika uchaguzi ujao.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema taratibu za uchaguzi hapa nchini zinafanyika kwa njia imara.

Ameeleza baadhi ya sifa anazopaswa kuwa nazo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Katika daraja ya kwanza Rais wa Jamhuri anapaswa kuwa mtu mwenye imani na itikadi ya Mungu mmoja, wananchi na katiba na katika daraja ya pili awe na moyo wa mapambano.
1218685
captcha