IQNA

Imam Khamenei

'Mwamko wa Kiislamu utajenga upya utamaduni wa Kiislamu'

21:20 - April 30, 2013
Habari ID: 2526644
Mkutano wa Kimataifa wa Maulamaa na Mwamko wa Kiislamu umeanza Jumatatu Aprili 29 mjini Tehran ukihudhuriwa na mamia ya wasomi, wanafikra na wanazuoni wa kidini kutoka katika ulimwengu wa Kiislamu. Mkutano huo umefunguliwa kwa hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ayatullah Ali Khamenei.
Punde baada ya kuwasili katika ukumbi wa mkutano huo Ayatullah Khamenei amekutana na kuzungumza na maulamaa kadhaa wanaoshiriki mkutano huo. Baada ya hapo Imam Khamenei ametoa hotuba muhimu akichunguza vikwazo vinavyoikabili harakati ya Mwamko wa Kiislamu huko Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati katika mitazamo mitano ambayo ni ulazima wa kulindwa vituo vya kidini kama marejeo ya Waislamu, kubuni malengo ya muda mrefu, kujiepusha na tajiriba chungu ya kuamini ahadi za Magharibi, kuwa macho mbele ya njama za kuzusha mapigano ya umwagaji damu ya kimakundi, kimadhehebu na kikaumu, na kutosahau kadhia ya Palestina kama kigezo kikuu na medani asili ya harakazi zote. Amesisitiza kuwa kusimama imara katika misingi ya Kiislamu na kuhudhuria katika medani ndizo sababu mbili kuu na muhimu zitakazopelekea kubatilishwa njama zote, propaganda chafu na hila za maadui.

Mwanzoni mwa hotuba yake Ayatullah Khamenei ameutaja Mwamko wa Kiislamu kuwa ni tukio la kustaajabisha ambalo iwapo libakia salama na kudumishwa litatayarisha uwanja mzuri wa wa kuibuka upya ustaarabu wa Kiislamu upeo usiokuwa mbali.

Ameashiria jinsi kambi ya ubeberu na wasiopenda maendeleo inavyoogopa neno Mwamko wa Kiislamu na kusema kuwa: Mwamko wa Kiislamu sasa ni hakika ambayo ishara zake zinaweza kuonekana katika dunia yote ya Kiislamu na kielelezo chake kikuu ni hamu ya fikra za waliowengi hususan tabaka la vijana ya kuhusisha fahari na adhama ya Uislamu na kudhihiri sura mbaya, ya kidhalimu na kiistikbari ya madola ya kibeberu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema upeo wa mwamko huo wenye baraka ni mkubwa na kuongeza kuwa, kutimia kimiujiza ahadi za Mwenyezi Mungu ni ishara inayotia matumaini inayotoa bishara ya kutimia ahadi kubwa zaidi.

Ayatullah Khamenei ametoa mifano ya Qur’ani ya kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu ambazo zinatayarisha uwanja wa kutimia ahadi kubwa zaidi na kusema, hiyo ni taktiki na mipango yake Mola. Amesisitiza kuwa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni mfano wa wazi wa mipango hiyo ya Alllah kwa sababu siku Uislamu ilipopata ushindi nchini Iran na kuweza kuvunja ngome ya Marekanai na Uzayuni katika mojawapo ya nchi nyeti sana katika Mashariki ya Kati, wale wenye hekima na busara walitambua kwamba, iwapo watakuwa na subira na kuona mbali ushindi mwingine utapatikana.

Amesema kuwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na matunda yake vilipatikana chini ya kivuli cha kuwa na imani na ahadi za Mwenyezi Mungu, subira, kusimama kidete na kuomba auni na msaada wa Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa, hii leo tajiriba hii yenye thamani iko mikononi mwa mataifa mbalimbali ambayo yamesimama kupambana na ubeberu na udikteta na kuweza kupindua au kuyumbisha tawala mbovu, vibaraka na tegemezi kwa Marekani.

Baada ya utangulizi huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amechambua Mwamko wa Kiislamu, changamoto na vitisho vinavyozikabili harakati mbalimbali. Nukta ya kwanza iliyoashiriwa na Ayatullah Khamenei ni nafasi na mchango mkubwa na muhimu wa maulamaa wa dini na wanamageuzi wa kidini katika matukio na harakati za marekebisho katika Mashariki ya Kati na kwenye nchi za Kiislamu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kazi kubwa na nzito ya wanazuoni wa dini katika uwanja huo na kusema kuwa: Maulamaa wa dini na wafuasi wa dini wanapaswa kuwa macho kikamilifu.

Ayatullah Ali Khamenei ameashiria pia jitihada za vibaraka wa Marekani na Uzayuni kwa ajili ya kubuni marejeo ya kifikra yasiyoaminika na kuwatia madoa watu wanaoshikamana na dini na takwa na akasema kuwa, kuketi katika meza iliyojaa maakuli ya aina mbalimbali ya kidunia, kuchafuliwa na hisani na bakshishi za wenye mali na kuwa na ushirikiano na mataghuti wa matamanio ya nafsi na madaraka ndio sababu kuu ya kutengana na wananchi na kupoteza imani na mapenzi yao.

Nukta ya pili iliyozungumziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika uchambuzi wake wa changamoto za Mwamko wa Kiislamu ni udharura wa kubuni malengo ya muda mrefu na ya mwisho ya mwamko wa Kiislamu.

Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa lengo hilo la mwisho si kitu kingine ghairi ya kutengenza ustaarabu wa kung’ara wa Kiislamu.
1219899
captcha