IQNA

Ayatullah Khamenei:

Kutunza nyumba na kuzaa watoto ni jihadi kubwa na sanaa ya wanawake

10:48 - May 02, 2013
Habari ID: 2527326
Kiongozi Muadhamu wa mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Imam Ali Khamenei amesema kuwa Amekosoa mtazamo wa Magharibi kuhusu suala la mwanamke na kusisitiza kuwa: Mtazamo wa Uislamu kuhusu haki za kijamii na za mtu binafsi za mwanamke na mwanaume ndio wenye mantiki zaidi, imara zaidi na wa kielimu zaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amehutubia umati mkubwa ulioshiriki katika majlisi hiyo iliyowakutanisha pamoja malenga na wasomaji wa tungo zinazotaja sifa na matukufu ya Ahlulbait wa Mtume wetu Muhammad (saw) akiwapongeza Waislamu kwa mnasaba wa siku hii tukufu ya kuazliwa Bibi Fatimatu Zahraa (as) na kukutana kwake na siku aliyozaliwa ndani yake mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhullah Khomeini. Ameitaja kazi ya kusoma mashairi na sifa za Ahlul Bait (as) kuwa ni mbinu ya kisanii ya kuzidisha maarifa, matumaini na kuamsha hisia katika nyoyo za watu. Amekosoa mtazamo wa Magharibi kuhusu suala la mwanamke na kusisitiza kuwa: Mtazamo wa Uislamu kuhusu haki za kijamii na za mtu binafsi za mwanamke na mwanaume ndio wenye mantiki zaidi, imara zaidi na wa kielimu zaidi.
Ayatullah Khamenei amekutaja kuwepo vipawa vikubwa na nyoyo zenye shauku kati ya wasomaji wa tungo za kuwasifu Watu wa Nyumba ya Mtume wetu kwa ajili ya kupanua ibada ya kutawasali na kudhihirisha mapenzi kwa Ahlulbait (as) kuwa ni fursa yenye thamani na neema kubwa hapa nchini. Ameongeza kuwa, kazi ya wasomaji tungo za kumsifu Mtume (saw) na Ahlul Baiti zake ni kuamsha hisia na kuziongoza kuelekea kwenye akili na fikra na katika kipindi chote cha historia kazi hii ya kuweka pamoja hisia, akili na mantiki imelinda masuala ya kiroho, dini na maadili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria taathira kubwa ya kusomwa kasida au mashairi katika kueneza maarifa ya kidini na kusema kuwa, fursa hii inapasa kutumiwa vyema.
Ayatullah Khamenei amekutaja kutumia kipawa cha mashairi na tungo mbalimbali kwa ajili ya kuzusha hitilafu na kuchochea taasubi na chuki za kimadhehebu kuwa ni kielelezo cha kupoteza fursa ya mashairi na tungo za kumsifu Mtume na Ahlul Bait (as).
Amezungumzia suala la kupanuka na kuongezeka zana za mawasiliano na utumiaji wa mienendo isiyokuwa ya kimantiki katika kuzusha hitilafu za kimadhehebu na akasema kuwa: Kuzusha hitilafu na kuchochea chuki za kimadhehebu ni hatua isiyokuwa sahihi na isiyokuwa na maslahi. Amesema kuwa maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) walikuwa wakizuia mienendo kama hiyo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuchochea hitilafu za ndani ni mfano mwingine wa kupoteza fursa na kuongeza kuwa, mwaka huu wa Hijria Shamsia umepewa jina la Mwaka wa Hamasa ya Kisiasa na Hamasa ya Kiuchumi na hamasa inaongozwa kwa akili na kusaidiwa na imani na kuchemka moyoni.
Amesema sharti la kuwepo hamasa ni kuwepo anga ya matumaini, nia njema na mtazamo chanya kuhusu mustakbali bora wa nchi. Ameongeza kuwa, hamasa haiwezi kupatikana kwa kuweka tashwishi na ukosefu wa matumaini katika fikra za wananchi au kwa kuwataka wajitenge, kutofanya kazi na kuwa wazembe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, harakati ya kudumu na ya kijihadi inayohitajiwa na kila nchi na kila ustaarabu kwa ajili ya maendeleo na ustawi inapitia katika njia ya nishati, shauku na kuwa na matumaini na kwamba washairi na wasomaji wa tungo mbalimbali wana mchango mkubwa katika kuzidisha maarifa na kupanda mbegu za hekima, matumaini na itikadi thabiti.
Ameashiria jinsi watu wanavyozingatia na kutazama kwa jicho makhsusi mienendo na maadili ya mahatibu wa kidini na wasomaji mashairi na kusema kuwa, kadiri walinganiaji wa dini na watu wanaosoma tungo za kumsifu Mtume na Ahlubaiti zake wanavyojipamba kwa uchamungu, maadili mema, dini na usafi wa moyo na ulimi, ndivyo wanavyoweza kuwa na taathira kubwa katika nyoyo na katika kuzidisha maarifa ya watu.
Suala la pili lililozungumziwa na Imam Khamenei katika hotuba yake ni udharura wa kumuenzi na kumkirimu mwanamke.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa siasa za nchi za Magharibi kuhusu mwanamke na kusema: Harakati iliyofanywa na ustaarabu wa kimaada wa Magharibi kuhusu maudhui ya mwanamke ni dhambi kubwa na isiyosameheka na taathira zake mbaya haziwezi kufidiwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa vielelezo vya ustaarabu wa Magharibi kuhusu suala la mwanamke ni kumuanika, kutayarisha uwanja nzuri wa kutumiwa mwanamke kwa ajili ya starehe ya wanaume na kumvunjia heshima; mambo ambayo Wamagharibi wanayataja kuwa ni uhuru na kinyume chake kuwa ni kumfanya mateka mwanamke.
Amesema matokeo ya mtazamo kama huo kuhusu mwanamke ni kusambaratika taasisi ya familia. Ameongeza kuwa, pale nguzo za familia zinapoyumbayumba katika jamii yoyote suala hilo husababisha matatizo katika jamii husika; na ustaarabu wa Magharibi utashindwa na kuporomoka kutokana na sheria za kihabithi zinazohusiana na masuala ya kujamiiana zinazotekelezwa katika nchi za Magharibi.
Imam Khamenei amesema: Kutoweka kwa ustaarabu hufanyika taratibu na hatua kwa hatua, sawa kabisa na kuundwa kwake na hali hiyo ndiyo inayotokea sasa kuhusu ustaarabu wa Magharibi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendeza hotuba yake kwa kueleza mtazamo wa Qur’ani Tukufu na nafasi makhsusi ya mwanamke katika Uislamu na kusema: Mtazamo huo ndio wa kimantiki, imara na wa kielimu zaidi. Ameongeza kuwa hakuna tofauti mbele ya Mwenyezi Mungu kuhusu daraja za kiroho na kimaanawi na katika haki za kijamii na za mtu binafsi kati ya mwanamke na mwanaume, japokuwa kila mmoja ana sifa zake tofauti na za mwenzake kwa mujibu wa maumbile ya mwanadamu.
Ametaja baadhi ya sifa makhsusi za mwanamke ikiwa ni pamoja na kutunza nyumba, kuzaa watoto, hamu ya kulinda mazingira ya familia, kulea na kukuza watoto na kusisitiza kuwa, kutunza nyumba na kuzaa ni jihadi kubwa na sanaa ya wanawake ambayo huambatana na subira, hisia safi na upendo; mambo ambayo iwapo yatapewa umuhimu yanaweza kudhamini maendeleo na ustawi wa jamii.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha udharura wa kumheshimu na kumkirimu mwanamke na akasema kuwa, kuna ulazima wa kuamiliana na wanawake kwa heshima na upendo sambamba na uungana na staha.
Mwanzoni mwa mkutano huo malenga na wasomaji tungo za kumsifu Mtume na Ahlibaiti zake kadhaa walisoma tungo zao wakieleza nafasi adhimu na kubwa ya binti wa Mtume Muhammad (saw), bibi Fatimatu Zahraa (as). 1221494
captcha