IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kitendo cha kuvunjiwa heshima kaburi la Sahaba Hujr bin Adi kinapaswa kulaaniwa

22:59 - May 06, 2013
Habari ID: 2529476
Imam Ayatullah Khamenei ameashiria tukio chungu na la kusikitisha la kuvunjiwa heshima kaburi la Sahaba wa Mtume (saw) Hujr bin Adi (ra) huko Syria na akasisitiza kuwa: Waislamu hususan wasomi na shakhsia wa kielimu, kisiasa na kidini katika ulimwengu wa Kiislamu wanawajibika kukabiliana na fikra hizi chafu na kuzuia kuenea moto wa fitina.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amekutana na kuhutubia mkusanyiko wa maafisa wanaosimamia uchaguzi wa rais na mabaraza ya miji na vijiji na kusisitiza kuwa, mahudhurio makubwa ya wananchi katika uchaguzi ujao wa rais yatalinda na kudumisha maendeleo ya nchi. Amesisitiza pia juu ya udharura wa taasisi zinazosimamia uchaguzi na wagombea wote kushikamana barabara na kuheshimu sheria katika awamu zote.
Imam Ayatullah Khamenei ameashiria tukio chungu na la kusikitisha la kuvunjiwa heshima kaburi la Sahaba wa Mtume (saw) Hujr bin Adi (ra) huko Syria na akasisitiza kuwa: Waislamu hususan wasomi na shakhsia wa kielimu, kisiasa na kidini katika ulimwengu wa Kiislamu wanawajibika kukabiliana na fikra hizi chafu na kuzuia kuenea moto wa fitina.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema uchaguzi ni amana kubwa na thamani ya kitaifa na Kiislamu na akaongeza kuwa, Baraza la Walinzi wa Katiba, na majmui ya taasisi zinazosimamia, kutekeleza na zile zinazolinda amani na usalama wa uchaguzi ndio wanaobeba amani hiyo kubwa na zina kazi muhimu, yenye thamani na ya kubakia siku zote.
Ayatullah Khamenei ameashiria mchango muhimu wa uchaguzi katika kuhuisha nchi na akasema kuwa, mahudhurio ya wananchi katika chaguzi mbalimbali zilizofanyika katika kipindi cha miaka 34 iliyopita yameikinga nchi na balaa za aina mbalimbali na kutia moyo na ari mpya katika moyo wa nchi, taifa na Mapinduzi ya Kiislamu.
Ameutaja uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 14 Juni kuwa una muhimu mkubwa zaidi ukilinganishwa na ule uliopita na kuongeza kuwa, kufanyika chaguzi mbili za rais na mabaraza ya miji kwa wakati mmoja ni miongoni mwa mambo yanayoupa umuhimu uchaguzi ujao.
Ayatullah Khamenei amesema kuundwa mabaraza ya miji na vijiji katika vijiji na miji yote hapa nchini ni dhihirisho la kushirikishwa wananchi katika mchakato wa kuchukua maamuzi na kazi zote na amewausia viongozi, wananchi na shakhsia wote kwamba uchaguzi wa rais usiwafanye wapuuze chaguzi za mabaraza ya miji na vijiji.
Akiendelea kueleza umuhimu mkubwa wa uchaguzi wa tarehe 15 Juni, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mamlaka ya rais na majukumu yake makubwa katika katiba ya nchi na sheria nyingine na akasema kuwa, nafasi hiyo ya rais inaonesha kuwa uchaguzi wa rais ni suala lenye umuhimu mkubwa.
Ayatullah Khamenei amesema Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu ndiye mhandisi wa mahudhurio makubwa ya wananchi na kushirikishwa kwao katika masuala mbalimbali ya utawala wa Kiislamu hapa nchini.
Vilevile ameashiria njama zinazofanywa na baadhi kwa ajili ya kudhoofisha na kupunguza mahudhurio ya wananchi katika nyanja mbalimbali na kusema: Baadhi ya watu wanafanya jitihada za kuwafanya wananchi wasishiriki kwa wingi katika uchaguzi ujao au usifanyike katika wakati uliopangwa lakini njama hizo zitafeli kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu.
Imam Khamenei amesema nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inategemea nyoyo, hisia, akili, fikra, kuona mbali na mahudhurio ya wananchi katika masuala mbalimbali na kama nguzo hiyo muhimu yaani wananchi isingekuwepo basi mabeberu waovu duniani wasingeiacha hai Jamhuri ya Kiislamu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake mbele ya hadhara ya maafisa wanaosimamia uchaguzi wa rais na mabaraza ya miji na vijiji, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza umuhimu wa kushikamana na sheria katika awamu zote za uchaguzi huo.
Ameashiria jitihada za siku zote za madola ya kigeni za kutaka kufifiza na kuzima athari nzuri za mahudhurio ya wananchi katika masanduku ya kupigia kura na akasema kuwa, katika uchaguzi uliopita wa rais pia waliwalazimisha baadhi ya watu kutenda kinyume na sheria kwa shabaha ya kuwachochea wananchi na kuwapambanisha na utawala wa Kiislamu hapa nchini lakini njama hizo zilishindwa kwa baraka zake Mwenyezi Mungu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kushikamana kikamilifu na sheria ndio njia ya kuzuia matatizo katika uchaguzi na amewataka wananchi wote katika miji na vijiji kuhakikisha kwamba kila mtu anafuata na kutekeleza sheria.
Vilevile amewataka viongozi na maafisa wote wanaosimamia uchaguzi kutekeleza sheria kikamilifu katika awamu zote za kuchunguza ustahiki wa wagombea, katika kusimamia zoezi la uchaguzi, kuhesabu kura, kulinda masanduku ya kura na kadhalika na kutenda kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu sifa za wagombea kiti cha rais, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Tunataka kumpa funguo za kuongoza nchi mchapakazi, mtu wa watu na mwenye kujali thamani. Amesema Rais wa Jamhuri anapaswa kuwa mtu mwenye msimamo imara mbele ya maadui, mwenye tadbiri, anayeshikamana na kuheshimu sheria na anayejali watu wa matabaka yote na kuelewa mashaka ya wananchi.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Ayatullah Khamenei ameashiria tukio chungu na la kusikitisha la kuvunjwa kaburi la Sahaba mkubwa wa Mtume (saw) Hujr bin Adi na kuvunjiwa heshima mwili wake na akasema: Jambo linalozidisha uchungu wa tukio hili ni kuwepo katika Umma wa Kiislamu watu wenye fikra chafu, mgando na zilizodumaa na kubakia nyuma ambao wanakutambua kuwaenzi watu adhimu na shakhsia wakubwa wa zama za awali za Uislamu kuwa ni shirki na ukafiri.
Amesema kuwepo kwa fikra kama hizi za hurafa ni msiba kwa Uislamu na Waislamu na kuongeza kuwa, watu hawa ndio wale ambao mababu zao walivunja makaburi ya Maimamu katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) katika eneo la Baqii mjini Madina na kama si kusimama imara Waislamu kote duniani, basi hata kaburi tukufu la Mtume wa Allah pia wangelivunja.
Imam Ayatullah Ali Khamenei amesema watu wenye fikra mbaya kama hizi ambao wanakutambua kwenda kwenye haram za watu adhimu na mawalii wa Mungu kwa ajili ya kuwaombea rehma za Mwenyezi Mungu na kujiombea wao wenyewe kuwa ni shirki wana fikra batili na nyoyo chafu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa shirki ni ile inayofanywa na watu vibaraka na nyenzo za siasa na mashirika ya kijasusi na Marekani na Uingereza na wanaowatia simanzi Waislamu kwa vitendo vyao.
Amehoji kuwa, ni fikra gani hizi ambazo hazikutambui kutii, kuwaabudu na kunyenyekea mbele ya matwaghuti hai kuwa ni shirki na wakati huo huo zinakutambua kuwaenzi watu adhimu kuwa ni shirki?
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema tapo ovu linalowakufurisha Waislamu na linalopewa misaada ya kifedha na isiyo ya kifedha ni msiba mkubwa na halisi kwa Uislamu.
Ameashiria msimamo sahihi wa jamii kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika kukabiliana na tukio hilo na kusema: Mashia hawakutumbukia katika mchezo wa adui unaotaka kuchochea moto wa hitilafu kati ya Waislamu wa madhehebu za Suni na Shia na wameonesha jinsi walivyokomaa kiakili.
Vilevile amesifu msimamo wa Waislamu wa madhehebu ya Suni akisema umedhihirisha werevu na mtazamo aali. Amesisitiza kuwa jibu la Waislamu dhidi ya tukio hilo chungu na kulaaniwa kitendo hicho kiovu kunapaswa kuendelea kwa sababu iwapo wasomi, wanafikra na shakhsia wa kisiasa wa Umma wa Kiislamu hawatatekeleza wajibu wao, fitina hazitaishia hapo.
Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza juu ya udharura wa kuzimwa moto wa fitina hiyo kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisiasa, kutoa fatuwa za kidini na makala za wasoni na wanafikra.
Ayatullah Ali Khamenei amesema mikono ya maadui inadhihiri katika vitendo kama hivi na kuongeza kuwa, jumuiya mbalimbali, shakhsia wa kimataifa na wanasiasa wanaofanya vikao vya misiba kutokana na kubomolewa athari moja ya kale wamenyamaza kimya mbele ya kitendo hiki kiovu cha kuvunjwa kaburi na kuvunjiwa heshima mwili wa Sahaba wa Mtume.
Amesema Mwenyezi Mungu anaona yote wanayoyatenda na atashinda vitimbi vyote vya maadui na atalizuia tapo linalotaka kukwamisha umoja na maendeleo ya Umma wa Kiislamu.
Mwanzoni mwa mkutano huo Katibu wa Baraza la Kulinda Katiba Ayatullah Ahmad Jannati alitoa ripoti fupi juu ya kuundwa kamati za kusimamia uchaguzi na mwenendo wa kuchunguzwa sifa za waliojiandikisha kwa ajili ya kugombea katika uchaguzi ujao.
Vilevile Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Muhammad Najjar amezungumza uchaguzi ujao wa Rais na mabaraza ya miji na vijiji na kusema maandalizi ya chaguzi hizo yalikamilika tangu miezi kadhaa iliyopita. 1223710

captcha