IQNA

Imam Khamenei atoa wito wa umoja wa Waislamu

22:19 - June 08, 2013
Habari ID: 2544130
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumamosi) ameonana na wahadhiri, maqarii na mahafidh wa Qur’ani Tukufu walioshiriki kwenye Mashindano ya Thelathini ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya mjini Tehran na kutaja moja ya mafundisho makubwa ya Qur’ani Tukufu ni kuwataka Waislamu walinde umoja, mshikamano, mapenzi na ushirikiano baina yao.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, leo hii kila koo na ulimi unaowalingania Waislamu kwenye umoja na mshikamano basi ni koo ya Mwenyezi Mungu na koo na ulimi wowote unaochochea uadui kati ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe na kati ya madhehebu za Kiislamu, basi ulimi huo ni wa shetani.

Ayatullahil Udhma Khamenei pia amesisitiza katika mkutano huo juu ya ulazima kwa Waislamu kuzidi kuwa na ukuruba na mapenzi makubwa kwa Qur’ani Tukufu na kuzidi kufundishwa Waislamu mafundisho yaliyojaa uongofu na ufanisi ya Kitabu hicho Kitukufu cha Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: Moja ya miito na milinganio ya Qur’ani kwa Waislamu ni umoja na kushikamana kwenye kamba moja ya Mwenyezi Mungu na kutofarikiana na kwamba mkabala wa jambo hilo kuna mafundisho na mbinu za wakoloni ambao lengo lao kuu ni kuzusha mizozo na mifarakano katika umma wa Kiislamu na kushadidisha taasubu za kimadhehebu baina ya Waislamu wenyewe kwa wenywe.

Aidha ameashiria jinsi baadhi ya tawala na serikali za nchi za Kiislamu zilivyotekwa kifikra na madola ya kibeberu na kufanywa zicheze mchezo unaotakiwa na mabeberu hao na amekumbusha kuwa: Umoja na mshikamano kati ya Waislamu ni jambo la faradhi linalopaswa kutekelezwa haraka sana.

Kiongozi Muadhamu ameyataja mauaji wanayofanyiwa Waislamu, ugaidi usio na macho na majanga yanayosababishwa na ugaidi huo na kupata fursa utawala wa Kizayuni wa Israel kutekeleza jinai na njama zake za kibeberu ni katika matunda maovu ya kuwepo mifarakano katika umma wa Kiislamu.

Ameongeza kuwa: Leo hii ni wakati wa kutahiniwa Waislamu pamoja na serikali za nchi za Kiislamu na kwamba mataifa ya Kiislamu yanapaswa kuwa macho sana katika kipindi hiki nyeti.

Ayatullahil Udhma Khamenei ameashiria pia wimbi la kueneza chuki dhidi ya Uislamu lililoanzishwa na nchi za Magharibi dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza kuwa: Maadui wa Kimagharibi, wamewaelekezea ncha za upanga Waislamu duniani, hivyo umma huu wa Kiislamu unapaswa kuimarisha nguvu na uwezo wake wa ndani na moja ya njia za kujiimarisha huko ni kuwa na umoja na mshikamano na kushikamana vilivyo na masuala yanayowaunganisha Waislamu ambayo ni mengi sana.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia kuwa, ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa una kiu ya kupata uhakika wa Kiqur’ani na kuongeza kwamba: Hivi sasa ni tofauti kabisa na huko nyuma. Kwani huko nyuma shakhsia wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu walikuwa wakitumia misamiati ya kisoshalisti na kikomunusti kutangaza sauti yao ya kupigania haki na ukombozi, lakini hivi sasa kuanzia mashariki hadi magharibi mwa ulimwengu wa Kiislamu, wakati watu wanapoamua kupigania uadilifu na istiklali na uhuru na heshima, utawaona wanatumia kaulimbiu za Kiqur’ani katika harakati zao.

Vile vile amesema, kufanyika jalsa na mashindano ya Qur’ani Tukufu ni moja ya njia ya kuzidi kuzikurubisha nyoyo za watu kwenye uhakika halisi wa Qur’ani Tukufu na kuongeza kwamba: Kuenea na kusambaa maarifa ya Qur’ani kunaandaa uwanja wa kufikia kwenye usalama, amani na heshima na kupangilika vizuri maisha ya Waislamu chini ya kivuli cha mafundisho matukufu ya Qur’ani.

Mwanzoni mwa mkutano huo, Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala na Mkuu wa Taasisi ya Wakfu na Mambo ya Kheri nchini Iran ametoa ripoti fupi kuhusu juhudi zinazofanywa na taasisi yake kwa ajili ya kupanua wigo wa kufikisha kwa watu mafundisho ya Qur’ani kama ambavyo pia ametoa ripoti kuhusu mchakato wa kufanyika Mashindano ya Thelathini ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu, mjini Tehran.

Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi, ametaja baadhi ya sifa za kipekee zilizokuwemo kwenye mashindano hayo ya mwaka huu ya Qur’ani Tukufu kuwa ni kushiriki ndani yake maqarii, mahafidh na wahadhiri wa Qur’ani kutoka nchi 70 tofauti duniani.

Vile vile amesema: Taasisi ya Wakfu ya Iran katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita imekuwa na ratiba nyingi za kila namna kwa ajili ya kupanua na vile vile kunyanyua kiwango cha idadi na ubora wa kazi za masuala ya Qur’ani nchini Iran.
1239341
captcha