IQNA

Imam Khamenei: Matukio ya Palestina yanatia uchungu mno

7:54 - August 10, 2013
Habari ID: 2573226
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, matukio ya magharibi mwa Asia hususan Palestina na yale ya kaskazini mwa Afrika yanatia wasi wasi mno.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo Ijumaa hii katika hotuba ya Sala ya Eid ul Fitri hapa mjini Tehran na kusisitiza kwamba, matukio ya Palestina ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina, dhulma wanayotendewa na ukandamizaji wanaofanyiwa wananchi hao kila leo ni mambo yanayotia uchungu.
Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Kiislamu amesema, kubomolewa nyumba za Wapalestina, kutenganishwa watoto na wazazi wao na kuongezeka wafungwa wa Kipalestina katika magereza ya Wazayuni ni miongoni mwa masaibu na misiba ya Wapalestina; hata hivyo chungu zaidi ni himaya ya kila upande ya madola ya Magharibi kwa utawala haramu wa Israel unaotenda jinai kila leo dhidi ya Wapalestina.
Ayatullah Khamenei amesema, madola yanayodai kuwa watetezi wa haki za binadamu yamekuwa yakiunga mkono jinai za Wazayuni makatili. Kiongozi Muadhamu ameashiria matukio ya sasa ya Misri na kusema kwamba, kila siku uwezekano wa kutokea vita vya ndani nchini humo umekuwa ukiongezeka. Ameyaonya madola ya kibeberu na kuyataka yaache kuingilia masuala ya ndani ya Misri; kwani hatua yao hiyo ni kwa madhara kwa taifa la Misri.

Kwingineko Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa imani na umoja ndio chachu ya mapambano ya mataifa mbalimbali dhidi ya njama zinazofanywa na maadui.

Ayatullah Khamenei ambaye Ijumaa amehutubia Baraza la Idd lililohudhuriwa na viongozi wa nchi, mabalozi wa nchi za Kiislamu mjini Tehran na matabaka mbalimbali ya wananchi amewapongeza Waislamu kwa mnasaba wa sikukuu ya Idil Fitri na kusema, njia ya kutibu na kuondoa hitilafu zilizopo katika nchi za Kiislamu ikiwa ni pamoja na maeneo ya magharibi mwa Asia na kaskazini mwa Afrika ni mataifa ya maeneo hayo kuchukua uamuzi kwa kutumia hekima za tabala la wasomi, mwongozo wa vinara wao na wazee wenye busara, kusitisha uingiliaji wa kichochezi wa madola ya kigeni na uenezaji wa sumu ya unafiki na migawanyiko baina ya watu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, nchini Iran watu wenye madhehebu na kaumu mbalimbali wanaishi pamoja kwa amani na makundi ya kisiasa yanasonga mbele kwa umoja na mshikamano; kwa sababu hiyo njama za maadui za kutaka kuzusha hitilafu za kimadhehebu, kikaumu na kisiasa zimefeli mbele ya moyo wa imani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Hassan Rohani wa Jamhuri ya Kiislamu pia amewapa Waislamu wote duniani mkono wa kheri ya Idil Fitri na akasisitiza kuwa mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa umoja na kwamba mataifa yote yanapaswa kuimarisha mshikamano wao kutokana na ibada za mwezi huo uliomalizika.
1270487
captcha