IQNA

Ayatullah Ali Khamenei:

Moto wa makundi ya takfiri utawachoma hata waungaji mkono wao

19:46 - August 26, 2013
Habari ID: 2580669
Ayatullah Khamenei amesema kuwa moja ya masuala hatari sana katika eneo hili ni kuingizwa masuala ya kidini, kimadhehebu na kikaumu katika hitilafu za kisiasa za nchi mbalimbali. Ameongeza kuwa, inasikitisha kuona kwamba, nchi kadhaa za eneo hili zimesaidia kuanzisha kundi linalowakufurisha Waislamu linalopigana na makundi yote ya Waislamu, lakini waungaji mkono wa kundi hilo wanapaswa kuelewa kwamba, moto wake utawakumba wao pia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo alimkaribisha ofisini kwake Sultan Qaboos wa Oman na ujumbe anaoandamana nao hapa mjini Tehran. Ayatullah Khamenei ameashiria uhusiano mzuri na wa kirafiki wa Iran na Oman na kusisitiza kuwa, kuna uwanja mzuri wa kuimarishwa zaidi uhusiano wa nchi hizi mbili katika sekta mbalimbali hususan sekta ya gesi. Ameitaja Oman kuwa ni jirani mwema na halisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kuhusu masuala ya eneo la Mashariki ya Kati, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema eneo hili liko katika kipindi nyeti na hatari sana ambacho kinahitaji ushirikiano zaidi wa nchi hizi mbili.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa moja ya masuala hatari sana katika eneo hili ni kuingizwa masuala ya kidini, kimadhehebu na kikaumu katika hitilafu za kisiasa za nchi mbalimbali. Ameongeza kuwa, inasikitisha kuona kwamba, nchi kadhaa za eneo hili zimesaidia kuanzisha kundi linalowakufurisha Waislamu linalopigana na makundi yote ya Waislamu, lakini waungaji mkono wa kundi hilo wanapaswa kuelewa kwamba, moto wake utawakumba wao pia.
Amesisitiza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel pia ni tishio la kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati linaloungwa mkono na Marekani na kusema: Utawala fasidi wa Kizayuni ambao unamiliki maghala makubwa ya silaha hatari za mauaji ya umati ni tishio kubwa kwa eneo hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, eneo la Mashariki ya Kati linahitaji amani na usalama na lengo hilo muhimu litafikiwa kwa kutangazwa marufuku ya kweli ya silaha za mauaji ya halaiki katika eneo hili.
Katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Rais Hassan Rohani wa Iran, Sultan Qaboos bin Said wa Oman ameeleza kufurahishwa na kukutana kwake na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuutaja uhusiano wa Iran na Oman kuwa ni mzuri sana kutokana na mifungamano ya kihistoria na kiutamaduni ya pande hizo mbili. Sultan Qaboos amesema kwamba katika mazungumzo yake na Rais Hassan Rohani pande mbili zimechunguza nyanja za kupanua zaidi uhusiano katika sekta mbalimbali kama uchumi, usafirishaji na hasa sekta ya gesi. Sultan Qaboos ametilia mkazo maneno ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu hali myeti na hatari ya Mashariki ya Kati na tishio la utawala ghasibu wa Israel na akasema: Utatuzi wa hali ya sasa unalazimu kutilia maanani maslahi ya watu wa Mashariki ya Kati na ushirikiano wa nchi za eneo hilo. 1278343

captcha