IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Marekani ni sehemu ya matatizo ya Mashariki ya Kati

0:05 - November 02, 2015
Habari ID: 3432363
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa malengo ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati yanatofautiana kwa daraja 180 na ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na mabalozi wa Iran nje ya nchi. Amesema kuwa siasa za Marekani katika eneo nyeti la magharibi mwa Asia ndiyo sababu kuu ya hali mbaya ya sasa katika eneo hilo. Ameongeza kuwa kinyume na mitazamo ya baadhi ya watu ambao wanadai kuwa Marekani inajua njia ya utatuzi wa masuala ya eneo hili, nchi hiyo ndiyo sehemu kubwa ya matatizo ya Mashariki ya Kati.

Ayatullahil Udhma Ali Khamenei amesema kuwa sababu kuu ya ukosefu wa amani ni himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na makundi ya kigaidi; na kwamba siasa hizo zinatofautiana na zile za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa daraja 180.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amepinga suala la kufanya mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati na kusema, Wamarekani wanataka kutwisha maslahi yao na si kutatua matatizo yaliyopo, wanataka kutwisha asilimia 60 na 70 ya matakwa yao katika mazungumzo na kulazimisha malengo yao mengine kwa njia zisizo za kisheria; hivyo basi mazungumzo yana maana gani?

Ayatullah Khamenei amesema, siasa za nje za Iran ni siasa zilezile za mfumo na katiba na kuongeza kuwa, siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu zimechukuliwa katika Uislamu na katika malengo na thamani za Mapinduzi, na maafisa wa Wizara ya Mambo Nje na mabalozi kwa hakika ni wawakilishi, askari na wahudumu wa misingi na thamani hizo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya Mashariki ya Kati inakubaliwa na dunia na ni imara. Ameeleza njia za utatuzi za Iran kuhusu masuala hayo na kusema: Kuhusu kadhia ya Palestina, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbali na kupinga kabisa utawala ghasibu, bandia na wa Kizayuni na kulaani vikali maafa na jinai zinazofanywa kila siku na utawala huo, inapendekeza kufanyike uchaguzi utakaowashirikisha Wapalestina wote, na mtazamo huo unaoana kikamilifu na vigezo vya sasa vya dunia.

Kuhusu hali ya Syria, Ayatullahil Udhma Ali Khamenei amesema: Hakuna maana kwa nchi nyingine kukusanyika pamoja na kuchukua maamuzi kuhusu serikali na rais wa serikali ya nchi nyingine; huu ni uzushi hatari sana ambao hauwezi kukubaliwa na serikali yotote ile duniani.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, utatuzi wa kadhia ya Syria ni uchaguzi, na kazi hii inawezekana kwanza kwa kusitisha vita na kukomesha machafuko kwa njia ya kusitisha misaada ya kijeshi na kifedha kwa wapinzani wanaotumia silaha ili wananchi wa Syria wamchague mtu wanayemtaka katika mazingira ya amani na utulivu.

3428231

captcha