IQNA

Kuakisiwa barua ya Kiongozi Muadhamu kwa vijana wa Magharibi

19:57 - November 30, 2015
Habari ID: 3458797
Barua ya pili ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa vijana wa nchi za Magharibi imeakisiwa kwa wingi katika vyombo vya habari vya kigeni.

Vyombo hivyo vya habari vimetoa uchambuzi na kuzungumzia kwa mapana na marefu kuhusu sehemu mbalimbali za barua hiyo kama vile suala la ugaidi ambao ni tatizo la pamoja linalousumbua ulimwengu wa Kiislamu na Magharibi, siasa za kindumakuwili za Marekani kuhusu ugaidi, ulazima wa kupambana na fikra za utumiaji mabavu na ukatili, hujuma za majeshi ya Magharibi dhidi ya nchi za Kiislamu, umwagaji damu unaofanyika huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, unyama unaofanywa na kundi la kigaidi la Daesh katika nchi za Iraq na Syria na upinzani wa Kiongozi Muadhamu dhidi ya mashambulizi ya Paris ni baadhi ya sehemu za barua ya Kiongozi Muadhamu kwa vijana wa Magharibi zilizoakisiwa na kuchambuliwa na vyombo vya habari vya Magharibi.

Likizungumzia barua hiyo, shirika la habari la Ufaransa limeandika kuwa, katika barua yake kwa vijana wa Marekani na Ulaya, Kiongozi Mkuu wa Iran ameashiria mashambulizi ya kigaidi ya Paris na kulaani misimamo na siasa za kindumakuwili za nchi za Magharibi.

Shirika la habari la Assosiated Press kwa upande wake limeandika kuhusu barua hiyo ya Ayatullah Khamenei kwa vijana wa Magharibi kwamba: Kiongozi Mkuu wa Iran ameyataja mashambulizi ya kigaidi ya Paris kuwa ni ugaidi kipofu. Shirika hilo la habari limemnukuu Ayatullah Khamenei kwamba, anaumizwa sana na umwagaji damu unaotokea Palestina na ukatili wa kundi la Daesh huko Iraq, Syria na Lebanon.

Tovuti ya lugha ya Kifarsi ya shirika la BBC la Uingereza imeandika kuwa, katika barua yake ya pili kwa vijana wa Magharibi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka vijana wa Magharibi wajenge nguzo za kuamiliana kwa njia sahihi na kiungwana na ulimwengu wa Uislamu kwa msingi wa utambuzi sahihi na uoni mpana.    

Kanali ya televisheni ya al Mayadeen ya Lebanon pia imerusha hewani sehemu kubwa ya barua ya Kiongozi Muadhamu kwa vijana wa nchi za Magharibi na kumnukuu akisema: Waislamu bilioni moja na nusu duniani wamejitenga na kujiweka mbali na vitendo vya makundi ya kigaidi la kitakfiri na wanawachukia magaidi hao.

Kanali ya televisheni ya al Manar ya huko huko Lebanon pia imetangaza sehemu kubwa ya barua hiyo ya kihistoria baada tu ya kutangazwa na kuandika kuwa: Katika barua hiyo Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, ni watu wachache ambao hawajui kwamba Marekani ilikuwa na mchango mkubwa katika kuundwa na kuyasaidia kwa silaha makundi ya kigaidi kama Daesh, Taliban na al Qaida.

Kituo cha habari cha al Nashra kimenukuu sehemu ya barua ya Kiongozi Muadhamu kwa vijana wa Magharibi inayosema: Mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea Ufaransa ni sawa na yale yanayofanyika kwa miaka mingi sasa katika nchi za Syria, Iraq, Afghanistan na Yemen.

Chini ya kichwa cha habari: "Marekani Inaunga Mkono Ugaidi", tovuti ya gazeti la al Nahar la Lebanon imeandika kuwa kiongozi mkuu wa Iran amekosoa vikali siasa za kindumakuwili za Magharibi kuhusu ugaidi katika barua yake kwa vijana wa Ulaya na Marekani.

Jana tarehe 29 Novemba, tovuti ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ilichapisha barua hiyo ya kihistoria kwa vijana wa Magharibi na kuandika kuwa, sababu ya kuandikwa barua hiyo ni matukio machungu ya ugaidi kipofu ya Paris. Hiyo ni barua ya pili ya aina hiyo kuandikwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja. Januari mwaka huu pia Ayatullah Khamenei aliandika barua kama hiyo kwa vijana wa Ulaya na America ya Kaskazini kwa mnasaba wa mashambulizi yaliyolenga ofisi za jarida la kila wiki la Charlie Hebdo mjini Paris, Ufaransa na maeneo mengine kadhaa ya mji huo akiwataka vijana kutafakari kwa makini kuhusu masuala hayo.

3458625

captcha