IQNA

UN: Saudi Arabia inaua raia wasio na hatia nchini Yemen

17:59 - December 23, 2015
Habari ID: 3468864
Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen umetajwa kuwa unahusika moja kwa moja na mauaji ya raia wa nchi hiyo.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al-Hussein ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kwamba mashambulizi yanayofanywa na muungano unaoongozwa na Saudia huko Yemen yanalenga makazi ya raia. Zeid al Hussein ameongeza kuwa, anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa mashambulizi ya Saudi Arabia yanayolenga miundombinu kama mahospitali, shule na maeneo yenye makazi mengi ya raia wa Yemen tangu nchi hiyo ianzishe mashambulizi ya anga miezi tisa iliyopita. Ameongeza kuwa maelfu ya watu ambao nusu yao ni raia wa kawaida, wameuawa katika mashambulizi ya Saudia huko Yemen.

Wakati huo huo mwakilishi wa New Zealand katika Umoja wa Mataifa, Gerard van Bohemen amesema kuwa, hatua za kinyama zinazofanyika ndani na kandokando ya maeneo na makazi ya raia nchini Yemen ikiwa ni pamoja na utumiaji wa silaha nzito na mabomu ya vishada zimesababisha vifo vya raia wengi.

Sambamba na hayo shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeonesha ushahidi na nyaraka zinazofichua uhalifu wa Saudi Arabia nchini Yemen na kutangaza kuwa: Muungano unaoongozwa na nchi hiyo unalenga maeneo ya raia hususan katika mji mkuu wa Yemen, San'aa.

Tarehe 26 Machi mwaka huu Saudi Arabia na kwa kushirikiana na Marekani, ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya watu wa Yemen kwa lengo eti la kumrejesha madarakani kibaraka wake aliyejiuzulu na kutoroka nchi, Abd Rabbuh Mansur Hadi. Ndege za kivita za Saudia zimekuwa zikilenga taasisi za umma na miundombinu ya Yemen kama mahospitali, shule, madaraja, viwanda na maeneo ya ibada kama misikiti na kadhalika sambamba na kufanya mauaji ya umati dhidi ya raia hususan wanawake na watoto wadogo. Mashambulizi hayo yamesababisha mgogoro mkubwa na maafa ya kibinadamu. Mbali na hayo kwa sasa Saudia na waitifaki wake wanaizingira Yemen na wanazuia aina yoyote ya misaada ya kibinadamu kuingizwa nchini humo, mbinu ya kikatili ambayo imekuwa ikitumiwa kwa miaka kadhaa sasa na utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya raia wasio na hatia wa Ukanda wa Ghaza huko Palestina.

Yemen inashambuliwa na Saudia na waitifaki wake kwa ruhusa ya nchi za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu ambazo zinaendelea kuipatia Riyadh silaha za aina mbalimbali na kufumbia macho ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanyika huko Yemen. Utumiaji wa mabomu ya vishada kutoka nchi za Magharibi katika mashambulizi hayo ya Saudia dhidi ya raia wa Yemen unaonesha kuwa maslahi ya kiuchumi ya nchi hizo yanatangulizwa na kupewa umuhimu na nchi za Magharibi kuliko masuala ya haki za binadamu.

Nchi za Magharibi husasan Marekani, Uingereza na Ufaransa zinaiona Saudi Arabia kuwa ni soko kubwa la silaha zao na kila mwaka zinaiuzia nchi hiyo silaha za mabilioni ya dola, suala ambalo ndilo huwa kigezo cha mahusiano wa pande mbili. Mienendo ya nchi za Magharibi kuhusu utendani wa ndani na nje ya nchi wa serikali ya Saudia Arabia hususan mashambulizi ya utawala wa Riyadh dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen inathibitisha kwamba, haki za binadamu ni wenzo na fimbo inayotumiwa na nchi zinazodai kutetea haki hizo kwa ajili ya kufikia malengo yao ya kisiasa. Kwa mtazamo wa nchi za Magharibi, dola za mafuta kutoka Saudi Arabia hazipaswi kufungamanishwa na masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na waitifaki wao hata kama itakuwa kwa gharama ya maafa ya kibinadamu na kuuawa maelfu ya wanawake na watoto wadogo wasio na hatia yoyote katika nchi ya Waislamu wa Yemen.

3468240

Kishikizo: yemen raia mauaji saudia
captcha