IQNA

Waislamu Kenya wazuia magaidi wa Al Shabab kuua abiria Wakristo

18:08 - December 23, 2015
Habari ID: 3468865
Abiria Waislamu wamezuia kuuawa wenzao wa Kikristo huko Kenya katika shambulio la magaidi wakufurishaji wa al Shabab.

Imearifiwa kuwa katika tukio hilo la Jumatatu abiria Waislamu waliokuwa ndani ya basi huko kaskazini mashariki mwa Kenya walikataa kutii amri ya magaidi walioshambulia basi hilo ili kwa lengo la kuwatenganisha na kishwa kuwaua abiria wa dini ya Kikristo waliokuwa wakisafiri pamoja na Waislamu hao.
Shambulio hilo lilijiri katika kaunti ya Mandera  ambapo  watu waliokuwa na silaha wanaosadikiwa kuwa na uhusiano na kundi la al Shabab la Somalia walipolifyatulia risasi basi hilo lililokuwa na abiria 60 na kuua watu wawili.
Abdi Mohamud Abdi abiria Mwislamu aliyekuwa miongoni mwa watu waliokuwamo ndani ya basi hilo amesema kuwa, wanamgambo kumi waliiingia ndani ya basi hiyo na kuwataka abiria wa Kiislamu kujitenga na wale wa Kikristo, hata hivyo abiria Waislamu walikataa kutii amri ya wanamgambo hao.
Baadhi ya Waislamu ndani ya basi hilo walitoa hijabu zao na kuwapatia wale wasio Waislamu ili kuwasaidia kuficha utambulisho wao wakati basi liliposimama. Itakumbukwa kuwa, mwaka jana wanamgambo wa al Shabab waliokuwa na silaha waliwaua raia wasio Waislamu karibu 30 waliokuwa wakisafari kwa basi katika eneo hilo hilo.
Gavana wa Mandera Ali Roba amesema wakaazi Waislamu wa Mandera waliokuwa ndani ya basi hilo walikataa njama ya Al Shabab ya kuwatenganisha na wasiokuwa Waislamu. Gavana huyo amesema amepongeza hatua ya wakaazi wa eneo hilo kukabiliana na Al Shabab na kusema hiyo ndio sababu ya Waislamu kujeruhiwa walipokuwa wakijaribu kuwalinda wasio kuwa Waislamu.

Maimamu Kenya wawasifu waliowanusuru Wakristo

Wakati huo huo Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu nchini Kenya CIPK limepongeza kile walichokitaja kuwa kitendo cha ushujaa cha Waislamu kuzuia mauaji ya halaiki dhidi ya Wakristo katika kaunti ya Mandera hivi karibuni.

Katibu Mkuu wa baraza hilo Sheikh Khalifa Khamis amesema kitendo hicho kinadhihirisha wazi kuwa Uislamu na ugaidi ni mambo mawili tofauti na kwamba Uislamu unafundisha juu ya kumlinda jirani. Sheikh Khalifa amesema hatua ya Waislamu hao kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kuyalinda ya ndugu zao Wakristo ndio mafunzo sahihi ya Qurani tukufu inayosema kuiokoa nafsi moja ni kama kuuokoa ulimwengu mzima na kuiua nafsi moja isiyo na hatia ni kama kuuwa ulimwengu mzima. Itakumbuka kuwa, siku chache zilizopita, abiria Waislamu waliokuwa ndani ya basi moja katika kaunti ya Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya walikataa kutii amri ya wanamgambo wa al-Shabaab walioshambulia basi hilo na kuwataka kuwatambua abiria wa dini ya Kikristo waliokuwa wakisafiri pamoja na nao ili wawauwe


Magaidi wa Al Shabab wamekuwa wakitekeleza hujuma mara kwa mara nchini Kenya na kuwashambulia raia hasa maeneo ya kaskazini mashariki.

3468528

captcha