IQNA

18:56 - February 10, 2016
News ID: 3470127
Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya tarehe 11 Februari 1979 ulikuwa ni mwanzo wa kutokea mabadiliko makubwa katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kwa ujumla, kutokana na athari kubwa ya mapinduzi hayo kimataifa.

Hayo ni mapinduzi matukufu ambayo yalifanyika kwa kutegemea imani na itikadi za dini tukufu ya Kiislamu chini ya kaulimbiu ya "si Mashariki na si Magharibi" na kufanikiwa kuunda Jamhuri ya Kiislamu katika nchi hii baada ya kuuangusha utawala wa kiimla wa Shah. Mapinduzi ya Kiislamu ni moja ya matukio muhimu na makubwa sana katika karne ya hivi sasa na imekuwa na matunda mazuri mno ndani ya Iran na nje ya Iran.

Roger Garaudy, msomi Muislamu wa nchini Ufaransa aliandika makala kuhusiana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran akisema: Kwa kweli Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na Imam Khomeini (MA) hayafanani hata kidogo na mapinduzi yoyote mengine yaliyotokea huko nyuma. Katika kipindi chote cha historia, yamekuwepo mapinduzi ya kila namna yaliyofanyika kwa lengo la kubadilisha mfumo wa kisiasa katika nchi mbalimbali, lakini mapinduzi yote hayo hayafanani hata chembe na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Kumetokea pia mapinduzi ya kijamii duniani ya kuonesha hasira za watu masikini dhidi ya matajiri. Kumetokea pia mapinduzi ya kitaifa, ya wananchi ili kuonesha hasira zao dhidi ya wakoloni na watu waliopora ardhi zao. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran nayo yalikuwa na misukumo yote hiyo. Hata hivyo mapinduzi hayo, mbali na masuala tuliyoyataja, yamekuja na maana mpya na si kwamba yamepindua utawala wa kisiasa, kijamii na kikoloni tu, bali muhimu zaidi ni kuwa, yameupindua utamaduni na mtazamo maalumu uliokuwepo duniani kuhusiana na dini.

Miongoni mwa taathira za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kutia nguvu udugu wa Kiislamu na kuleta na kuimarisha mshikamano kati ya Waislamu. Mapinduzi hayo yalifufua hima ya kuzingatia mafundisho ya Qur'ani Tukufu na sira tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na kuweka msingi wa umoja wa Kiislamu na kuleta kigezo cha mshikamano na utangamano kati ya Waislamu.
Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, tangu awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitoa mwito kwa Waislamu wote duniani kuungana na kuwa kitu kimoja kwa ajili ya kukabiliana na watawala madikteta na maadui wa Uislamu. Alisisitiza mara nyingi kuwa siri ya kuweza mataifa ya Waislamu kurejesha heshima yao ni kufungamana na kuwa na kauli moja.
Katika moja ya matamshi yake, Imam Khomeini alisikika akisema: Enyi Waislamu duniani ambao mnauamini kikweli Uislamu! Simameni na muungane pamoja chini ya bendera ya tauhidi na chini ya kivuli cha mafundisho ya Uislamu ili kukata mikono ya madola ya kibeberu yanayopora utajiri wa nchi zenu na rejesheni heshima ya Uislamu kwa kujiweka mbali na mizozo na matamanio ya nafsi. Tambueni Waislamu kuwa nyinyi mna kila kitu.
Kuandaa mazingira mazuri ya kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu na kutayarisha uwanja wa kupatika umoja kati ya Waislamu kupitia kuasisi Jumuiya ya Kimataifa ya Kuyakurubisha Pamoja Madhehebu ya Kiislamu kupitia kupanua wigo wa welewa wa mafundisho ya kinadharia na kivitendo ya umoja na kuishi pamoja kwa salama Waislamu wote. Ni kwa kuzingatia malengo hayo ndio maana katika miaka ya awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikatangaza Wiki ya Umoja wa Kiislamu ambayo ni kipindi cha baina ya mwezi 12 hadi 17 Mfunguo Sita, kutokana na kuweko riwaya mbili tofauti kuhusu siku aliyozaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW. Kila mwaka, Iran inakuwa mwenyeji wa kongamano la umoja wa Kiislamu kwa mnasaba huo, kongamano ambalo linawakusanya pamoja maulamaa wa madhehebu yote ya Kiislamu kutoka maeneo tofauti duniani.

Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo msingi wake ni Qur'ani Tukufu na mafundisho sahihi ya Uislamu, imeiwadhifisha serikali kuhakikisha kuwa siasa zake kuu zinalenga kwenye kufanikisha umoja na mshikamano wa pande zote kati ya mataifa ya Waislamu.
Aya ya 92 ya Suratul Anbiyaa inasema: اِنَ هذِهِ اُمَتُکُم اُمَةً وَحِدَةً وَ اَنَا رَبُکُم فَاعبُدون Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi. Kwa mujibu wa aya hiyo tukufu, Waislamu wote ni umma mmoja, na ndio maana kifungu cha 11 cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kikasema wazi kwamba serikali ya Iran ina jukumu la kuhakikisha kuwa siasa zake kuu zinasimama juu ya msingi wa kuleta mfungamano na mshikamano baina ya mataifa yote ya Waislamu na ihakikishe kuwa umoja wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni unapatikana katika ulimwengu wa Kiislamu.
Imam Khomeini tangu katika miaka ya mwanzoni kabisa mwa Mapinduzi ya Kiislamu, siku zote alikuwa akisisitizia suala la kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu na kuleta umoja baina ya Waislamu. Alikuwa akiwataka Waislamu watumie vizuri ibada tukufu ya Hija kuimarisha umoja baina yao.
Kiongozi huyo mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema katika ujumbe wake mmoja wa Hija kwamba: Tukiwa tumekaribia kuingia katika fursa ya kuzidi kukurubiana zaidi Waislamu wote duniani na kupatikana maelewano baina ya madhehebu yote ya Kiislamu kwa ajili ya kuzipapatua nchi za Waislamu kutoka kwenye makucha machafu ya madola ya kibeberu na katika wakati huu wa kukaribia kukatwa mikono ya mabeberu wa Mashariki na Magharibi nchini Iran kwa kutumia nembo ya kuwa na kauli moja na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Mkubwa na kukusanyika pamoja Waislamu chini ya bendera ya Uislamu na tauhidi, tunaona shetani mkubwa amekusanya vifaranga vyake ili vitumie kila hila inayojulikana, kuzusha mizozo baina ya Waislamu na kuutumbukiza kwenye mifarakano umma wa tawhidi ambao watu wake ni ndugu katika imani ili kwa njia hiyo waweze kufungua milango ya kufanya ubeberu wao.
Stratijia na mkakati wa kukusanyika pamoja kwenye mhimili wa umma mmoja wa Kiislamu una nafasi ya kipekee katika fikra za kisiasa na kidini za Imam Khomeini MA. Mfungamano thabiti, wa kina na wa pande zote za kiitikadi na kidini kati ya harakati mbalimbali za Kiislamu ulimfanya Imam Khomeini MA apiganie mno ufanikishaji wa umma mmoja wa Kiislamu na ndio maana aliyaunganisha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na harakati nyinginezo za Kiislamu duniani na alisisitiza mara zote kuwa, kufanikisha jambo hilo ndiyo stratijia na njia bora kabisa ya kupambana na mabeberu wa dunia na kuwashinda. Katika sehemu moja ya matamshi yake muhimu sana alisema: "Sisi tumejiandaa kuulinda Uislamu na mataifa ya Waislamu ya kupigania ukombozi wa mataifa hayo. Mpango wetu ambao ndio mpango wa Uislamu ni kuwafanya Waislamu kuwa na kauli moja na kuyaungangisha mataifa ya Waislamu. Lengo letu ni kuleta udugu baina ya makundi yote ya Waislamu katika kila kona ya dunia na kuwa pamoja na madola yote ya Kiislamu ulimwenguni. Na huo ndio msimamo wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya kwamba mwamko wa Kiislamu wa nchini Iran si kitu kinachohusiana na Iran tu, bali ni tukio linalohusu pia nje ya Iran na nje kabisa ya eneo hili.”

Amma kuhusiana na umuhimu wa umoja katika umma wa Kiislamu na taathira zake katika kuundwa serikali ya Kiislamu, Imam Khomeini MA alikuwa anaamini kuwa, kuundwa serikali hiyo kunapaswa kuwe ni kwa ajili ya kuulinda mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuleta umoja baina ya Waislamu. Moja ya misingi mikuu ya siasa za ndani na nje za Jamhuri ya Kiislamu ni kusisitizia umoja na mshikamano baina ya Waislamu. Kuwalinda na kuwatetea Waislamu duniani ni miongoni mwa misingi mikuu ya siasa za mambo ya nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Katiba.

Stratijia ya kuhimiza mno suala la umoja wa Kiislamu imeendelezwa na Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyechukua nafasi ya Imam Khomeini MA. Katika moja ya hotuba zake mbele ya maulamaa wa Kisuni na Kishia katika mji wa Kermanshah, wa magharibi mwa Iran alisema: Tunapozungumzia umoja hatuna maana kwamba madhehebu yote ya Waislamu yaache imani na itikadi zao na kuunda madhehebu mengine mapya, kwani jambo hilo haliyumkiniki, bali makusudio yetu kuhusu umoja ni kuwa kila madhehebu yabakie na imani na itikadi zake lakini pia yawe na uvumilivu na yaishi kwa salama na watu wa madhebu mengine na kutoruhusu taasubu za kimadhehebu ziwasahaulishe Waislamu mambo mengi yanayowaunganisha na mwishowe kuzusha vita na mapigano baina yao. Qur'ani Tukufu inasema: وَلاَ تَنَازَعُواْ فَتَفْشَلُواْ وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ وَاصْبِرُواْ إِنَّ اللّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ Wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri.

Ayatullah Khamenei analielewa vizuri jambo hilo kama ambavyo anatambua vyema hali ilivyo duniani leo na stratijia za madola ya Magharibi na hasa Marekani ambayo lengo lao kuu ni kuzusha mizozo na mifarakano baina ya Waislamu wa madhehebu mbalimbali, na kuonesha sura potofu na ya kichochozi dhidi ya Uislamu. Kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, njia ya kimsingi ya kukabiliana na stratijia ya kuzusha mifarakano kati ya Waislamu, ni kuhakikisha Waislamu wa madhehebu yote wanakuwa na mazungumzo ya pamoja na kuhimiza umoja baina yao pamoja na kujiweka mbali na kila aina ya chuki na taasubu za kimadhehebu.
Jambo la kusikitisha ni kuona kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumezuka makundi ya kigaidi yanayomkufurisha kila asiyekubaliana na fikra zao, na hivyo kuwa balaa kwa ulimwengu wa Kiislamu. Makundi hayo yanafanya vitendo vya kikatili vizivyokubaliana hata kidogo na mafundisho ya Uislamu vitendo ambavyo si tu havina nafasi katika historia ya Uislamu, bali utamaduni wa Kiislamu nao uko mbali kabisa na vitendo vya makundi hayo na ndio maana Waislamu wamesimama kukabiliana nayo.
Wakati wa Bwana Mtume Muhammad (rehema za Allah ziwe juu yake na Aal zake), jambo hilo halikuwepo kabisa na hakuna Muislamu yeyote aliyethubutu kumwita kafiri Muislamu mwenzake. Mafundisho ya madhehebu yote ya Waislamu nayo yanapinga vikali kitendo cha makundi hayo cha kuwaita makafiri Waislamu wa madhehebu mengine au kuvihusisha na dini ya Kiislamu vitendo vya kikatili vinavyofanywa na magenge hayo yaliyo dhidi ya Uislamu.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu azilainishe nyoyo za Waislamu wa madhehebu yote na kuzifanya zishikamane na mafundisho ya dini yao inayohimiza umoja na mshikamano baina ya Waislamu wote.


3474716
Name:
Email:
* Comment: