IQNA

Mamillioni waadhimisha miaka 37 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

0:49 - February 12, 2016
Habari ID: 3470129
Madhimisho ya mamilioni ya watu ya miaka 37 ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, yamefanyika leo kwa mafanikio makubwa mjini Tehran na katika zaidi ya miji 1000, mikoa, wilaya na kata na katika zaidi ya vijiji 4000 ndani ya Iran.
Tarehe 22 Bahman, Hijria Shamsia inayosadifiana na Februari 11 kila mwaka, huwa ni siku ya kufikia kileleni sherehe za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Tarehe 11 Februari 1979, sawa na tarehe 22 Bahman mwaka 1357 Hijiria Shamsia, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakiongozwa na Imam Khomein (MA) mwasisi mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yalifanikiwa kuupindua utawala kibaraka wa Kipahlavi. Katika maadhimisho ya leo, mamilioni ya wananchi waliokuwa wameshika picha za Imam Ruhullah Khomeini (MA) na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, wametoa nara za 'Kifo kwa Marekani' 'Kifo kwa Israel' 'Kifo kwa utawala wa Aal Saud' na 'Labbaika yaa Khamenei', na kwa mara nyingine wametangaza utiifu wao kwa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu na kwa Imam Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Zaidi ya wandishi wa habari 5200 wa ndani na nje ya Iran walikuwepo kuripoti maadhimisho ya leo hapa nchini. Aidha zaidi ya wageni 450 kutoka nchi 28 wakiwemo shakhsia wa kielimu, kisiasa na viongozi wa ngazi za juu wa nchi za Ulaya, Afrika, Asia na Marekani, walihudhuria katika shere hizo ambazo zimefana sana. Baada ya maandamano ya kuadhimisha Mapinduzi ya Kiislamu, waandamanaji wamesoma azimio lao la siku ya Mwenyezi Mungu ya 22 Bahman hapa mjini Tehran. Katika azimio hilo, waandamanaji wameyataja mafanikio na uwezo wa Iran ya Kiislamu katika sekta ya ulinzi hususan uwezo wa makombora, kuwa ni mambo ambayo ni haki ya wazi ya Iran na hayafai hata kujadiliwa. Aidha wameyaonya madola ya kibeberu kuwa endapo yatajaribu kuidhoofisha au kuitisha Iran, basi taifa la Iran kwa msaada wa vikosi vyake vya ulinzi litatoa majibu makali mno kwa aui atakaeleta chokochoko zozote zile.
Katika maadhimisho hayo Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amehutubia umati mkubwa uliokusanyika kwenye uwanja wa Azadi hapa Tehran na sambamba na kuashiria kupanuliwa wigo wa makubaliano baina ya Iran na Russia, China na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuwa na ushirikiano wa pamoja wa muda mrefu, amesema kuwa, dunia ya leo imetambua kuwa, kipindi cha kutumia lugha ya vikwazo na kulivunjia heshima taifa la Iran kimepita na kwamba sasa umewadia wakati wa kuzungumza na Iran ya Kiislamu kwa lugha ya heshima na busara. Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais Rouhani amesema kuwa, Wairani ni watu wa amani na usalama katika eneo hili na dunia nzima kwa ujumla.
3474869
captcha