Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei katika
mazungumzo hayo na Rais Johann Schneider-Ammann wa Uswisi aliashiria historia
ya uhusiano wa nchi hizo mbili na taswira nzuri ya mwenendo wa Uswisi katika
fikra za Wairani na amekaribisha suala la kuzidishwa ushirikiano wa kiuchumi na
kielimu wa pande mbili. Amesema kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya
Iran na Uswisi ni kidogo na hakina mlingano, na kusisitiza kwamba,
wafanyabiashara na wawekezaji wa Uswisi wanaweza kuboresha mizani hiyo kwa
kuelewa vyema uwezo mkubwa wa Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema historia ya Uswisi ya kutojiunga na
mashinikizo na vikwazo vya baadhi ya nchi za Magharibi dhidi ya Iran ni
miongoni mwa nyanja nzuri za kiutamaduni kwa ajili ya kuzidisha ushirikiano wa
pande hizo mbili. Ameongeza kuwa: "Tangu awali sisi tunaitambua Uswisi kuwa ni
kituo cha amani, urafiki na ushirikiano lakini baadhi ya nchi za Ulaya hazina
sifa hizo na zinayaona maslahi yao katika kuanzisha vita na kochochea
hitilafu”.
"Tunaitambua Uswisi kuwa ni kituo cha
amani, urafiki na ushirikiano lakini baadhi ya nchi za Ulaya hazina sifa hizo
na zinayaona maslahi yao katika kuanzisha vita na kochochea hitilafu”.
Ameashiria pia tajiriba ya wananchi wa Iran kuhusu hatua ya baadhi ya nchi za
Ulaya ya kuchochea vita ikiwa ni pamoja na kuupatia utawala wa Saddam Hussein
makombora na ndege za kivita wakati wa vita vilivyoanzishwa na utawala huo
dhidi ya Iran na akasema: Mwenendo huo umejenga taswira hasi katika fikra za
wananchi wa Iran lakini taswira kama hiyo haiko hapa nchini kuhusu Uswisi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, serikali ya Jamhuri ya
Kiislamu inaunga mkono kikamilifu mahusiano ya kiuchumi na dhamana ya kisheria
ya makubaliano ya Iran na Uswisi na kuongeza kuwa, jambo muhimu ni kuona
makubaliano hayo yakitekelezwa kivitendo kwa ushirikiano halisi, azma na irada
thabiti.
Katika mkutano huo ambao pia umehudhuriwa na Rais Hassan Rouhani, Rais Johann
Schneider-Ammann wa Uswisi ameeleza kufurahishwa kwake na safari yake hapa
nchini na kuashiria historia ya miaka mingi ya uhusiano wa kirafiki wa nchi
yake na Iran. Amesema: "Ni fahari kwetu sisi kuwa hapa Iran na tunashuhudia
harakati inayosonga mbele ya uhusiano wa nchi hizi mbili”.
Bwana Johann Schneider-Ammann amesema kuwa anaandamana na ujumbe mbili za
kielimu na kiuchumi hapa nchini na kuongeza kuwa, katika safari yake mjini
Tehran kumejadiliwa ramani ya njia ya ushirikiano mpana zaidi na wa nyanja
mbalimbali kati ya Iran na Uswsi na kwamba, kutiwa saini ramani hiyo ya njia
kunaweza kupeleka kupanuliwa zaidi uhusiano wa pande mbili.
Rais wa Uswisi amegusia pia changamoto kubwa zilizopo duniani na kusema: Athari
za mtikisiko na changamoto hizo zimefika hata Ulaya na kandokando ya Uswisi na
kunahitaji ushirikiano kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hizo.