IQNA

21:13 - April 20, 2016
News ID: 3470259
Tarehe 13 Rajab inasadifiana na siku ya kuzaliwa Amirul Muuminiin Ali bin Abi Talib AS mmoja kati ya Watu wa Nyumba tukufu ya Mtume Muhammad SAW.

Amani iwe juu ya mzaliwa ambaye, Mwenyezi Mungu amejaalia Nyumba yake yaani al Kaaba, kuwa ni mahala pake pa kuzaliwa na kupata malezi kutoka kwa Mtume Muhammad SAW, ambaye ni mbora wa Mitume wote, ili kigezo chake hicho kamili kiweze kumjenga mwanadamu na kuifungua milango ya rehema za Allah kwa waja wake.

Wakati Ali AS alipozaliwa, umri wa Bwana Mtume SAW haukuwa umepindukia miaka thelathini. Miaka michache baadaye, Mtukufu huyo alitoa shauri kwa Ami yake Abu Talib la kumsaidia ulezi wa Ali kutokana na aila na familia kubwa aliyokuwa nayo ami yake huyo, ili kumpunguzia mzigo mzito wa gharama za kukidhi mahitaji ya familia yake. Abu Talib aliafiki ushauri huo, na kuanzia kipindi cha utoto wake, Ali AS akawa pamoja na Bwana Mtume. Ali alikuwa mwanaumme wa kwanza kumwamini Bwana Mtume SAW. Alikuwa mpwekeshaji wa Allah tangu udogoni mwake na hakuwahi hata mara moja kuabudu masanamu kama walivyokuwa watu wengine wa zama hizo.

Mtume Mtukufu Muhammad SAW wakati aliposikia habari za kuzaliwa binamu yake huyo alisema; 'Mwenyezi Mungu SW amefungua milango ya rehema kwa waja Wake, kutokana na baraka za mazazi ya mtukufu huyu'. Allamah Shahidi Murtadha Motahhari anasema: 'Kama Ali tumemkubali kuwa ni kigezo, ruwaza na Imamu wetu, basi bila shaka kiongozi huyo ni mwanadamu kamili, mwenye mlingano na mtu ambaye amekusanya thamani zote za kibinadamu kwa mlingano uliokuwa sawa".

Moja kati ya mambo yaliyokuwa yakisisitizwa mno na Imam Ali AS wakati wa uhai wake na hasa katika kipindi kifupi cha utawala wake, lilikuwa ni suala la kuchungwa haki za binadamu. Leo hii tunakusudia kuzungumzia kwa mukhtasari tu kuhusiana na maudhui ya haki za binadamu za Kiislamu katika utawala wa Imam Ali AS.

Leo hii ulimwengu umegubikwa na vita na vitendo vya umwagaji mkubwa wa damu, jambo ambalo linatushawishi kuliangalia kwa makini suala la haki za binadamu, ili utukufu na maisha ya mwanadamu yaweze kuhifadhiwa kwenye tangazo la kimataifa la kuchunga haki za binadamu. Hata hivyo, tangazo hilo lina mapungufu mengi na wala halitekelezwi ipasavyo kutokana na ukomo na kukubali makosa akili ya wanadamu.

Kwa upande mwingine, ni wazi kwamba Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo, anajua zaidi siri alizonazo mwanadamu kuliko yeyote yule na anajua pia mahitaji na nguvu zake, kwani Yeye ndiye anayejua maisha na utukufu huu aliompa mwanadamu ataweza kuuhifadhi kwa kutumia njia zipi na kwa namna gani. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameteremsha haki za kimsingi za mwanadamu katika njia iliyokamilika kabisa kupitia njia ya Wahyi aliyomteremshia Mtume Muhammad SAW; na Mtume Mtukufu pamoja na Ahlul Bayt zake Alayhimus Salaam wakachukua jukumu la kuwabainishia wanadamu. Kipindi kifupi tu cha utawala wa Imam Ali AS na mbinu alizozitumia mtukufu huyo wakati wa utawala wake, zinaweza kuwa kigezo cha kivitendo cha masuala ya haki za binadamu za Kiislamu kuliko zama nyingine, kwani katika kipindi hicho Uislamu uliimarika katika maeneo mbalimbali, na watu kutoka makabila, lugha na rangi mbalimbali wakaifuata dini ya haki ya Kiislamu. Kwa utaratibu huo, mbinu ya kivitendo iliyokuwa imejikita kwa kiongozi huyo mwadilifu, ilitoa taswira ya kuwepo chimbuko la haki za binadamu za Kiislamu.

Kwa mtazamo wa haki za binadamu za Kiislamu, hauwezi kudhaminiwa utukufu wa mwanadamu, bila ya kuzingatiwa misingi miwili muhimu ambayo ni 'kudumu' na 'kumtafuta Allah'. Dhati ya mwanadamu ni kumuomba Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu SW pia humzingatia na kumuangalia mja Wake na kumpatia rehema Zake. Hivyo, mwanadamu katika mtazamo wa Kiislamu, sio kiumbe asiyekuwa na malengo na mwenye kutangatanga tu, bali ni kiumbe mwenye shauku na raghba ya kumfikia Mwenyezi Mungu SW. Bila shaka matini na makubaliano ya kisheria yanapasa kufungamana kikamilifu na moyo wa kumpenda Allah SW. Suala hili linajitokeza katika hali ambayo, haki za binadamu kwa mtazamo wa Wamagharibi, zinamuwezesha mwanadamu kufanya jambo lolote lile alitakalo, bila ya kumzingatia Mwenyezi Mungu. Amma kwa mtazamo wa dini tukufu ya Kiislamu, nguzo na mhimili ni Mwenyezi Mungu.

Imam Ali AS amesema hivi kwenye wasia aliompa mwanawe Imam Hassan AS: 'Tambua kwamba wewe umeumbwa kwa ajili ya ulimwengu wa akhera na wala si kwa ajili ya ulimwengu huu, na wala hautaishi milele kwenye ulimwengu huu bali kwa siku chache tu na kisha utaelekea kwenye ulimwengu wa akhera. Kwa hiyo, jipinde katika kufanya mema duniani na wala usiuze akhera yako kwa ajili ya dunia hii".

Kuna aya nyingi katika Qurani Tukufu ambazo zinaeleza kuwa, maisha ya hapa duniani ni ya kupita tu na kwamba maisha ya milele yako katika ulimwengu wa akhera na kumtahadhirisha mwanadamu kwamba, nyendo zake njema katika ulimwengu huu zitampatia maisha ya saada na utukufu huko akhera.

Kwa minajili hiyo mpenzi msikilizaji, wakati tunapozungumzia masuala ya haki za binadamu, lazima haki hizo ziwe zinadhamini utukufu wa mwanadamu hapa duniani na kudhamini pia saada ya milele ya huko akhera, ambapo jambo hilo haliwezi kupatikana isipokuwa kwa kutii na kutekeleza mafundisho sahihi ya Kiislamu na kuwa mnyenyekevu mbele ya Allah SW. Amma haki za binadamu ambazo hivi sasa zinanukuliwa na vyombo vya kisiasa na kutumiwa kama kisingizio kwa lengo la kufikiwa malengo yao haramu, hazina sifa hizo maalumu na bora za dini tukufu ya Kiislamu.

Tumeangazia misingi ya haki za binadamu za Kiislamu na sasa tutaelezea mifano yake. Imam Ali AS amelitilia umuhimu mkubwa suala hilo kwenye hotuba zake na hata alikuwa akiwafundisha watu wake juu kuheshimu na kuchunga haki hizo na kuzitekeleza kikamilifu sheria na hukumu hizo. Umuhimu wa haki ya kuishi kwenye fikra ya Imam Ali AS ilikuwa na nafasi muhimu na hata kwenye amri mashuhuri aliyoitoa wakati wa utawala wake na kumpa Malik Ashtar alisema: 'Jiepushe na kumwaga damu zisizokuwa na makosa, kwani jambo hilo la kumwaga damu bila ya hatia hupelekea mtu kushtakiwa, jambo hilo ni dhambi kubwa na huondosha neema na hupunguza umri wa mtu'.

Katika dini tukufu ya Kiislamu, muumini yeyote anaheshimiwa kutokana na imani yake na asiyekuwa muumini pia anapasa kupewa heshima yake kwa vile ni mwanadamu na mwenye haki ya kuishi.

Uhuru ni kitu ambacho kila mwanadamu anapasa kuwa nacho, lakini wengine hulitumia jambo hilo vibaya na kimakosa; badala ya kumpa mwanadamu heshima yake ipasavyo humdhalilisha na kumdunisha. Ni wazi kuwa, wanafikra na watu wenye akili timamu wanabainisha maana ya uhuru kwamba, sio hali ya mtu kujiachilia na kufanya jambo lolote alitakalo bila ya kuwepo mipaka na masharti kama wanavyofanya wanyama. Kwa mfano, hakuna uhuru wa kuwadhuru au kuwaibia watu wengine, bali uhuru ni ule wenye mipaka na masharti maalumu. Mipaka hiyo katika dini ya Kiislamu imewekwa na Mola Muumba.

Imam Ali bin Abi Talib AS alikuwa akiwahabarisha watu uhuru wa aina hiyo wakati alipokuwa akihutubia msikitini, na wapinzani wake walikuwa wakimkosoa na hata baadhi ya wakati walikuwa wakivuruga hotuba zake. Imam AS hakuwa akitoa nara tupu kuhusiana na uhuru, bali alikuwa akiutekeleza kivitendo kwa lengo la kujenga misingi imara ya kijamii kwa namna ambayo watu walipata moyo na ari kubwa na hata kumshangilia kwa kumuona kuwa ni kigezo kamili cha mwanadamu.

Msingi mwingine wa haki za binadamu, ni kuwepo usawa kati ya wanadamu. Bila shaka msingi huo umekubalika katika dini ya Kiislamu na wala sio wenye kukinzana na msingi mwingine muhimu uitwao uadilifu. Kwani uadilifu maana yake ni kutoa haki kwa mtu yeyote kwa kile anachostahiki, katika hali ambayo usawa unaweza kupatikana pasipokuwa na uadilifu ndani yake.

Maarifa na elimu kubwa ya Ali bin Abi Twalib AS kuhusu Mwenyezi Mungu SW ndio chanzo cha upendo na hisi yake ya kupigania uadilifu na haki. Aliitambua vyema nafsi yake na huu ulikuwa msingi wa maarifa aali yaani kumjua Mola Muumba na mkamilifu mutlaki. Ali AS alikuwa akisema: "Dunia na vilivyomo haviwezi kufikia nafasi aali ya mwanadamu, na hadhi ya mwanadamu iko juu kiasi kwamba haiwezi kuuzwa kwa thamani ya dunia, kwani dunia ni wenzo na chombo cha kutumia kwa ajili ya kufikia makazi halisi ya mwanadamu." Imam AS alikuwa akisema: "Sikuona kitu chochote ila nilimuona Mwenyezi Mungu kabla yake, baada yake na pamoja nacho."

Katika sira na nyendo za Imam Ali AS na hata wakati wa uongozi wake, kumeshuhudiwa ushahidi mwingi unaoonyesha kwamba, mtukufu huyo pamoja na kukabiliana na matatizo na mushkeli mwingi, hakuwa tayari kukiuka misingi ya uadilifu na usawa na daima alikuwa akihifadhi na kusimamisha misingi hiyo ya haki hadi kufikia hatua ya kuhatarisha na kujitolea muhanga maisha yake. Iwapo tutaangalia kwa makini amri aliyompa Malik Ashtar tutaona kwamba, Imam Ali AS alikuwa akichunga misingi ya haki za binadamu bila ya kutofautisha watu kutokana na mtazamo wao wa kiutaifa, kikabila, kimatabaka, rangi na mengineyo, na miongoni mwa mambo hayo ni ugawaji wa Baitul Maal na utekelezaji wa sheria. Kwa mfano, baadhi ya watu katika zama zake walimtaka Imam Ali AS apewe hisa nyingi zaidi ya Baitul Maal kutokana na ukuruba aliokuwa nao kwa Mtume Mtukufu Muhammad SAW, lakini Imam Ali AS aliwajibu watu hao kwa kusema; 'Jueni kwamba kila mtu miongoni mwa Muhajirina na Ansar ni miongoni mwa masahaba wa Mtume SAW, na jueni kwamba yeye mwenyewe ni mbora, na fahamuni kwamba ubora ulio wazi uko kesho Siku ya Kiyama mbele ya Mwenyezi Mungu na zawadi ya amali hizo itatolewa na Yeye mwenyewe. Hivyo nyinyi ni waja wa Mwenyezi Mungu SW na mali ni mali ya Mwenyezi Mungu, ambayo ninaigawanya kwenu kwa usawa na hakuna mtu yeyote aliye mbora mbele ya mwenzake. Iwe ni waarabu au waajemi, kesho Siku ya Kiyama watapata malipo na kile kilicho bora mbele ya Allah.'

Kisa kingine ambacho kilitokea katika maisha ya Imam Ali AS kinaonyesha kwamba, mtukufu huyo alikuwa mwadilifu na msawa hata katika kuchunga haki za wafuasi wa dini za wachache. Mwanamume mmoja wa Kiyahudi aliiba deraya la Imam Ali AS na kulipeleka sokoni ili aliuze. Imam AS wakati alipoliona deraya hilo alilitambua kuwa ni lake na kumtaka Myahudi amrejeshee, ingawa Myahudi huyo alikataa katakata kulirejesha. Hivyo shauri hilo likapelekwa mahakamani. Ijapokuwa Imam Ali AS wakati huo alikuwa mtawala wa umma wa Kiislamu, alihudhuria mahakamani kama mtu wa kawaida. Jambo la kushangaza ni hili kwamba, Imam AS hakuwa na ushahidi wa kutosha wa kuweza kuutoa mahakamani ili apewe vazi lake, hivyo hakimu alitoa hukumu ya kumpa ushindi Myahudi, na Imam AS alikubaliana na hukumu hiyo. Lakini Myahudi yule aliamua kusilimu na kuingia katika dini ya Kiislamu, baada ya kumuona Amirul Muuminiin akikubali na kuheshimu hukumu iliyotolewa mahakamani, licha ya kujua wazi kwamba vazi lile lilikuwa ni haki na mali yake. Haki ya binadamu ya Kiislamu ambayo ilikuwa ikifungamana na Imam Ali AS hadi mwisho wa uhai wake, imeweza kutoa taswira na taathira kubwa kama hizo katika jamii.

3490560

Name:
Email:
* Comment: