Alikuwa anapitisha mwaka wa arobaini wa umri wake na katika miaka
yote hiyo watu walikuwa wakimpongeza kwa ubora wa tabia na uaminifu wake.
Pango la Hiraa lilikuwa mahala ambapo Muhammad alikuwa akitulia kiroho. Katika
sehemu hii alikuwa akipitisha baadhi ya siku akiwa amezama katika ibada na
kutafakari. Kila alipokuwa akimaliza ibada zake hapo alikuwa akielekea katika
Kaaba na kutufu.
Wakati Mtume SAW alipokaribia miaka 40, alikithirisha ibada na itikafu. Sijda
zake zilikuwa ndefu zaidi, minong'ono yake na Mola wake iliongezeka na kuzama
katika kina kirefu zaidi wakati wa kutafakari. Kwa kweli alikuwa na hali
tafauti kabisa kimaanawi. Mahaba na mapenzi ya Mohammad SAW kwa Mwenyezi Mungu
yalikuwa makubwa sana kiasi cha yeye kustahiki kupokea Wahyi.
'Soma kwa Jina la Mola Wako Mlezi aliyeumba'
Muhammad SAW katika hizo lahadha zilizojaa nuru, alisikia sauti wakati akiwa
amezama katika hali ya kumuabudu Mola wake. Sauti hiyo ilimuamrisha asome.
Jibril, Malaika wa Wahyi alikuwa ameamurishwa kumpa Muhammad ujumbe muhimu.
Alimwambia, 'Ewe Mohammad! Soma.' Muhammad ambaye alikuwa hajui kusoma, huku
akiwa ameshangaa sana aliuliza: ‘Nisome nini? Sijui kusoma. Kwa mara nyingine
Jibril alirudia na kusema: 'Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba,
Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu
kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa
hayajui.' (Surat al A'laq aya ya 1-5)
Muhammad hapo alifahamu kuwa alikuwa ameteuliwa kwa amri ya Mwenyezi Mungu
kuwaongoza wanaadamu kwa kueneza ujumbe Wake. Hivi sasa imepita zaidi ya miaka
1400 tokea lijiri tukio hilo ambalo lilikuwa nukta adhimu katika historia ya
mwanaadamu. Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za kheri na fanaka kwa
mnasaba wa kumbukumbu ya kubaathiwa Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW na
tunawakarisbisha kusikia machache tuliyowaandalia kwa munasaba huu.
Mwenyezi Mungu SWT katika aya ya pili ya Surat al Jumua anasema: Yeye ndiye
aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na
awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa
katika upotofu ulio dhaahiri.
Nukta ya kwanza ya ayah hii inahusu kusoma aya za Mwenyezi Mungu. Kwa kusoma
aya za Mwenyezi Mungu na kuwajulisha watu kuhusu aya hizi, Mtume wa Uislamu SAW
alikuwa anaandaa mazingira ya kuwafundisha.
Emile Dermenghem, mtaalamu wa masuala ya Mashariki na mwandishi Mfaransa
anasema hivi kuhusu nukta hii: ‘Sheria muhimu zaidi ya mabadiliko na mafundisho
ni ule ukweli ambao ulikuja kwa jina la Wahyi na hatua kwa hatua kumteremkia
Mohammad SAW na leo miongoni mwa wanaadamu jina lake ni Qur'ani.'
Mohammad SAW, mkamilishaji maadili mema
Moja kati ya hatua muhimu zaidi zilizochukuliwa na Mtume wa Uislamu SAW ni
kuwalea wanaadamu.
Malezi haya yanamaanisha kuandaliwa mazingira ya kunawirisha vipawa vya
mwanaadamu katika njia inayofaa.
Jitihada zote za Mtume SAW zilielekezwa katika kuandaa mazingira ya uhusiano
bora baina ya mwanaadamu na Allah SWT na halikadhalika na wanaadamu wenzake.
Ili kufikia lengo hili, kulikuwa na ulazima wa kuisafisha nafsi ya mwanaadamu
ili kuitayarisha kupokea ukweli bora zaidi.
Katika Qur'ani Tukufu amali hii imetajwa kuwa ni Tazkiyatun Nafs kwa maana ya
kulea vizuri na utakasaji unaojumuisha kuwa mtakasifu kwa mtazamo wa kiitikadi,
kiakhlaqi na kitabia.
Umuhimu wa akhlaqi au maadili mema na Tazkiyatun Nafs ni mambo ambayo
hayajafichika kwa yeyote na jamii mbali mbali zinayahitaji hayo. Hii ni kwa
sababu njia ya kuokoka kutoka upotofu, ufisadi, ujahili, vita na umwagaji damu
ni kupitia kujipamba kwa thamani na maadili bora.
Mtume Mtukufu SAW alisema lengo la kubaathiwa na kutumwa kwake ni kukamilisha
maadili mema: "Hakika si jambo jingine bali nimetumwa ili kukamilisha
maadili mema."
Naam, Mtume SAW alikuja kwa ajili ya kulea na kukamilisha maadili na kutakasa
moyo wa mwanaadamu sambamba na kukuza elimu na ujuzi wake. Kwa kutumia mabawa
hayo mawili ya maadili bora na elimu, mwanaadamu huweza kupaa na kupata saada
katika njia ya kuelekea kwa Allah SWT na hivyo kufika katika nafasi ya juu
anayostahiki. Kwa hakika katika Qur'ani Tukufu suala la elimu au mafunzo
limetajwa sambamba na utakasaji nafsi na hili linaonyesha ni kwa kiwango gani
kila moja ya nukta hizo huathiri nyingine.
Hakuna shaka kuwa katika kila uga hasa katika masuala ya kiakhlaqi, wanaadamu
wanahitaji kigezo bora na kilichokamilika.
Mohammad SAW, kigezo bora zaidi
Mwenyezi Mungu SWT amewaonyesha wanaadamu kigezo bora zaidi.
Amewaonyesha mwanadamu yule yule ambaye ameteuliwa kuwaongoza wanaadamu wenzake
kuelekea katika njia ya Mwenyezi Mungu na ambaye binafsi alikuwa kigezo bora
zaidi cha maadili na vitendo. Katika Qur'ani Tukufu tunasoma hivi:
‘Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ....'Surat al
Ah'zab Aya ya 21
Kwa mujibu wa aya hii, Mtume SAW sambamba na kubainisha nadharia ya maadili,
ili kakamilisha maadili bora katika jamii, yeye mwenyewe alitekeleza kivitendo
maadili mema. Kuhusiana na hili, Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu Aya ya
nne Surat al Qalam amemhutubu Mtume SAW kwa kusema, ‘Na hakika wewe una tabia
tukufu.'
Taathira hii kubwa ya kimaadili ya Mtume SAW ndiyo iliyompelekea kuwakusanya
Waarabu Mabedoui wa zama za Jahiliya na kuwahubiria dini ili kuwaondoa katika
dimbwi la ujalili na kuwapeleka katika njia iliyojaa nuru ya Mwenyezi Mungu.
Lengo kuu la kubaathiwa Mtume SAW na Mitume wote ni kuongoza na kutakasa nafsi
za wanaadamu wote.
Mitume wote walitumwa katika mhimili wa kumuamini Mwenyezi Mungu na hawakuwa na
lengo lingine ila kuwaongoza wanaadamu. Kwa hivyo Mitume wote walifuata njia
moja. Kile kilichotofautiana ni kuhusu masuala ya dini na sheria.
Wanaadamu katika vipindi vyote vya historia wamekuwa wakitegemea juhudi za
Mitume wa Mwenyezi Mungu kwani bila wao, wangefuata mkondo wa waliopotea.
Mtume wa Mwisho Mohammad SAW, ambaye alibeba ujumbe wa mwisho wa Allah na
kuleta rehma na dini kamilifu zaidi duniani, alibaathiwa ili kuwaokoa wanaadamu
wote.
Mtume Muhammad SAW kwa kusoma aya za Wahyi na kuweka wazi njia iliyonyooka ya
Mwenyezi Mungu, aliweza kuongoza nyoyo za wanaadamu kuelekea katika nuru ya
uongofu. Hili ndilo lengo la juu la kubaathiwa Mtukufu huyo. Kwa hivyo malezi
bora na kuwaongoza wanaadamu katika njia ya haki sambamba na kutenganisha haki
na batili na kheri na shari ni jukumu muhimu la mitume hasa Mtume Mtukufu SAW.
Hili ni lengo ambalo limesisitizwa mara kadhaa katika Qur'ani Tukufu. Katika
aya ya 11 ya Surat al Mujaadalah Allah SWT anasema: ... Mwenyezi Mungu
atawainua walio amini miongoni mwenu, na walio pewa ilimu daraja za juu....
Kwa hivyo, lengo muhimu na la juu la kubaathiwa Mtume Mtukufu wa Uislamu ni
Tazkiyatun Nafs au kutakasa nafsi za watu na kuondoa mafungamano ya kimaada
katika nyoyo za watu na kuwaongoza katika ubora wa kimaanawi.
Dunia inahitaji mafundisho ya Mohammad SAW
Wakati tunapoangalia hali mbaya ya hivi sasa duniani tunahisi kuwa Bwana Mtume
aliteuliwa kwa ajili ya zama hizi na malengo na mafunzo yake ni yenye
kumuongoza mwanaadamu anayekumbwa na masaibu katika karne ya 21.
Maadili bora na umaanawi ni johari zilizopotea za mwanaadamu katika zama hizi
na hayo mawili yaliweza kuwasilishwa na Mtume SAW kwa njia ya juu na bora zaidi
kwa wanaadamu wote. Ni kwa sababu hii ndio hivi sasa tunashuhudia namna siku
hadi siku watu wanavutiwa na dini ya Mtume Muhammad SAW ambayo ujumbe wake
mkubwa ulianzia katika Pango la Hiraa ili kuwaongoza wanaadamu katika njia
kamilifu iliyojaa nuru.
Sala na Salamu za Mwenyezi Mungu zimfikie Mtume (SAW) na Kizazi chake
Kitoharifu (AS).