Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qasemi ametuma salamu za rambirambi na mkono wa pole kwa familia za wahanga wa mashambulizi hayo na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani ugaidi wa aina zote na popote pale unapotokea duniani na unazitaka nchi zote kupambana kwa nguvu zote na vyanzo, sababu na wanaofanya mashambulizi ya kigaidi.
Qasemi amesema kuwa ugaidi hususan katika Mashariki ya Kati umeonesha
kuwa, ovu hilo halitambui mipaka wala utaifa na hakuna njia nyingine ya
kukabiliana nalo isipokuwa mshikamano na umoja wa kimataifa.
Naye Waziri wa Mambo ya Iran Mohammad Javad Zarif katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa twitter amesema magaidi hawana mistari myekundu tena na kwamba Waislamu wote wa madhehebu ya Shia na Sunni wanalengwa na hivyo kunapaswa kuwa na umoja kukabiliana na ugaidi.
Magaidi wawili waliokuwa na mabomu jana jioni walijilipua karibu na
Masjidu Nabawi mjini Madina na katika msikiti mwingine wa Waislamu wa
madhehebu ya Shia katika mji wa Qarif huko mashariki mwa Saudia.
Mashambulizi hayo yaliyotekelezwa na magaidi wakufurishaji wa Kiwahhabi yamesababisha vifo vya watu wasiopungua sita na
kujeruhi wengine kadhaa.