IQNA

Ujumbe wa Hija wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Waislamu Duniani 1437 Hijria

15:05 - September 05, 2016
Habari ID: 3470550
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma Ujumbe muhimu kwa Waislamu duniani na hasa Mahujaji wa Nyumba tukufu ya Allah mwaka huu 1437 Hijria). Ifuatayo ni matini kamili ya ujumbe huo.
Ujumbe huo umesambazwa mwaka huu katika hali ambayo, kutokana na vikwazo na vizuizi vingi vilivyowekwa na watawala wa Saudi Arabia, Waislamu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameshindwa - mwaka huu - kwenda kutekeleza ibada hiyo tukufu.
Katika ujumbe wake wa Hija wa mwaka huu, Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, ulimwengu wa Kiislamu iwe ni tawala au wananchi Waislamu, wanapaswa wawatambue vyema watawala wa Saudia na wautambue uhakika hatari na mchungu na ukosefu wao wa imani na kutawaliwa watawala hao na mambo ya kimaada. Vile vile amewataka Waislamu wasiruhusu watawala hao wapite hivi hivi bila ya kukumbwa na madhara ya jinai kubwa wanazozifanya dhidi ya Waislamu duniani. Vile vile amewataka Waislamu wakae na kutafakari dhulma iliyofanywa na watawala hao dhidi ya wageni wa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema na wafikirie kwa kina njia za kusimamia na kuendesha Haram mbili tukufu za Makka na Madina na uendeshaji wa suala zima la ibada ya Hija. Amesema, upuuzaji na uzembe wa aina yoyote katika utekelezaji wa jukumu hilo, utautumbukiza mustakbali wa umma wa Kiislamu katika matatizo makubwa.
Matini kamili ya ujumbe huo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao umesambazwa mchana wa siku ya Jumatatu Novemba 5, 2016 ni kama ifuatavyo:
 

Bismillahir Rahmanir Rahim.
Na hamdu na shukrani zote zinamstahikia Allah, Mola Mlezi wa viumbe wote. Na rehema na amani ziwe juu ya Bwana wetu Muhammad na Aal zake watoharifu na masahaba wake wateule na wote waliowafuata hao kwa wema hadi Siku ya Kiyama.

Ndugu zangu makaka na madada Waislamu kote ulimwenguni!
Msimu wa Hija kwa ajili ya Waislamu ni msimu wa kujifakharisha nao, ni msimu wa kujivunia mbele ya macho ya walimwengu. Msimu wa Hija ni wa kuzinawirisha nyoyo na kuingiza humo khushuu na unyenyekevu mbele ya Muumba. Hija ni faradhi tukufu ya kidunia, Kiungu na kiwatu. Hija ni faradhi itokanayo na amri ya Mwenyezi Mungu aliposema:


فَاذْكُرُواْ اللَّهَ كَذِكْرِكُمْ آبَاءَكُمْ أَوْ أَشَدَّ ذِكْرًا

Basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyokuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi. Na amri inayosema:

وَاذْكُرُواْ اللَّهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ

Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku chache zinazohisabika.

Vile vile Hija inatokana na maneno ya Mwenyezi Mungu aliposema:


الَّذِي جَعَلْنَاهُ لِلنَّاسِ سَوَاء الْعَاكِفُ فِيهِ وَالْبَادِ


(Msikiti Mtakatifu wa Makkah) Ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na wageni.

Yote hayo yanabainisha kwa uwazi vipengee visivyo na kifani na hali tofauti za Hija.
Katika faradhi hii ya kidini isiyo na mfano, suala la usalama wa wakati na sehemu ni mithili ya ishara iliyo wazi na nyota inayong'ara ambayo inazipa utulivu nyoyo za watu na kumtoa hujaji kutoka katika mzingiro wa mambo yanayovunja usalama yanayosababishwa na madhalimu mabeberu ambayo daima yamekuwa yakitishia usalama wa wanadamu, na hatimae kumpa hujaji furaha ya usalama katika kipindi fulani maalumu.
Hija ya Kiibrahimu ambayo ni zawadi waliyopewa Waislamu na (dini tukufu ya) Uislamu, ni dhihirisho la heshima, umaanawi, umoja na adhama; inawadhihirishia kwa uwazi kabisa maadui na wale wanaowatakia mabaya Waislamu, utukufu wa umma wa Kiislamu na kutegemea kwao nguvu isiyo na kikomo ya Mwenyezi Mungu, na vile vile kuchora picha ya namna wanavyoweza kuwa mbali na karo za ufisadi, udhalilishaji na udunishaji; mambo ambayo mabeberu na waistikbari wa kimataifa wamezitishwa jamii za wanadamu duniani. Hija ya Kiislamu na kitauhidi, ni dhihirisho la kweli la aya ya Qur'ani Tukufu inayosema:


أَشِدَّاء عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاء بَيْنَهُمْ


...wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao.

Hija ni mahala pa kujibari na kujiweka mbali na washirikina na ni mahala pa kutia nguvu umoja na mshikamano wa waumini.
Wale watu ambao wameifanya Hija kuwa ni safari ya kitalii na matembezi ambao wanaficha chuki zao kwa taifa la waumini na wanamapinduzi la Iran ndani ya madai ya kukataa kuingiza siasa ndani ya Hija, ni mashetani dhalili na duni ambao wanatetemeka wanapoona tamaa za shetani mkubwa Marekani zinaingia hatarini. Watawala wa Kisaudi ambao mwaka huu wamewazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na Masjidul Haram na kuwafungia njia mahujaji wenye ghera na waumini wa Kiirani wasiweze kufanya ibada katika nyumba ya Mahbubu wao, ni watu waovu waliopotea ambao wanaona kuwa hawawezi kubakia kidhulma katika madaraka ila kwa kuwalinda waistikbari na mabeberu wa dunia na kuwa waitifaki wa Uzayuni na Marekani ambao muda wote wanafanya juhudi za kuwakidhia waistikbari hao matakwa yao; hawasiti hata kidogo kufanya usaliti wa aina yoyote ile kwenye jambo hilo.
Hivi sasa karibu mwaka mzima umepita tangu lilipotokea tukio la kutisha la Mina. Ndani ya tukio hilo, maelfu kadhaa ya mahujaji waliokuwa katika nguo za Ihram, chini ya jua na midomo yenye kitu waliuawa kidhulma ndani ya siku ya Idi. Siku chache kabla ya tukio hilo, majimui ya mahujaji waliokuwa katika ibada na katika hali ya kutufu na kusali waliuawa ndani ya Masjidul Haram. Watawala wa Kisaudi ndio wa kulaumiwa katika matukio yote hayo mawili; na hicho ni kitu ambacho kinakubaliwa kwa kauli moja na watu wote waliokuwepo, wachunguzi na kila aliyeyafanyia utafiti kiutaalamu matukio hayo; bali wako baadhi ya wataalamu wanazungumzia uwezekano wa kwamba jambo hilo lilifanywa kwa makusudi. Kupuuza na kufanya uzembe katika kuwaokoa mahujaji ambao walikuwa hawajakata roho ambayo nyoyo zao ambao roho zao zenye shauku na nyoyo zao zenye hamu katika Siku ya Idi ya Kuchinja ziliambatana na ndimi zao zilizokuwa zikimtaja Allah kwa dhikri na kusoma aya za maneno ya Mwenyezi Mungu. Wasaudi watenda jinai na wenye nyoyo ngumu waliwachukua majeruhi hao na kuwafungia kwenye makontena pamoja na mahujaji waliofariki dunia; na badala ya kuwatibu na kuwasaidia au hata kuwafikishia maji katika midomo yao iliyokuwa na kiu (kali), waliwaua shahidi (mahujaji hao ambao walikuwa bado hawajakata roho). Maelfu kadhaa ya familia kutoka nchi mbalimbali zilipoteza wapendwa wao na mataifa yao yakapatwa na msiba. Kulikuwa na karibu mashahidi laki tano katika mashahidi hao kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Nyoyo za familia zao bado zimejeruhika na zina msiba, huku taifa nalo likiwa bado limo katika majonzi na limekasirika.
Badala ya watawala wa Kisaudi kuomba radhi, kujuta na kuwafuatilia kisheria wahusika wa moja kwa moja wa tukio hilo la kutisha; ndio kwanza wanakataa - kijeuri kabisa na bila ya kuona haya - hata kuunda tume ya kimataifa ya Kiislamu ya kutafuta ukweli kuhusu tukio hilo; na badala ya watawala hao kukaa kwenye kizimba ya mtuhumiwa, wamekaa nafasi ya mdai na kuzidi kudhihirisha na kuonesha uadui wao wa muda mrefu - kikhabithi na kipuuzi - kwa Jamhuri ya Kiislamu na kwa kila bendera ya Kiislamu inayopeperushwa kwa ajili ya kukabiliana na ukafiri na Uistikbari.
Honi zao za kipropaganda; kuanzia wanasiasa wao ambao mienendo yao kuhusu Wazayuni na Marekani ni aibu kwa ulimwengu wa Kiislamu hadi mamufti wao wasio wacha Mungu na walaharamu ambao wanatoa fatwa zinazokwenda kinyume kabisa na Kitabu na Sunna, na hadi kundi la vyombo vyao vya habari ambavyo hata maadili yao ya kiutaalamu hayawazuii kutunga na kusema uongo, wanafanya njama za kipuuzi kuituhuma Jamhuri ya Kiislamu kuwa eti ndiyo iliyosababisha mahujaji wa Iran wasiende kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu. Watawala waenezaji fitna wa Kisaudi ambao wameanzisha ya kuyatia nguvu makundi ya kitakfiri na ya kishari, yameutumbukiza ulimwengu wa Kiislamu katika vita vya ndani na kuuliwa na kujeruhiwa watu wasio na hatia na ambao mikono yao imejaa damu za watu hao katika nchi za Yemen, Iraq, Sham, Libya na katika nchi nyinginezo duniani; wacheza siasa ambao hawamuogopi Mwenyezi Mungu ambao wameunyooshea mkono wa urafiki utawala vamizi wa Kizayuni, na kuwasababishia masaibu na mateso makubwa Wapalestina na kupanua wigo wa dhulma na usaliti wao hadi katika miji na vijiji vya Bahrain; watawala wasio na dini wala maadili ambao hata nyoyo zao haziwasuti na ambao wamesababisha maafa makubwa ya Mina ambao wamevunja utukufu wa Haram yenye usalama ya Mwenyezi Mungu kwa jina la watumishi wa Haram mbili tukufu na ambao wamewatoa muhanga wageni wa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema katika siku ya Idi huko Mina na kabla ya hapo ndani ya Masjidul Haram; hivi sasa wanapiga domo la kukataa kuingizwa siasa katika Hija na wanawatuhumu wengine kufanya madhambi makubwa ambayo ni wao wenyewe walioyafanya au kusabibisha kutokea kwake. Watawala hao ni ‘misdaki' na dhihirisho kamili la maneno yaliyo wazi ya Qur'ani Tukufu yanayosema:


وَ اِذا تَوَلّىٰ سَعىٰ فِی الاَرضِ لِیُفسِدَ فیها وَ یُهلِکَ الحَرثَ وَ النَّسلَ وَ اللّهُ لا یُحِبُّ الفَساد * وَ اِذا قیلَ لَهُ اتَّقِ اللّهَ اَخَذَتهُ العِزَّةُ بِالاِثمِ فَحَسبُه‌ُ جَهَنَّمُ وَ لَبِئسَ المِهاد

Na anapotawala hufanya juhudi katika ardhi kufanya ufisadi humo, na huangamiza mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi. Na akiambiwa: Mche Mwenyezi Mungu, hupandwa na mori wa kutenda madhambi. Basi huyo inamtosha Jahannam, nayo ni makao mabaya mno.

Mwaka huu pia kwa mujibu wa ripoti mbali mbali zilizotolewa, mbali na kuwazuia mahujaji wa Kiirani na wa mataifa mengine, mahujaji wa nchi nyinginezo nao wanadhibitiwa kwa njia isiyo ya kawaida kwa msaada wa mashirika ya kijasusi ya Marekani na utawala wa Kizayuni, na nyumba ya Mwenyezi Mungu iliyo salama, imekuwa haina salama kwa watu wote. Ulimwengu mzima wa Kiislamu, iwe ni tawala au wananchi Waislamu wa nchi hizo, wanapaswa kujua vizuri uhakika wa kutisha na ukosefu wa imani wa watawala wa Kisaudi na namna watawala hao walivyotekwa na mambo ya kimaada; na haupaswi kuwaacha vivi hivi watawala hao kutokana na jinai walizousababishia ulimwengu wa Kiislamu. Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kufikiria kwa kina suala la kusimamia haram mbili tukufu na suala zima la Hija kutokana na vitendo vya kidhulma vilivyofanywa na watawala hao dhidi ya wageni wa Mwingi wa rehema. Kufanya uzembe katika kutekeleza jukumu hilo, kutauutumbukiza mustakbali wa umma wa Kiislamu katika matatizo makubwa zaidi.
Ndugu zangu Waislamu, wake kwa waume! Mwaka huu nafasi ya mahujaji wenye shauku na ikhlasi wa Kiirani iko wazi katika ibada ya Hija, lakini mahujaji hao wako pamoja na mahujaji wengine kutoka kona zote za dunia kwa nyoyo zao, na wanawaombea dua ili mti uliolaaniwa wa mataghuti kuwasababishia madhara yoyote yale. Wakumbukeni ndugu zenu wa Iran katika dua na katika ibada na kunong'ona kwenu na Mwenyezi Mungu na ombeni dua Mwenyezi Mungu aziondolee matatizo jamii za Waislamu na aukate mkono wa waistikbari na Wazayuni na vibaraka wao katika umma wa Kiislamu.
Ninapenda kuitumia fursa hii kuwakumbuka na kuwaenzi mashahidi wa Mina na wa Masjidul Haram na mashahidi wa Makka wa mwaka 1366 (Hijria Shamsia sawa na Julai 31, 1987) [*13] na ninamuomba Mwenyezi Mungu ‘Azza Wajalla, awape maghufira, awarehemu na awanyanyue daraja za juu za utukufu. Ninamuombea rehema Imam wa zama (Imam Mahdi AF - roho yangu iwe fidia kwake) nikiomba dua yenye kutakabaliwa ya mtukufu huyo iwe sababu ya kupata utukufu umma wa Kiislamu na kuwaokoka Waislamu mbele ya fitna na shari ya maadui.
Na Taufiki ni ya Mwenyezi Mungu, Naye Ndiye Mbora wa kutegemewa.


Sayyid Ali Khamanei
Mwishoni mwa Mfunguo Pili Dhul Qaad 1437 (Hijria)
12/06/1395 (Hijria Shamsia)
(Septemba 5, 2016).

 


[*13]: Maafa ya Ijumaa ya umwagaji damu ya mjini Makkah ni mfano mwingine wa uadui wa Marekani ambayo yalitokea Mwezi Sita Mfunguo Tatu Dhil Hijja 1407 katika msimu wa Hija na baada ya kumalizika ibada ya kujibari na kujiweka mbali na washirikina. Watawala wa ukoo wa Aal Saud waliivunjia heshima ya amani iliyotangazwa na Mwenyezi Mungu kwa watu wanaoingia eneo hilo na kuwaua shahidi kwa umati karibu mahujaji 400 wa Kiirani na wasio wa Iran - wengi wao wakiwa ni wanawake - na kuwajeruhi wengine wengi zaidi ya hao kwa mara kadhaa.



3527923
captcha