IQNA

Mufti wa Saudi awakufurisha Wairani, Waziri Zarif amjibu

10:53 - September 08, 2016
Habari ID: 3470553
Waziri wa Mambo ya nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa jibu kwa matamshi ya kijahili na dharau yaliyotolewa hivi karibuni na mufti mkuu wa Saudi Arabia.

Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu alijibu matamshi ya dharau na ya kipumbavu ya mufti huyo Abdul Aziz Aal Sheikh  kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, ambaye alidai kwamba Wairani sio Waislamu. Zarif aliandika kwamba  ni kweli kuwa Uislamu wa Wairani na wa Waislamu walio wengi duniai hauwezi kufananishwa na Uislamu bandia, wa kupindukia mipaka na wa kibaguzi unaoenezwa na Mufti huyo wa Kiwahhabi pamoja na waanzilishi wa ukoo wa Saudia unaoneza ugaidi katika ulimwengu wa Kiislamu.

Hii ni katika hali ambayo chanzo na chimbuko la itikadi na fikra za kundi la kigaidi la Daesh zinatokana na fatwa zinazokinzana na Uislamu halisi wa Mtume Muhammad (saw), makundi ya Kiwahhabi na mamufti wa Saudia, fatwa ambazo kwa hakika zimechafua jina na sura halisi ya Uislamu ulimwenguni na kumwaga damu ya Waislamu wasio na hatia katika nchi za Syria, Iraq, Yemen na nchi nyinginezo za Kiislamu. Matamshi ya Wasaudia si tu kwamba yamevuka mipaka ya kiburi na kutokuwa na mantiki bali yanaandamana na wendawazimu ambao unaonekana wazi si  kwenye maneno yao tu bali hata kwenye vitendo vyao na hilo limewadhihirikia wazi walimwengu wote. Hivi sasa watawala wa Saudia wamekwama kwenye kinamasi ambapo kila wanapojaribu kujikwamua ndipo wanapozidi kuzama zaidi kwenye kinamasi hicho.

Badala ya kutoa matamshi ya dharau na yasiyo ya kimantiki, watawala hao wanapasa kujirudi na kutalii historia yao ili kuona ni wapi walipoanza kupotea njia, na ni hadi lini wanaweza kuendeleza mchezo huo mchafu. Wasaudi wanatumia vyombo vitatu katika mchezo huo mchafu. Chombo cha kwanza ni Hija ambayo kutokana na usimamizi wao mbaya na usiofaa wamebadilisha eneo hilo takatifu na la amani na utulivu kwa waumini wa Kiislamu kuwa kichinjio cha kuwachinja Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Kwa kujaribu kupotosha ukweli wa mambo kuhusiana na maafa ya Mina, watawala hao waovu wa Saudia sasa wanadai kwamba iwapo zaidi ya Mahujaji 7000 wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu walipoteza maisha yao kwenye Hija ya mwaka uliopita wakiwemo Mahujaji wa Kiirani wapatao 464 tena katika siku ya Idul Adh'ha, basi maafa hayo ambayo yalipelekea Mahujaji waliokuwa na kiu kali ya maji kuuawa kinyama hayakutokana na usimamizi mbaya wa watawala wa Riyadh bali yalitokana na Iran ambayo inataka kuifanya Hija kuwa ya kisiasa.

Chombo cha pili kinachotumiwa na Wasaudia katika mchezo huo mchafu wa kisiasa ni kutumia mbinu ya kijeshi ambayo tunashuhudia ikitekelezwa kiyama nchini Yemen kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa nchi za Magharibi na utawala haramu wa Israel. Saudia inasema inatekeleza hujuma hiyo ya kijeshi nchini Yemen kutokana na kuhofia mustkabali wake wa kidemokrasia na kwamba inataka kuinusuru nchi hiyo kutokana na mgogoro unaoikabili, na hii katika hali ambayo nchi hiyo yenyewe haijui misingi ya demokrasia ni nini na imekuwa ikitumia mabomu na silaha zilizopigwa marufuku kuwaua kinyama wananchi wa Yemen pamoja na kuharibu miundombinu muhimu ya nchi hiyo.Mufti wa Saudi awakufurisha Wairani, Waziri Zarif amjibu

Chombo cha tatu kinachotumiwa na Wasaudi katika kuendeleza mgogoro huo ni pesa zinazotokana na mauzo ya mafuta ambapo imefanya njama ya wazi na ya makusudi ya kuzidisha uzalishaji wa mafuta wa kupindukia na hivyo kupunguza kwa njia isiyo ya kawaida bei ya bidhaa hiyo muhimu katika soko la kimataifa, njama ambayo imeugeuka yenyewe na kutoka kwenye udhibiti wake ambapo hivi sasa nayo inadhurika moja kwa moja na kupungua huko kukubwa kwa bei ya mafuta katika soko la mafuta duniani na hivyo kuifanya ikabiliwe na nakisi ya bajeti ya zaidi ya dola bilioni 100.

Katika hali hiyo Saudi inakabiliwa na changamoto nyingine kubwa nayo ni ya nchi za Kiislamu kupoteza imani nayo kuhusiana na uendeshaji wake wa ibada muhimu ya Hija. Hiyo ni changamoto muhimu ambayo watawala wa Saudia wamehindwa kukabiliana nayo na kwa hivyo wanafanya juhudi kubwa za kuzua uchochezi wa kisiasa kwa shabaha ya kupotosha ukweli wa mambo kwa kuelekeza lawama kwingine. Ni kutokana na ukwei huo ndipo Bahram Qassimi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akasema hivi karibuni kwamba watawala wa Saudia wanafanya juhudi kubwa za kukwepa majukumu na lawama kubwa wanayoelekezewa kutokana na usimamizi wao mbovu wa Hija, katika hali ambayo wanapasa kuwajibika na kutoa jibu la kukinaisha kuhusiana na maafa ya Mina kwa familia za wahanga wa maafa hayo.

3528473

captcha