IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ukatili wa Saudia dhidi ya raia Yemen ni aina mbaya zaidi ya ugaidi

12:38 - October 27, 2016
Habari ID: 3470637
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa ugaidi ni miongoni ma masaibu yanayoiumiza sana jamii ya mwanadamu.

Ayatullah Khamenei aliyasema hayo jana jioni katika mazungumzo yake na Rais Sauli Niinistö wa Finland hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, mauaji ya halaiki kama yale yanayofanywa na serikali ya Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen ndio aina mbaya zaidi ya ugaidi. Amesisitiza kuwa, mapambano dhidi ya ugaidi yanahitaji azma kubwa ya wale wote wenye ushawishi ndani ya mamlaka ya kimataifa, na kwamba watu wenye busara, nchi mbalimbali na wale wenye nguvu na sharafu duniani wanapaswa kutafakari na kuchukua hatua za kuondoa uovu huo. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Marekani na baadhi ya nchi hazina azma thabiti ya kupambana na ugaidi na kuongeza kuwa, nchi hizo zinayahesabu masuala yote kwa mujibu wa maslahi yao na hazifikirii kabisa suala la kutokomeza maradhi ya ugaidi iwe ni huko Iraq au Syria. 

Vilevile Ayatullah Khamenei amesema msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu utatuzi wa kadhia ya Syria ni wa kimantiki na unaotetea taifa na serikali halali ya nchi hiyo. Ameongeza kuwa, Marekani na baadhi ya nchi nyingine zinasisitiza suala la kuondolewa madarakani serikali ya Syria ilhali ni lazima kwanza kuainishwa aliyeanzisha na kuchochea vita kwa ajili ya kukomesha vita hivyo.

Vilevile amekosoa misimamo ya Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa na kusema: Katibu Mkuu wa umoja huo amesema waziwazi kwamba kutokana na taasisi hiyo kutegemea fedha za Saudi Arabia hakuna uwezekano wa kulaaniwa mauaji yanayofanywa na nchi hiyo dhidi ya watoto wa Yemen, suala ambalo linadhihirisha hali ya kusikitisha ya kimaadili ya wanasiasa katika uongozi wa jumuiya za kimataifa. Amesisitiza kuwa, anatajia Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa atalinda kujitawala kwa taasisi hiyo ya kimataifa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekaribisha suala la kuzidishwa kiwango cha ushirikiano wa Iran na serikali ya Finland na akasema kuwa: Makubaliano yaliyotiwa saini baina ya pande mbili yanapaswa kutekelezwa kivitendo na kutotekelezwa kwake kutakuwa na taathira mbaya katika fikra za wananchi.

Kwa upande wake Rais Sauli Niinistö wa Finland ameeleza kuridhishwa na mazungumzo yake hapa mjini Tehran na ameunga mkono mtazamo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu ugaidi. Amesema kuwa, nchi mbalimbali na Umoja wa Mataifa zimefeli katika suala la kudhibiti na kupambana na ugaidi. 

Amezungumzia pia nafasi na ushawishi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na mchango wake mkubwa katika kupambana na ugaidi na kasema kuwa, Iran imefanya jitihada kubwa katika suala la kung'oa mizizi ya ugaidi na kwamba hapana shaka kuwa kazi hiyo itadumishwa. 

3541134

captcha