IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kwa mapambano na umoja, Utawala wa Kizayuni utaangamia katika kipindi cha miaka 25

21:48 - December 14, 2016
Habari ID: 3470743
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Pamoja na kuwa waitifaki wa utawala wa Kizayuni wanaibua migogoro mara kwa mara ili kadhia ya Palestina isahaulike, lakini ardhi hii takatifu itakombolewa kwa baraka za muqawama na jihadi ya taifa na makundi ya Palestina".

Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumatano mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Ramadhan Abdullah Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, njia pekee ya kuikomboa Quds Tukufu ni mapambano na muqawama na kwamba njia zinginezo haziwezi kuwa na mafanikio.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, "Kama ambavyo tuliwahi kusema, iwapo Wapalestina na Waislamu wataungana na kupambana na utawala wa Kizayuni, basi utawala huo hautakuwepo katika kipindi cha miaka 25 ijayo."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema chanzo kikuu cha matatizo mengi katika eneo ni, "Muistikbari Mkuu  na Shetani Mkubwa " yaani Marekani. Ameashiria uingiliaji wa mashetani wadogo wa eneo katika kuibua migogoro iliyopo na kusema: "Lengo lao wote ni kupelekea kadhia ya Palestina isahaulike au kudunishwa katika fikra za Umma katika eneo.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na kuwa inakabiliana na masuala mengine ya eneo, daima na kwa uwazi kabisa imetangaza kuwa kadhia ya Palestina ni ya kwanza kwa umuhimu katika Ulimwengu wa Kiislamu na imetekekeza wajibu wake kuhusiana na suala hili."

Kiongozi Muadhamu ameashiria kufurashishwa kwake na mpango wa vipengee 10 wa Jihad Islami ya Palestina kwa ajili ya umoja na muqawama katika kukabiliana na Wazayuni. Amesema nukta muhimu katika vipengee hivyo ni mapambano na kupinga kikamilifu mikataba ya maelewao na Wazayuni sambamba na kusisitiza kuhusu umoja wa makundi ya Palestina na  kulaani baadhi ya madola ya eneo yanayopinga mapinduzi na ambayo yanahimiza malewano na Wazayuni.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, mpango huo unapaswa kutekelezwa na kuongeza kuwa, hakuna shaka kuwa, kuna watu waliotumwa ambao watajaribu kuzuia utekelezwaji  wa vipengee hivyo vya Harakati ya Jihad Islami na kwa msingi huo lazima kuwepo uangalifu kuhusu mpango huo ili usibakie tu kwenye makaratasi na hatimaye kusahaulika.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, moja ya masuala muhimu ya eneo ni kukabiliana kwa pamoja na makundi ya wakufurishaji kama vile ISIS au Daesh, Jabhatun Nusra na makundi mengine kwani kinyume na hilo, kutokana na kuendelea kuibuliwa migogoro na hao wakufurishaji, kadhia ya Palestina itasahaulika.

Kwa upande wake, Ramadhan Abdullah Katibu Mkuu wa Harakati ya  Jihad Islami  ya Palestina amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa misimamo yake ya kishujaa na hekima. Aidha ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuunga mkono malengo ya taifa la Palestina. Ameashiria kuongezeka mara kadhaa uwezo wa kivita wa makundi ya Palestina ikilinagnishwa na wakati wa vita vya siku 50 vya mwaka 2014 vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza na kusema Palestina ni ardhi yenye kuainisha hatima na maadamu haki ya watu wake haijarejeshwa eneo halitashuhudia utulivu.

3553993

Habari zinazohusiana
captcha