IQNA

Rais Kenyatta asaini sheria inayoimarisha Mfumo wa Fedha wa Kiislamu Kenya

12:54 - January 04, 2017
Habari ID: 3470779
IQNA-Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesaini sheria itakayoimarisha nafasi ya Kenya kama kitovu cha mfumo wa fedha wa Kiislamu barani Afrika.

Hivi karibuni rais wa Kenya alisaini na kuidhinisha Sheria ya Bima (iliyorekebishwa) ya mwaka 2016 ambayo kimsingi itapalekea mashirika ya bima ya Kiislamu yaani Takaful kufanya kazi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na hivyo kuhimiza mashirika ya kimataifa kuwekeza katika sekta hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, hatua hiyo inakuja wiki moja baada ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Kenya (CMA) kuruhusiwa na Baraza la Bodi ya Huduma za Kifedha za Kiislamu (IFSB) kuwa mwanachama wa bodi hiyo. IFSB ina makao yake huko Kuala Lumpur Malaysia ni ni bodi ya kimataifa inayoweka viwango na kustawisha huduma za kifedha za Kiislamu zenye uwazi na usimamizi bora duniani.

Uamuzi wa kuingiza Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Kenya katika IFSB ulichukuliwa katika kikao kilichofanyika Cairo, Misri Disemba 14.

Mwezi Oktoba mwaka jana serikali ya Kenya ilizindua ofisi maalumu ijulikanayo kama Kurugenzi ya Mradi wa Kifedha wa Kiislamu (PMO) itakayoongozwa na Shirika la Kimataifa la Kutoa Ushauri na Dhamana Kuhusu Huduma za Kifedha za Kiislamu (IFAAS).

Mkurugenzi Mkuu wa CMA Paul Muthaura amesema hatua ya mamlaka hiyo kujiunga na IFSB ni muhimu katika kustawisha Kenya kama kitovu cha huduma za kifedha za Kiislamu eneo la Afrika Mashariki. Amesema hatua hiyo ni kati ya misingi muhimu ya kuufanya mji wa Nairobi uwe kituo cha kimataifa cha kifedha. "Kenya imekuwa ikiweka misingi ya kuwa kitovu cha huduma za kifedha na moja ya sekta ambazo zinazingatiwa na kuifanya nchi hii iwe kitovu cha mfumo wa kifedha wa Kiislamu,” amesema Muthaura.

Kwa mujibu wa ripoti ya IFSB yam waka 2016, sekta ya huduma za kifedha za Kiislamu ilikuwa na thamani ya $ trilioni 1.88 mwaka 2015.

Kwa mujibu wa CMA sekta ya mfumo wa kifedha wa Kiislamu Kenya imestawi kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni huku taasisi kadhaa zenye kufuata sharia za Kiislamu zikiendesha shughuli zao nchini humo. Amesema hivi sasa kuna benki mbili kamili za Kiislamu, benki tano zenye kutoa huduma maalumu za Kiislamu, shirika boja la bima aina ya Takaful, mashirika mawili ya kifedha ya ushirika au sacco, na Mfuko wa Soko la Mitaji na Dhamana.

Muthaura ameongeza kuwa, bado kuna fursa kubwa katika sekta ya mfumo wa kifedha wa Kiislamu nchini Kenya kwa faida ya Waislamu n ahata waisokuwa Waislamu kitaifa na kimataifa.

3559602

captcha