Kwa mujibu wa
mwandishi wa IQNA, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Mohammad Javad Zarif amemuandikia barua katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio
Guterres akitaka umoja huo uzingatie zaidi hali mbaya ya Waislamu wa kabila la
Rohingya wanaoteswa na kuangamizwa nchini Myanmar.
Katika barua
yake hiyo, Zarif amebainisha wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya Waislamu wa
kabila la Rohingya na kuongeza kuwa: "Serikali ya Myanmar inapaswa kufahamishwa
udharura wa kusitisha mara moja ukiukwaji wa haki za Waislamu sambamba na
kuhakikisha wanapata misaada ya haraka ya kibinadamu."
Katika barua
hiyo kwa Guterres, Zarif ameongeza kuwa: "Waislamu Warohingya mbali na kuwa
wamepokonywa haki yao ya kimsingi ya kuwa wenyeji wa ardhi yao, kila siku
wanakabiliwa na mauaji na mateso huku idadi kubwa miongoni mwao wakiwa wakimbizi
katika nchi zingine."
Waziri wa Mambo
ya Nje wa Iran katika barua yake ameongeza kuwa, hali ya Waislamu Warohingya ni
kinyume kabisa na hati ya Umoja wa Mataifa na mikataba ya kimsingi ya haki za
binadamu. Amesema hali ya kusikitisha ya Waislamu hao ni jambo ambalo limewatia
wasi wasi mkubwa Waislamu duniani. Waziri Zarif amesema kuvunjiwa haki za
kimsingi Waislamu Warohingya ni jambo linaloweza kuvuruga uthabiti na usalama
nchini humo na pia katika nchi jirani.
Waziri wa Mambo
ya Nje wa Iran ameseama anataraji jamii ya kimatiafa na serikali ya Myanmar
itachukua hatua ili kuzuia Mabudha wenye misimamo mikali kuwakandamiza
Waislamu.
Hivi karibuni
John McKissick, Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR
kusini mwa Bangladesh ametangaza kuwa, jeshi la Myanmar na viongozi wa serikali
ya nchi hiyo wamekuwa wakiwalazimisha Waislamu wa jamii ya Rohingya kuyahama
makazi yao na kukimbilia katika nchi jirani. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa
amesisitiza kuwa serikali ya Myanmar inatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya
Waislamu.
Kwa mujibu wa
Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani
inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. Serikali ya Myanmar inakataa kuwapa haki
za uraia Waislamu hao ambao idadi yao ni zaidi ya watu milioni moja na laki
tatu.
Katika miaka ya
karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au
kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia
na Indonesia kutokana na mashambulio ya vikosi vya serikali na Mabudha wenye
misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi
hiyo.