IQNA

Ayatullah Hashemi Rafsanjani ameaga dunia

22:24 - January 08, 2017
Habari ID: 3470787
IQNA-Ayatullah Ali Akbar Hashemi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuanisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu Iran ameaga dunia leo baada ya umri mrefu wa jihadi na jitihada zisizo na kikomo kwa ajili ya Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Hashemi Rafsanjani amepata mshtuko wa moyo leo Jumapili usiku katika hospitali moja Tehran na madaktari wamejitahidi kumpa matibabu ya haraka lakini hawakufanikiwa.
Hashemi Rafsanjani, ambaye ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 82, alijiunga na chuo cha kidini akiwa kijana na kuanza masomo ya kidini hadi kufikia daraja ya Ijtihad.
Tokea mwaka 1958 alijiunga na mapambano dhidi ya utawala wa kiimla  wa Shah ambapo alifungwa jela mara saba na kuendeleza mapambano hayo hadi wakati wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.
Ayatullah Rafsanjani alikuwa mwenye azma imara katika harakati ya Mapambano ya Kiislamu yaliyoongozwa na Imam Khomeini MA.
Kati ya nyadhifa ambazo Ayatullah Rafsanjani aliwahi kushika baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Kaimu Amri Jeshi Mkuu, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Ulinzi wa Kitaifa na nafasi aliyoishika hadi kifo chake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.
Viongozi mbali mbali wa Iran na wananchi wametuma salamau za rambi rambi kufuatia kifo cha Ayatullah Rafsanjani. Mazishi ya mwanazuoni huyo wa Kiislau na mwanampainduzi yamepangwa kufanyika Jumanne mjini Tehran.
 
captcha