Habari zinasema kuwa, Najib Razak, Waziri Mkuu wa Malaysia ndiye anayetazamiwa kuwa mwenyekiti wa mkutano huo wa OIC unaotazamiwa kufanyika wiki ijayo mjini Kuala Lumpur.
Wawakilishi 56 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushrikiano wa Kiislamu OIC wanatazamiwa kushiriki mkutano huo utakaofanyika Januari 19.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa unafanya uchunguzi kuhusiana na ukandamizaji na mauaji yanayoripotiwa kufanywa dhidi ya jamii ya walio wachache ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar, ukandamizaji unaofanywa na jeshi la nchi hiyo likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali.
Tangu mwaka 2012 Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na maafisa usalama wa Myanmar wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za ukatili, mauaji na hata kubaka wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo.
Serikali ya Myanmar imekataa kuwapa uraia Waislamu wa jamii ya Rohingya wapatao milioni 1.1 na kuwataja kama wahamiaji haramu kutoka Bangladesh.