IQNA

Mwanamke wa kwanza Mwislamu kula kiapo kwa Qur'ani bungeni Marekani

20:00 - January 17, 2017
Habari ID: 3470800
IQNA: Ilhan Omar amekuwa mwanamke wa kwanza kula kiapo kwa Qur'ani Tukufu katika Baraza la Wawakilishi nchini Marekani.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, mnamo Januari 3, Bi. Omar aliapishjwa kama mjumbe wa bunge la Baraza la Wawakilishi katika Jimbo la Minnesota na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza Mwislamu Marekani kushika wadhifa huo. Bi. Omar ambaye anawakilisha eneo la House District 60B la Minnesota, aidha ameweka historia kama Msomali-Mmarekani kuchaguliwa kama mbunge nchini Marekani.

Bi. Omar alikula kiapo (yamini) kwa Qur'ani Tukufu, na hivyo kuwa mtu wa pili kufanya hivyo baada ya Bw. Keith Ellison kuwa Mwislamu wa kwanza kuchaguliwa katika Bunge la Kitaifa la Congress ya Marekani akiwa Mjumbe wa Jimbo la Minnesota. Wawili hao ni wanachama wa chama cha Democratic na Ellison hivi sasa anawania kuwa mwenekiti Kamati ya Kitaifa ya Chama cha Democratic.

Ilhan Omar, ambaye pia huvaa Hijabu, ana umri wa miaka 34 alizaliwa Somalia kabla ya kukimbilia Marekani kutokana na vita katika nchi yake.

Alipokimbia Somalia awali aliishi kwa muda wa miaka mine katika kambi ya wakimbizi nchini Kenya kabla ya kuelekea Marekani katika eneo lenye Wasomali wengi la Cedar-Riverside ambapo aliishi kwa miongo miwili na sasa ni mkurugenzi wa Jumuiya ya Kuwaleta Pamoja Wanawake.

Bi.Omar anamshukuru baba yake, mume na watoto wake pamoja na hayati babu yake kwa kumfundihsa kuhusu demokrasia.

Akisimulia kisha chake, Bi. Omar anasema:"Vita vya Somalia vilianza nikiwa na umri wa miaka minane. Siku moja wanamgambo walijaribu kuvunja mlango wa nyumba yetu na walimiminia nyumba yetu risasi. Familia yetu ilikimbia mapigano huku tukipita juu ya miili ya watu waliouawa na magofu ya nyumba zilizobomolewa."

Amesema kuchagliwa kwake ni ishara kuwa ubaguzi unaweza kuangamizwa duniani.

Bi. Omar aligonga vichwa vya habari hivi karibuni baada ya kudhalilishwa na dereva wa teksi ambaye alimtusi kwa maneno ya chuki dhidi ya Uislamu mjini Washington.

Katika tukio hilo la mwezi Disemba mwaka jana, Bi. Omar alichapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa: "Nilipokuwa nikiondoka kwenye mkutano wa sera katika Ikulu ya White House nikielekea hotelini, nilikumbana na tukio la kibaguzi na chuki ambalo sijawahi kulishuhudia tena. Dereva wangu wa teksi alianza kunitolea maneno ya chuki na kuniita mfuasi wa kundi la kigaidi la ISIS huku akitishia kunivua hijabu."

Mtunga sheria huyo wa Kisomali ameongeza kuwa: "Sielewi watu wanatoa wapi ujasiri wa kueneza wazi wazi chuki zao dhidi ya Waislamu."

Kumejiri matukio kadhaa ya kushambuliwa wanawake Waislamu waliokuwa wamevaa vazi la stara la hijabu huku maandishi ya kibaguzi yakiandikwa katika misikiti.

3563615

captcha