IQNA

Iran: Nchi za Kiislamu ziwasaidie Waislamu wanaoteswa Myanmar

11:16 - January 21, 2017
Habari ID: 3470805
IQNA: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa wito kwa nchi za Kiislamu kuwasaidia Waislamu wa kabila la Rohingya nchiniMyanmar wanaokabiliwa na mateso.
Iran: Nchi za Kiislamu ziwasaidie Waislamu wanaoteswa Myanmar
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa mambo ya nje ya Iran ambaye pia amekosoa kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu kukandamizwa Waislamu hao wa Myanmar.
Zarif alitoa kauli hiyo katika kikao maalumu cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC huko, Kuala Lumpur Malaysia.
Katika kikao hicho cha Alhamisi, Zarif alilaani vyombo vya habari duniani kwa kupuuza masaibu ya Waislamu wa Rohingya.  Aidha ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka kuwasaidia Waislamu wa Myamnamr ambao wamenyimwa haki ya uraia huku wakibaguliwa na kuteswa.
 Zarif aidha amezitaka nchi za OIC kuishinikiza Myanmar kuwaheshimu Waislamu wa Rohingya na kuwapa haki zao huku akisema kuna haja ya kuwatumia Waislamu hao misaada ya dharura.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mkuu wa Malaysia, Najib Razak ameilaumu serikali ya Myanmar kwa kuhusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu. Aidha amebainisha wasi wasi wake mkubwa juu ya mgogoro wa kibinaadamu unaowakabili Waislamu wa mkoa wa Rakhine wa nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia.
Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wamekuwa wakishambuliwa na Mabudhha wenye misimamo ya kufurutu ada tokea mwaka 2012  huku vikosi vya usalama navyo vikiwashambulia mara kwa mara. Kutokana na hujuma hizo maelfu ya Waislamu wameuawa na malaki ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi. Serikali ya Myanmar pia imewanyima uraia Waislamu hao na kudai kuwa eti ni wakimbizi walio nchini humo kinyume cha sheria.
3563982


Kishikizo: zarif myanmar
captcha