IQNA

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu Mashariki ya Kati

15:46 - February 09, 2017
Habari ID: 3470841
IQNA-Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja ya nchi zenye nafasi kubwa katika matukio ya eneo la Mashariki ya Kati.

Iran imepata ushawishi huo pamoja na kuwepo njama zisizo na kikomo za nchi za Magharibi za kuitenga Iran na kuifanya isiwe na nafasi katika medani za kieneo na kimataifa.

Ushawishi wa Iran uliimarika punde baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran miaka 38 iliyopita. Wananchi wa Iran Ijumaa 10, Februari wanaadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 chini ya uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini (MA).

Kutokana na taathira mbaya za zama za ukoloni, katika miaka ya hivi karibuni migogoro mingi ya Mashariki ya Kati imepelekea eneo hilo lisiweze kufanikiwa kuwa na mashirikiano mazuri ya kieneo.

Jambo hili limepelekea kudhoofika mshikamano wa nchi za eneo na kwa upande wa pili kutoa mwanya kwa madola ya kibeberu kujipenyeza katika eneo.

Eneo la Mashariki ya Kati au Asia Magharibi, katika miongo mitatu iliyopita limeshuhudia panda shuka nyingi ikiwa ni pamoja na vita na umwagaji mkubwa wa damu na hivyo kuzua mgawanyiko mkubwa katika eneo.

Hali hii imepelekea idadi kubwa ya nchi za eneo hili kuwa tegemezi na jambo hilo limekuwa na taathira hasi kwa usalama jumla. Kufuatia Mwamko wa Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na Afrika Kaskazini kuanzia mwaka 2011 imebainika kuwa Marekani imekuwa ikitekeleza mpango maalumu wa kuingilia moja kwa moja masuala ya eneo hilo pana na pia kutumia shirika la kijeshi la NATO kuvuruga mlingano wa eneo.

Kwa mujibu wa Eliza Jones mtaalamu wa masuala ya kimataifa, eneo la Mashariki ya Kati lina akiba kubwa zaidi ya petroli na gesi duniani. Aidha anasema mabomba ya mafuta ya eneo hili yanaweza kutajwa kuwa mishipa ya uhai wa sekta za viwanda na kijeshi duniani. Jones anaongeza kuwa, nchi za Ulaya na Marekani ziliweza kufahamu ustaarabu kupitia Mashariki ya Kati, eneo ambalo lina historia ndefu ya ustaarabu. Aidha anasema Marekani imejipenyeza Mashariki ya Kati si kwa ajili ya demokrasia bali kwa ajili ya kudhamini maslahi yake haramu.

Njama za Marekani, NATO kubadilisha ramani ya Mashariki ya Kati

Kutokana na nafasi yake muhimu kwa mtazamo wa jiostratijia na jiografia ya kisiasa, eneo la Mashariki ya Kati katika kipindi chote cha historlia limekuwa likikodolewa macho na madola ya kibeberu. Hujuma ya Marekani dhidi ya Afghanistan na Iraq na uingiliaji wa NATO nchini Libya kwa kisingizio cha kutekeleza azimio nambari 1973 la Umoja wa Mataifa na pia hujuma inayoendelea ya Saudia dhidi ya Yemeni, yote hayo yanaweza kutathiniwa katika fremu hiyo ya uingiliaji wa madola ya kibeberu katika eneo. Hivi sasa pia Marekani, Uingereza na NATO zinashirikiana na nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi kubadilisha muundo wa usalama katika eneo. Lengo la uingiliaji huo ni utekelezaji wa ramani mpya ya jiografia ya kisiasa Asia Magharibi.

Mpango huu unatekelezwa kwa misingi mitatu ya kile kinachodaiwa kuwa ni demokrasia, haki za binadamu na ugaidi. Ni kwa sababu hiyo ndio tukashuhudia kuongezeka ukosefu wa usalama katika eneo hili.

Mtaalamu wa masuala ya kisiasa John Tang anasema Kati ya nukta zinazoashiria uingiliaji wa madola ya kigeni katika eneo la Asia Magharibi ni hujuma ya Iraq dhidi ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979. Baada ya hapo tulishuhudia hujuma ya Iraq dhidi ya Kuwait na kisha hujuma ya Marekani dhidi ya Iraq. Hivi sasa nchini Syria na Iraq pia kunajiri vita ambavyo vinaashiria uingiliaji wa madola ya kigeni hasa Marekani

Migogoro ya nchi hizi mbili ni tishio na fursa kwa eneo la Asia Magharibi. Kuibuka ugaidi wa makundi ya wakufurishaji kama vile ISIS au Daesh ni jambo lililobadilisha mlingano wa kieneo. Ni wazi kuwa Marekani inahusika katika ugaidi huo kwani inaunga mkono makundi ya kigaidi. Kuna faili la sauti lililofichuka ambapo waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anasikika akisema Washington inatumai kuwa kundi la kigaidi la ISIS litachukua usukani Syria. Katika kikao cha siri na wapinzani wa serikali ya Syria, Kerry alisema:

"Marekani imeshuhudia ISIS ikiibuka na inatumai kuwa jambo hilo litamshinikiza Bashar Assad. Tunaweza kusimamia suala hili ili kumshinikiza Assad lakini ghafa hali imekuwa ngumu sana."

NATO yaizingira Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Kuongezeka majeshi ya Marekani, NATO na Uingereza katika nchi zinazopakana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jambo ambalo linapelekea kuwepo ulazima wa kuchunguza kwa kina sera za kijeshi zinazofuatwa na nchi za Magharibi chini ya NATO. Hivi sasa nchi za eneo hazina nafasi huru katika matukio ya eneo hili lilolojaa changamoto. Lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutegemea mantiki na busara ya kisiasa inalenga kuleta mlingano na imeweza kutumia mashirika ya kimataifa kukabiliana na sera za upande mmoja za Marekani na hivyo kufanikiwa kuwa na nafasi yenye taathira kieneo. Jitihada hizo za Iran zinajumuisha kushiriki katika vikao vya kimataifa na kuwasilisha mitazamo yenye kuashiria udharura wa kubadilishwa muundo wa Umoja wa Mataifa hasa baraza lake la usalama.

Mchambuzi wa masuala ya Iran Adnan Hussein Adnan anasema: "Iran ni nchi muhimu na yenye taathira katika Mashariki ya Kati na bila shaka nchi hii ina haki ya kuhusika katika kuleta mlingano wa kieneo na sio Marekani ambayo imekuja kutoka bara la mbali hadi katika maji ya Iran. Aidha Iran inalenga kuwa na uhusiano mzuri wa kisiasa na kiusalama na nchi jirani huku ikisimama kidete dhidi ya utumiaji mabavu wa Marekani."

Hivi sasa Iran pia inahesabiwa kuwa mojawapo ya nchi muhimu katika vita dhidi ya ugaidi ambao umeibuka katika eneo. Iran imekuwa na nafasi muhimu katika kusaidia utatuzi wa migogoro ya Iraq na Syria na imekuwa ikishirikiana na Russia katika jambo hilo hasa katika vita dhidi ya ugaidi Syria.Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu Mashariki ya Kati

Alki Morghulan mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Iran ni dola lenye nguvu katika eneo na ina nafasi muhimu katika utatuzi wa mgogoro wa Syria. Iran na Syria zina uhusiano mzuri na kwa msingi huo hakuna shaka Iran ina nafasi isiyopingika katika utatuzi wa mgogoro huo. Aidha Russia ina mtazamo unaokaribiana na wa Iran na hivyo ushurikiano wa nchi hizi mbili ni muhimu katika utatuzi wa migogoro ya eneo hasa nchini Syria."

Eneo la Mashariki ya Kati linakumbwa na migogoro mingi na kwa msingi huo ni jambo linalotarajiwa kwa Iran kuwa na nafasi muhimu katika eneo hili. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikizihimiza nchi za eneo ziwe na mshikamano na ushrikiano ili ziweze kuwa na nafasi katika maamuzi ya masuala ya eneo hili. Ili kukabiliana na nguvu na uwezo wa Iran, madola ya Magharibi yamekuwa yakiingilia mambo ya eneo. Pamoja na hayo imebainika kuwa matatizo ya eneo hayawezi kutatuliwa pasina kushiriki Iran na hata Marekani imekiri kuwa mgogoro wa Syria hauwezi kutatuliwa pasina kuwepo ushiriki wa Iran. Hali kadhalika Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya pia umesisitiza kuhusu nafasi ya Iran katika utatuzi wa masuala ya eneo.

Iran yaimarisha uthabiti katika eneo

Ukweli wa mambo ni kuwa, leo baada ya kupita zaidi ya miaka 38 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran imefikia uthabiti wa kisiasa na ni dola lenye taathira katika kuimarisha usalama na uthabiti wa kieneo.

Iran imeweza kuwa na nguvu pamoja na kuwa kwa muda mrefu imekuwa chini ya mashinikizo na vikwazo. Ni wazi kuwa ushirikiano mzuri wa Iran na nchi zenye taathira na nguvu kieneo kama vile Russia ni jambo ambalo limechangia nchi hii iwe na ushawishi mkubwa. Iran na Russia zimeungana na kukabiliana na sera za kibeberu za Marekani na ushirikiano huo umebainika vizuri nchini Syria.

Kwa mtazamo jumla, stratijia ya Iran Magharibi mwa Asia imejengeka katika msingi wa kuwepo usalama na uthabiti pamoja na ushirikiano mzuri wa nchi zote za eneo sambamba na kupinga satwa ya madola ya kibeberu duniani.

Iran inaamini kuwa changamoto zilizopo duniani zinapaswa kutatuliwa kwa kuwepo uwajibikaji sambamba na kuimarishwa nafasi ya Umoja wa Mataifa. Ni kwa msingi huu ndio Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikasisitiza kuimarisha uhusiano wake na Umoja wa Mataifa.


captcha